Friday, February 28, 2014

BENKI YA DUNIA YAISIMAMISHIA UGANDA MSAADA-Ni matokeo ya kura ya kupinga ushoga.

Benki ya dunia imesitisha mkopo wa dola milioni 90 kwa Uganda wa kuimarisha sekta ya afya kufuatia kupitishwa kwa sheria inayoharamisha ushoga na kutoa adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia
Hatua hiyo ya benki ya dunia haikutarajiwa na wengi kwani taasisi hiyo mara nyingi hujiepusha kuingilia masuala ya ndani ya kisiasa ya nchi wanachama au kuhusiana na masuala kama haki za mashoga, kuepuka kuzishurutisha nchi wanachame wake 188.
Hata hivyo msemaji wa benki hiyo David Theis amesema katika barua pepe kuwa wamesitisha mradi huo wa kuboresha sekta ya afya ya Uganda hadi watakapoufanyia tathmini na kuhakikisha malengo yake ya maendeleo hayataathiriwa na sheria hiyo mpya ya kuharamisha ushoga.
Rais wa benki hiyo Jim Yong Kim amewatumia wafanyakazi wake barua akisema benki ya dunia inapinga ubaguzi na itawalinda wafanyakazi wake wote na kuongeza kupitishwa kwa sheria hiyo ya Uganda sio nchi ya kwanza kufanya hivyo kwani ushoga umeharamishwa katika nchi 83 na zaidi ya nyingine 100 zinawabagua wanawake.
Mkopo ulikuwa uimarishe sekta ya afya
Licha ya kusimamishwa kwa mkopo huo wa dola milioni 90,benki ya dunia bado ina miradi mingine nchini Uganda ya kiasi cha dola bilioni 1.56. Mkopo huo ulitarajiwa kuidhinishwa hapo jana na ulipaswa kuangazia miradi ya kuboresha afya ya uzazi,afya ya watoto wachanga na uzazi wa mpango
Kutiwa saini kwa sheria hiyo ya kuharamisha ushoga Uganda na Rais Yoweri Museveni mapema wiki hii kumeibua shutuma kali kutoka kwa nchi za magharibi na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Norway,Denmark na Uholanzi zimetangaza kuwa zitasitisha misaada kwa serikali ya Uganda kutokana na sheria hiyo na nchi nyingine wafadhili ikiwemo Marekani pia zimetishia kusitisha misaada na kutafakari upya uhusiano kati yao na Uganda.
Ghadhabu hiyo ya nchi za magharibi kuhusu kuharamishwa kwa ushoga ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani kwa watakaokutikana na hatia imeporomosha thamani ya shilingi ya Uganda na kusababisha Benki nchini humo kuingilia kati kwa siku mbili mfululizo
Kutiwa saini kwa sheria hiyo ya kuharamisha ushoga Uganda na Rais Yoweri Museveni mapema wiki hii kumeibua shutuma kali kutoka kwa nchi za magharibi na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Norway,Denmark na Uholanzi zimetangaza kuwa zitasitisha misaada kwa serikali ya Uganda kutokana na sheria hiyo na nchi nyingine wafadhili ikiwemo Marekani pia zimetishia kusitisha misaada na kutafakari upya uhusiano kati yao na Uganda.
Ghadhabu hiyo ya nchi za magharibi kuhusu kuharamishwa kwa ushoga ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani kwa watakaokutikana na hatia imeporomosha thamani ya shilingi ya Uganda na kusababisha Benki nchini humo kuingilia kati kwa siku mbili mfululizo
Serikali ya Uganda haina wasiwasi
Hata hivyo msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amesema Uganda inaweza kujiendeleza bila ya misaada kutoka nchi za magharibi na kuongeza Uganda haina wasiwasi na hatua hizo kwani ni wakati kwa Afrika kupinga ukoloni, utumwa na ubabe kutoka magharibi.
Mwanaharakati ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuwatetea mashoga nchini Uganda Frank Mugisha alikutana na maafisa wa ngazi ya juu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani mjini Washington hapo jana kuomba usaidizi utakaowalinda mashoga.
Ofisi ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa umelaani kuchapishwa kwa majina ya watu wanaodaiwa kuwa mashoga nchini Uganda katika gazeti moja la udaku nchini humo na kuonya hatua hiyo inakiuka haki ya kuwa na faragha na kuonyesha wazi kuwa maisha ya mashoga yamo hatarini.
Kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye ameishutumu serikali kwa kutumia suala hilo kuwahadaa raia wa nchi hiyo ili wasiangalie masuala muhimu kama ufisadi au kuwepo kwa jeshi la Uganda Sudan Kusini.(E.L)

Thursday, February 27, 2014

Homa ya nguruwe yalipuka tena Mbeya

 
Ugonjwa wa homa ya nguruwe umelipuka tena mkoani Mbeya na kuua zaidi ya nguruwe 900 katika wilaya za Mbeya na Rungwe.

Mganga Mkuu wa Mifugo Mkoani Mbeya, Solomon Nong'ona akizungumza na NIPASHE jana alisema, ugonjwa huo umerudi tena baada ya kuzuka kwa mara ya kwanza Januari mwaka huu na kutokomezwa.

Alisema kufuatia kuzuka tena kwa ugonjwa huo, serikali kupitia sekta ya mifugo imepeleka dawa mkoani humo ambazo zinasaidia kupunguza kasi ya kuenea.

Nong'ona  alisema kufuatia kuzuka kwa ugonjwa huo wananchi nao wanajitahidi kununua dawa hizo ili kuudhibiti na kuwakinga nguruwe wanaowafuga.

Alisema ugonjwa wa homa ya nguruwe  bado haijathibitika kuwa na madhara kwa binadamu, hivyo wananchi wanaruhusiwa kula nyama ya nguruwe lakini aliyechinjwa katika machinjio rasmi na kuthibitishwa na daktari wa mifugo.

"Nguruwe hawa wanaweza kuliwa lakini wananchi wawe waangalifu kula nyama hizo kwani kula myama ambaye amekufa mwenyewe ni hatari kwani huenda amekufa kwa ugonjwa mwingine," alisema Nong'ona.

Alisema ugonjwa huo ulianza katika wilaya ya Mbeya na baadaye katika wilaya ya Rungwe.
CHANZO: NIPASHE

Monday, February 24, 2014

Milipuko ya mabomu yarindima Z’bar


Zanzibar. Watu wanne wamejeruhiwa baada ya milipuko minne inayoaminika kuwa ni mabomu kutokea katika maeneo matatu tofauti Zanzibar.
Katika moja ya matukio hayo, watu wanne walijeruhiwa, mmoja akikatika mguu, katika eneo la Unguja Ukuu, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Mkoa wa Kusini Unguja, Hamad Said Masoud alisema mlipuko wa kwanza ulitokea juzi katika eneo la Fuaoni Maili Nne wakati watu wasiojulikana waliporusha kitu kinachoaminika kuwa ni bomu wakati waumini wa Kanisa la Evangelist wakiendelea na ibada ya Jumapili.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema tukio la juzi, kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kilirushwa wakati waumini wa kanisa hilo wakiendelea na ibada na kutoa mlipuko na kishindo kikubwa. Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo, milipuko mingine mitatu ilitokea jana.
Katika mlipuko wa kwanza kwa jana uliotokea saa 6.30 mchana katika kituo kimoja cha fundi vyuma aliyetambulika kwa jina la Juma Abdallah huko Unguja Ukuu ndiko kulikokuwa na watu waliojeruhiwa.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Pandu Haji Pandu aliyekatika mguu na Shaaban Khamis Ibrahim ambaye aliumia sehemu za kiuno.
Hamad alisema mtu mmoja aliokota chuma kizito na kukipeleka kwa fundi akitaka atengenezewe nanga kwa ajili ya uvuvi.
Alisema mhunzi huyo alipokea kazi hiyo na alipokuwa akijiandaa kwa matengenezo ndipo mlipuko huo ulipotokea. Mlipuko huo ulitokea sambamba na mwingine katika Mgahawa wa Mercury’s uliopo Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha huduma za chakula kusitishwa kwa muda.
Tukio la mwisho lilikuwa saa 7:15 mchana katika Kanisa la Anglikana, Mkunazini. Katibu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Zanzibar, Nuhu Saranya alisema: “Nilisikia kishindo cha mlipuko, wakati nikitafakari ni kitu gani hicho, nikasikia mlipuko wa pili nje ya kanisa letu,” alisema.
Mmoja wa majeruhi, Mohamed Ibrahim alisema hakujua kilichotokea huku akilalamika kuwa masikio yake hayasikii vizuri kutokana na kishindo hicho.

Friday, February 21, 2014

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE-WASICHANA WATESA-LINK HII HAPA.

Watahiniwa wa kike wamefanya vizuri kwa kuchukua nafasi saba kati ya 10 za juu, huku Shule ya Marian Girls ya Pwani ikiongoza kwa kuwa na wanafunzi wanne.
Mwanafunzi aliyeongoza ni Robina Nicholaus wa Shule ya Marian Girls, akifuatiwa na Magrath Kakoko wa St Francis (Mbeya) wakati wa tatu ni Joyceline Marealle kutoka Shule ya Canossa (Dar es Salaam).
Wengine ni Safarina Mariki na Abby Sembuche wa Marian Girls, wakati wavulana pekee kwenye wanafunzi 10 bora ni Sunday Mrutu kutoka Anne Marie (Dar es Salaam) na Nelson Rugola Anthony na Emmanuel Mihuba Gregory wa Kaizirege (Kagera).
Wanaofuata ni Janeth Urassa kutoka Marian Girls (Pwani) na Angle Ngulumbi wa St Francis (Mbeya).
Wasichana 10 bora
Wasichana waliofanya vizur kwenye mtihani huo wameongozwa na Robina Nicholaus (Marian Girls), Magrath Kakoko (St Francis), Joyceline Leonard Marealle (Canossa), Safarina W Mariki, Abby T Sembuche na Janeth Urassa (Marian Girls).
Wengine ni Angle Ngulumbi (St Francis), Getrude James Mande wa Precious Blood (Arusha), Violet Mwasenga wa St Francis na Catherine Swai kutoka Marian Girls.
Wavulana 10 Bora
Wavulana waliofanya Vizuri ni Sunday Mrutu wa Anne Marie, Nelson Rugola Anthony na Emanuel Mihuba Gregory wote kutoka Kaizirege, Razack Hassan wa St Matthew’s (Pwani) na Hamis Msangi kutoka Eangles (Pwani).
Wengine ni Joshua Zumba wa Uwata (Mbeya), Brian Laurent na Mohamed Ally wa Marian Boys (Pwani), Shahzill Msuya wa St Amedeus (Kilimanjaro) na Shabani Hamisi Maatu wa Mivumon Islamic Seminary (Dar es Salaam).

KAMPENI BUNGE LA KATIBA ZAANZA CHINICHINI-Sitta na Membe wahusishwa.


Dodoma,
Wakati ratiba ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba, ikitarajiwa kutangazwa rasmi siku ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo, jana baadhi ya wajumbe walikuwa wakifanya kampeni za wazi ndani ya Ukumbi wa Bunge. Ratiba ya uchaguzi ilitarajiwa kutangazwa jana jioni na ingeonyesha ni lini Rais Jakaya Kikwete, atalizindua bunge hilo na kuelezea siku kamili ya uchaguzi wa viongozi wake.


Ndani ya ukumbi jana, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), alionekana akizungumza na wajumbe, jambo ambalo baadhi ya watu wamelitafsiri kuwa ni kufanya kampeni. Chenge ni mmoja wa makada wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.


Mwingine anayetajwa ni Mbunge wa Urambo Mashariki ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.


Wakati Chenge akiendelea na kampeni zake, Sitta alitumia muda mwingi kuzungumza na wajumbe ambao wengi walikuwa wakimfuata mahali alipoketi na baadaye, alionekana akiwazungukia wajumbe.


Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde, alisema hana jambo lolote la kufanya juu ya mapenzi yake kwa Sitta kwani ndiye anayeweza kuendesha shughuli hizo.


“Mimi Lusinde, kwa mapenzi yangu kabisa nasema kuwa kama jina la Sitta litachomoza basi lazima nimsaidie kuhakikisha anakalia kiti hicho kwa kuwa naona anaweza kuliko wengine,” alisema Lusinde.


Alisema kuwa bunge hilo limesheheni wataalamu wa sheria waliobobea na ambao kila mmoja anaweza kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu, lakini akasisitiza kwamba kwa kuwa anayetakiwa ni mmoja basi angetamani nafasi hiyo imwendee Sitta.


Mjumbe mwingine kutoka katika Bunge la Muungano ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa kumchagua Sitta ni sawa na kumsaliti Chenge ambaye ni jirani yake na wanakaa viti karibu bungeni.

Chanzo:Mwananchi.

Wednesday, February 19, 2014

LOWASSA NA WENZAKE WATIWA KITANZINI-WAFUNGIWA KUGOMBEA UONGOZI CCM.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza uamuzi mzito dhidi ya wanachama wake sita ambao hivi karibuni waliitwa na Kamati Ndogo ya Maadili na kuwahoji kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2015.
CCM imewatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, hivyo kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wanachama hao wote sita walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya wakati jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo kali. Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za chama hicho inamaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha,” alisema Nnauye.
Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo hao, kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote watakuwa wakichunguzwa mienendo yao.
Nnauye alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni za kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema Nnauye.
Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali.”
Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.
Nnauye alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
CHANZO:MWANANCHI.

BUNGE LA KATIBA VITUKO TUPU.

Mh.Pandu Amir Kificho

MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, jana alinusuru mchakato wa uchaguzi wa mwenyekiti wa muda baada ya kuibuka vituko.
Mbowe katika ushauri wake alitaka mchakato huo uanze upya kwa karatasi za kura kugawiwa kwa utaratibu makini ili kila mmoja apige kura huku milango ikiwa imefungwa.
Ushauri wake ulikubaliwa na mwenyekiti wa kikao hicho ambapo mchakato ulifanyika upya kwa usimamizi mkali wa polisi, huku Bunge likiahirishwa kwa robo saa kutoa fursa ya kura kuhesabiwa.
Awali vituko kejeli na malumbano vilitawala zaidi uchaguzi huo wa Bunge lililoanza vikao vyake jana mkoani hapa.
Dalili za kuvurugika kwa uchaguzi huo zilianza kuonekana mapema kutokana na idadi kubwa ya wajumbe kusimama na kuwasha vipaza sauti bila kufuata taratibu walizoambiwa mapema.
Katika uchaguzi huo Mheshimiwa Pandu Amir Kificho alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba baada ya kupata kura 393 sawa na 69.19% ya kura 558 zilizopigwa na kuwaacha kwa mbali Costa Mahalu na Magdalena Rwebangira ambao wamepata kura 84 kila mmoja ambazo ni sawa na 14.79%
Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba, mwenyekiti huyo wa muda atakuwa na jukumu la kuandaa na kupitisha kanuni za Bunge hilo zitakazotumika katika mijadala mbalimbali.