Thursday, December 6, 2012

JAJI BOMANI AWAKOSOA POLISI


DAR ES SALAAM-TANZANIA,KUJIRUDIA kwa matukio ya polisi kutumia silaha za moto dhidi ya raia, kumepokewa kwa hisia tofauti, huku Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Serikali, Jaji Mark Bomani akilitaka jeshi hilo kuacha kutumia nguvu wanapokuwa katika operesheni zao.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu tukio la hivi karibuni la kupigwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, watu wa kada mbalimbali walisema, kitendo cha polisi kutumia nguvu sio busara.
Jaji Bomani kitendo cha polisi kutumia nguvu badala ya busara katika operesheni zao kinaweza kuleta uhasama kati ya wananchi na jeshi hilo.
“Kwa ujumla matumizi ya nguvu kwa polisi si mazuri  na nadhani tunatakiwa kubadilika katika hilo.” alisema Jaji Bomani.  
Bomani alieleza kuwa  kwa ujumla polisi wanatumia vibaya silaha zao ingawa bado hajapata uhakika wa jinsi  tukio la kujeruhiwa kwa Matutu lilivyokuwa .
Alisema tukio la Mwangosi lilikuwa baya zaidi lakini picha anayoiona na kuihusisha na tukio la juzi, ni kuwa kuna matumizi mabaya ya mashambulizi ya polisi kwa raia.
Hata hivyo wakati Jaji Bomani akieleza hayo Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Ramadhan Manento  alisema kila tukio linalofanywa na polisi linatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuanza kulizungumzia.
Jaji Manento alisema akiwa ni mwanasheria hawezi kutoa hitimisho ya tukio la kujeruhiwa kwa Matutu kabla ya uchunguzi wa kisheria kufanyika.
“Tunahitaji kujua mambo mengi, ya michakato ya makosa ya jinai, (criminal procedure) kwa mfano polisi walipoingia walifanya nini, walipotoka, ni maneno gani walimuuliza mtu wa kwanza waliyekutana naye.
Tunahitaji kujua iwapo walitumia kizuizi cha usalama(safe cage) katika silaha zao au la” alisema Jaji Manento
Alisema kulingana na taarifa zilizopo katika magazeti bado unahitajika uchunguzi wa kujua  ni namna gani polisi waliingia ndani ya nyumba hiyo.
Aidha Jaji huyo mstaafu alisema hawezi kuwahukumu polisi moja kwa moja kwani hakuna ushahidi kuwa walikuwa wakimwinda mwandishi, bali inawezekana waligundua kuwa ni mwandishi baada ya kumjeruhi.(CHANZO:MWANANCHI).

No comments:

Post a Comment