Wednesday, September 5, 2012
DK.MARY NAGU AENGULIWA KINYANG'ANYIRO CHA UJUMBE NEC
KILIMANJARO-TANZANIA,
Harakati za uchaguzi ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang'.
kwa mujibu wa taarifa kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na kanuni inayowataka wanachama wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea nafasi hiyo.
Imeelezwa kuwa licha ya baadhi ya wajumbe kujaribu kumtetea Dk Nagu bado hali ilikuwa ngumu baada ya wajumbe wengine wliozidi idadi kupinga suala hilo.
“Kikao kilikuwa kizito, lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na uwezo wa wagombea hasa katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alinukuliwa mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Mjumbe huyo aliongeza kuwa mapendekezo ya kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa uamuzi zaidi na baadaye yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
Huko Lindi mke wa Rais mama Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini huku akiwa hana mpinzani na hivyo kuwa na nafasi ya kupita moja kwa moja katika nafasi hiyo.
Labels:
habari mpya,
tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment