Monday, December 10, 2012

JOHN DRAMANI NDIYE RAIS MPYA GHANA



ACCRA-GHANA,Tume ya uchaguzi nchini Ghana imemtangaza rais John Dramani Mahama mshindi wa uchaguzi wa urais  baada ya kupata ushindi wa asilimia 50 nukta 7 na kumshinda mpinzani wake Nana Akufo Addo aliyepata asilimia 47 nukta 7.

Ushindi wa Mahama wa asilimia 50 umeepusha zoezi hilo kuingia katika duru ya pili katika uchaguzi huo ambao asilimia 80 ya wapiga kura walijitokeza kupiga kura.
Licha ya tume hiyo ya uchaguzi kumtangaza Mahama kuwa mshindi, upinzani umepinga matokeo hayo na kusema kura ziliibiwa na zoezi hilo halikuwa huru na haki.
Upinzani umeongeza kuwa matokeo yaliyotangazwa hayaoneshi sauti ya watu wa Ghana na viongozi wa upinzani wa chama cha NPP watakutana siku ya Jumanne kujadili mustakabali wa uchaguzi huo.

Hali ya wasiwasi imeendelea kushuhudiwa jijini Accra huku kukiwa na hofu ya wafuasi wa upinzani kuzua fujo kupinga ushindi wa rais Mahama, wakati waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na wale wa Kimataifa wakisema zoezi hilo lilikuwa huru na haki.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, rais Mahama ametoa wito kwa upinzani kukubali matokeo hayo aliyoyasema yanaonesha sauti ya wananchi wengi wa Ghana.
Mahama mwenye umri wa miaka 54 awali alihudumu kama Makamu wa rais kabla ya kuwa rais kwa muda, baada ya kufariki kwa rais John Atta Mills mwezi wa Saba mwaka huu.

Naye kiongozi wa upinzani Akufo Addo mwenye umri wa miaka 68 ni wakili wa maswala ya haki za binadamu na mtoto wa rais wa zamani wa nchi hiyo na itakumbukwa pia mwaka 2008 alishindwa kwa chini ya asilimia 1 katika uchaguzi huo.

Wafuasi wa rais Mahama wameendelea kusherehekea katika sehemu mbalimbali nchini humo  kuanzia usiku wa Jumapili  baada ya kiongozi wao kutangazwa mshindi.(CHANZO:GHANAWEB,RFI)

No comments:

Post a Comment