Tuesday, June 18, 2013

Arfi, Lissu watiwa mbaroni Arusha


ARUSHA-TANZANIA,Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jana kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana na vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea kwenye uwanja huohuo, Jumamosi iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa la kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa gari la Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa wamelazimika kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia shughuli za Chadema kwenye eneo lao.
Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua aliyosema imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja wa Soweto.
Mabomu yarindima
Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada ya polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja hapo yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu yalianza kurindima wakati Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.
“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya mabomu.

No comments:

Post a Comment