Saturday, December 15, 2012

MAREKANI KUTUMA MAKOMBORA UTURUKI



WASHINGTON-MAREKANI, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panneta ameagiza kutumwa kwa makombora  katika mpaka wa Uturuki na Syria pamoja na wanajeshi 400 kuilinda Uturuki dhidi ya uvamizi wa kijeshi kutoka  Syria.

Hatua hiyo pia imeungwa mkono na muungano wa majeshi ya Mataifa ya Magharibi NATO, baada ya Uturuki kuomba msaada huo ili kujilinda.

Panneta amesema makombora hayo yanatarajiwa kuwekwa katika mpaka huo katika siku chache zijazo ili kuisadia Uturuki ambayo ni washirika wake wa karibu.
Mataifa ya Ujerumani na Uholanzi pia yamekubali kuleta makombora yake ili kuisaidia Uturuki katika uvamizi wowote kutoka Syria.
Hii inakuja siku chache baada ya wasiwasi kuzuka kuwa serikali ya Syria inapanga kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake na pia kulenga jirani zao Uturuki ambao wameendelea kushinikiza kujiuzulu kwa rais Bashar Al Assad.
Kwingineko,Urusi imekanusha habari zilizotolewa siku ya Alhamisi na Naibu Waziri wa Mambo ya nje Mikhail Bogdanov kuwa waasi wanaelekea kuwashinda wanajeshi wa serikali.
Wizara ya mambo ya nje nchini humo imesisitiza kuwa matamshi ya Bogdanov hayakumaanisha kuwa sera na msimamo wa Urusi imebadilika kuhusu rais Bashar Al Assad ambaye wataendelea kumuunga mkono.
Marekani ilikuwa imepongeza mtazamo huo wa Urusi kwa kile walichokisema kuwa nchi hiyo ilikuwa sasa inatambua kinachoendelea nchini humo na kuanza kubadilisha msimao wake.

Mapigano kati ya wapiganaji wa upinzani na majeshi ya serikali ya Syria yameingia katika mwaka wake wa pili na kusababisha zaidi ya vifo vya watu elfu 40.(CHANZO:RFI)
 

No comments:

Post a Comment