Friday, March 1, 2013

GHARAMA ZA SIMU KUSHUKA KUANZIA LEO

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj7fdrp-Z-VFJkJ0kPpmt89ZnxyvBi1oulN2nW8mK1hguM5dtc_gs3vnwQxcRl6imdeUUjOmBnwZyyPUuzWuPIC18OCfqvr6x1sKcXrpPhU8dFcWCsUjL6MIsKg-vt3OLJseKTYv9djPJQ/s1600/Mwenyekiti+wa+Kamati+ya+Nishati+na+Madini+January+Makamba+akizungumza+na+waandishi+kuhusu+mipango+ya+kamati+yake+kuangalia+tat.jpgDAR ES SALAAM-TANZANIA,
GHARAMA za kupiga simu kutoka mtandao wa kampuni moja ya simu za mkononi kwenda mwingine nchini, zinatakiwa kushuka kuanzia leo kutoka Sh 115 hadi Sh 34.92 kwa dakika huku gharama za mwingiliano kwa kampuni zote zikiwa sawa.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi uliofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya kufanya mapitio ya gharama za mwingiliano kwa kampuni za simu nchini wa mwaka 2013.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema ni jambo nzuri kupunguza gharama hizo.
Alisema mwaka 2008 hadi 2009 baada ya kujengwa Mkongo wa Taifa, bei za simu zilipungua, lakini za muingiliano zilibaki kama zilivyokuwa.
Alisema huo ni mwanzo na wataendelea kupunguza gharama hizo kila mwaka, kwani dhamira ya Serikali ni gharama ya mwingiliano kubakia sifuri na wananchi kubaki wakigharimia kupiga simu.
Alisema ili kuhakikisha punguzo hilo linafika kwa wateja, kuanzia mwezi Juni mwaka huu watajenga mtambo wa kufuatilia mfumo wa mawasiliano nchini.
Makamba alisema mtambo huo, pia utahakikisha kampuni za simu zinatoa huduma zenye ubora, kama kudhibiti kukatika kwa simu na kutopatikana ili kampuni hizo zichukuliwe hatua.
Alisema kwa hatua ya leo, inadhihirisha sekta ya mawasiliano imepiga hatua kubwa kwani Watanzania watapata thamani ya mawasiliano huku Serikali ikipata mapato na kuondoa malalamiko.
Wakizungumzia kupungua kwa gharama hizo, Meneja Mawasiliano wa Airtel , Jackson Mbando alisema wataanza kutekeleza maagizo hayo kama Mdhibiti wao alivyoagiza.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya simu ya TTCL, Amini Mbaga alisema wanafurahi Watanzania kupata punguzo hilo, kwani wao walikuwa wadau wa kwanza kupeleka ombi hilo TCRA.
Alitaka Kampuni za simu kuangalia biashara na upande wa wananchi kwani mawasiliano yao kwa ajili ya kuleta maendeleo, lakini gharama kubwa za mawasiliano zinaweza kupunguza maendeleo kwa wananchi hivyo kuwataka kuacha kufanya biashara kwa kutaka kuvuna.

No comments:

Post a Comment