DAR ES SALAAM-TANZANIA,
KONDOMU zinazodaiwa kuwa ni bandia ambazo zilipigwa marufuku nchini Uingereza kutokana na kubainika kuwa hazina ubora unaotakiwa, zimetapakaa katika maduka mbalimbali ya dawa nchini, Mwananchi limebaini.
Kondomu hizo ni Durex na Trojan ambazo zina vipele na uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa zinauzwa katika maduka mbalimbali ya dawa kwa bei ya Sh5,000.
Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ya Uingereza ilifanya msako mkali kwa lengo la kukamata mamilioni ya kondomu hizo, wakati ambao ilikuwa imepita takriban miezi 18 tangu zilipokuwa zimeingizwa nchini humo.
Mdhibiti wa Dawa na Bidhaa za Afya wa Uingereza alinukuliwa akisema kuwa mamilioni ya kondomu hizo feki ziliingizwa kutokea Mashariki ya Mbali na kwamba tayari zilikuwa zimetumiwa na idadi kubwa ya watu.
Kondomu hizo zinadaiwa kutokuwa na ubora hali inayoweza kuongeza hatari kwa watumiaji kwa kusambaza kwa kasi magonjwa ya zinaa, virusi vya Ukimwi au kusababisha mimba zisizohitajika, hivyo kuharibu mikakati ya uzazi wa mpango.
Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza akizungumza na gazeti hili jana, alithibitisha kuwapo kwa taarifa za kondomu hizo za Durex na Trojan na kuongeza kuwa mamlaka hiyo imewaagiza wakaguzi wake kuzichunguza ili kubaini kama zina ubora ama la.
“Wakaguzi walichukua sampuli ya kondomu hizo kwa lengo la kuzichunguza, nipe muda kidogo ili nizungumze na mkurugenzi ili kujua uchunguzi ule umefikia wapi,” alisema Simwanza.
Alipotafutwa baadaye alibainisha kwamba uchunguzi wa sampuli hiyo bado upo maabara na kwamba majibu yake hayajatoka. Hata hivyo hakusema ni lini yatatolewa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Leandri Kinabo aliomba apewe muda ili afuatilie kujua ni kondomu za aina gani zilizowahi kukamatwa na kupigwa marufuku zisitumike.
“Nipe muda kidogo nifuatilie ili kujua zilizopigwa marufuku na ambazo tulizizuia kuingizwa nchini, nitafute mchana,” alisema Kinabo ambaye alipotafutwa baadaye alisema yuko kwenye kikao na kwamba alikuwa hajaweza kuwasiliana na watu wa maabara.
Hii siyo mara ya kwanza kuibuliwa kwa taarifa za kuwapo kwa kondomu feki nchini, kwani Desemba 20, mwaka jana kontena lililosheheni kondomu za kiume aina ya Melt Me kutoka nchini India lilikamatwa na kuzuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya kubainika kuwa hazifai kwa matumizi.
Maofisa wa TBS walilazimika kufanya msako katika baadhi ya maduka ya dawa jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kuziondoa kondomu hizo katika soko.(MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment