Monday, May 20, 2013
NGASA ARUDI YANGA.
DAR ES SALAAM-TANZANIA, Mshambuliaji wa Azam, Mrisho Ngasa, aliyekuwa akiitumikia klabu ya Simba kwa mkopo, na ambaye mkataba wake na Azam unamalizika leo, amesema kwamba ameamua kurejea kwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga kwa sababu ndiyo klabu anayoipenda na kwamba kwingine alikuwa akienda kutafuta riziki kama mchezaji.
Ngasa aliibusu jezi ya Yanga wakati akitambulishwa mbele wa waandishi wa habari jana kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo kwenye kona ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo jijini Dar es Salaam na akasema kwamba amesaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili.
Licha ya uongozi wa Yanga na mchezaji kuficha dau alilosaini, inadaiwa nyota huyo amepewa fedha na gari jipya aina ya Nissan X-Trail.
Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi, Ngasa ambaye pia ni tegemeo kwenye timu ya Tanzania (Taifa Stars), alisema kuwa ana furaha na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha yeye kurejea Yanga baada ya kuondoka kwa kipindi cha miaka miwili.
Ngasa alisema kuwa anawashukuru mashabiki wake ambao walikuwa wanamsapoti wakati wote alipokuwa Azam na hata alipotua kwa mkopo kwa watani zao Simba.
"Ni kweli naipenda Yanga na nawashukuru viongozi wangu (Yanga) kwa kufanikisha mimi kurejea tena katika timu hii, nawashukuru pia mashabiki wangu ambao walikuwa wakinishangilia nilipokuwa Azam, Simba nilienda kikazi na naamini nimeisaidia kufika hapo ilipo," alisema Ngasa.
Alimaliza kwa kuukana mkataba wa mwaka mmoja aliosaini wakati anatambulishwa kujiunga na Simba na kueleza kuwa haiwezekani kusaini mkataba juu ya mkataba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Binkleb, alisema kuwa wanamkaribisha mchezaji huyo nyumbani na wamefurahi kwa ujio huo ambao umekamilisha mazungumzo ya miezi sita waliyofanya naye.
Binkleb alisema kwamba wamemsajili nyota huyo kwa sababu ameonyesha yeye ni mchezaji wa kimataifa kwa kutumikia kwa kiwango cha juu klabu za Azam na Simba licha ya kuwa na mapenzi na Yanga.
"Ngasa ameonyesha uaminifu akiwa Azam na Simba, na bila yeye Simba isingeweza kumaliza ya tatu labda ingemaliza ya tano au sita kwenye msimamo," alimaliza.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na katibu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala, kwa nyakati tofauti jana walisema kwamba Ngasa ni mchezaji wao halali na mkataba aliosaini walienda kuusajili katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Rage alisema sasa wanasubiri kuona kama Simba itatendewa haki au watanyang'anywa haki hiyo kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa beki, Kelvin Yondani aliyehamia Yanga.
Ofisa wa TFF, ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema kwamba ni kweli Simba ilipeleka mkataba wa Ngasa katika shirikisho hilo lakini umekosewa.
"Inakubalika kumsainisha mkataba mchezaji lakini ni lazima ionyeshwe kwamba utaanza kutumika baada ya mkataba wa sasa, lakini Simba wamekosea katika hilo," alisema ofisa huyo.
Kusajiliwa kwa Ngasa katika klabu hiyo, kumeendeleza neema ya kimapato ya nyota huyo ambaye wakati alipouzwa na Yanga kwa Sh. milioni 58 kwenda Azam FC Mei 2010 aliripotiwa kupewa mkononi Sh. milioni 40 na alipopelekwa kwa mkopo Simba Agosti 2012 alipewa gari aina ya Toyota Verossa pamoja na Sh. milioni 12.
Wakati akipelekwa kwa mkopo Simba, Wekundu hao walipewa na Azam sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngasa mshahara wake kamili (Sh.milioni 2 kwa mwezi) pamoja na stahiki zake nyingine zote za kimkataba.(IPP MEDIA)
Labels:
habari mpya,
michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment