Thursday, March 28, 2013

POLISI WANAFUGA UHALIFU VURUGU ZA KIDINI-PENGO

DAR ES SALAAM-TANZANIA, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku akisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”
“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”". "
- Polycarp Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.

“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na kuongeza:

“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”

Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”
Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la amani.”
Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.

Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.

“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.

“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.

Polisi wanena
Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.

Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.

Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Mwanakwerekwe.

Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.(MWANANCHI).

No comments:

Post a Comment