Nyumba aliyokuwa akiishi Osama bin Laden ambayo baadae ilibomolewa. |
Wake watatu wa Osama Bin Laden wamefikishwa mahakamani kwa kosa la Kuingia na kuishi nchini Pakistani kinyume cha sheria . Wanawake hao ambao wawili kati yao ni raia wa Yemen na mmoja wa Saudi Arabia ni miongoni mwa watu 16 waliokamatwa baada ya kikosi maalum cha Marekani kuvamia nyumba aliyokuwa akiishi Osama Bin Laden na familia yake katika mji wa Abbottabad nchini Pakistan mwezi mei mwaka jana wanashikiliwa na serikali ya Pakistan.
Kwa Mujibu wa waziri wa Mambo ya ndani ya Pakistan Bw.Rehman Malik wanawake hao tayari wamefunguliwa mashitaka katika mahakama ambayo hakutaka kuitaja kwa sababu za kiusalama na kuongeza kuwa wanahaki ya kumtafuta Wakili atakayewatetea katika kesi hiyo.
"Wamefikishwa mahakamani na baada ya hapo sheria ndio itakayoamua, hata hivyo kesi hiyo itawahusu wao pekee na watoto hawatoshitakiwa ....... Pia wanaweza kuwa na wakili na wana uhuru kamili wa kujitetea wenyewe mbele ya mahakama"
Waziri huyo hakutaja ni adhabu gani ambayo itawakabili wanawake hao endapo watapatikana na hatia ingawa kwa Mujibu wa Sheria za Pakistan wanaweza kukabiliwa na kifungo cha Hadi Miaka kumi (10) na faini ya dola 110 kila mmoja.
Hatima ya Watoto?
Kuhusu hatima ya watoto Bw.Malik amesema wamewekwa katika nyumba salama yenye vyumba vitano (5) vya kulala na wanapata mahitaji na haki zote kama nyumbani na wataweza kurudishwa katika nchi zao ikiwa mama zao watakubali.
No comments:
Post a Comment