Thursday, March 14, 2013

PAPA MPYA APATIKANA-MATUKIO KATIKA PICHA

Papa Mpya Jorge Bergoglio





Papa Francis akijitokeza mbele ya umati wa waumini Vatican na kuwabariki.



ROME-ITALIA,
HATIMAYE Kanisa Katoliki duniani, limemchagua Kardinali Jorge Bergoglio kuwa Papa mjini Rome nchini Italia jana. Papa huyo kutoka Argentina, alichaguliwa jana baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kutokana na aliyekuwa akiishikilia, Papa Benedict XVI kujizulu nafasi hiyo, Februari 28 mwaka huu.

Dalili za kupatikana kwa papa huyo, zilitanguliwa na moshi mweupe uliofuka kutoka mnara wa paa la Kanisa dogo la Sistina, Vatican mjini Rome Italia jana usiku ukiitangazia dunia kwamba makardinali waliokusanyika ndani ya kanisa hilo wamemchagua papa mpya wa kuliongoza kanisa hilo. Umati wa watu ukiwa na miavuli, uliujaza uwanja huku ukipeperusha bendera za mataifa mbalimbali duniani.
Baada ya saa kadhaa za kukabiliana na baridi kali na mvua kubwa, umati mkubwa ulipaza sauti za kushangilia tukio hilo ‘Habemus Papam’ na ‘Tuna papa’ huku kengele za Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na za makanisa mengine ya mjini Rome zikilia.

Ndani ya saa moja baadaye mrithi wa Papa Benedict XVI akafahamika kuwa ni Askofu Mkuu wa Buenos Aires nchini Argentina, Jorge Mario Bergoglio, ambaye amechagua jina la Papa Francis I.

Uchaguzi wa papa huyo mpya wa 266 mwenye umri wa miaka 76 na ambaye anakuwa papa wa kwanza asiyetoka barani Ulaya na wa tatu asiye Muitaliano, ulipokelewa kwa shangwe kubwa na makumi kwa maelfu ya Wakatoliki katika viwanja hivyo vya Mtakatifu Petro.

Alipojitokeza katika kibaraza cha kanisa hilo, papa mpya alianza hotuba yake kwa utani, akisema kaka zake makardinali wamekusanyika kumchagua Askofu wa Rome na kwamba wameshamchagua mmoja wao kutoka mbali ambaye ni yeye.

Kisha akasali kumuombea mtangulizi wake ambaye bado yu hai yaani Papa Benedict XVI.

Katika maneno yake, alisema, “Kwanza kabisa napenda kumuombea Papa wetu mstaafu Benedict XVI, kwamba Kristo na Bikira Maria wawe naye.

“Tuwe katika safari hii pamoja, safari hii kwa Kanisa la Roman Katoliki ni safari ya urafiki na upendo na imani baina yetu, tuombeane kila mmoja wetu, tuwaombee wote duniani,” alisema Papa Francis.

Baada ya kusema hayo, akautaka umati kukaa kimya kwa muda na kumuombea wakati akikubali kupokea wadhifa huo mpya kwake.

“Naomba mniombee kwa Mungu ili anibariki,” Papa Francis alisema, akiongoza sala ya kimya kimya, akifuatiwa na vifijo kutoka kwa umati wa watu.

Pia alisema dunia inapaswa kuonyesha njia ya upendo na mtangamano na wakati akiondoka aliuambia umati huo, kwamba usiku mwena na ninawatakia mapumziko ya amani.

Papa Francis anazungumza kwa ufasaha lugha za Kijerumani, Kihispania na Kiitaliano.

Makardinali 115 walikuwa wakikutana kwa siku ya pili jana kumchagua mrithi wa Papa Benedict XVI, ambaye uamuzi wake wa mwezi uliopita wa kutangaza kujiuzulu uliwashangaza wengi baada ya kushikilia wadhifa huo kwa miaka minane.

Uamuzi huo pia ulimfanya Papa Bebedict XVI aweke rekodi ya kuwa papa wa kwanza kujiuzulu katika miaka 600 ya historia ya Kanisa Katoliki.

Makardinali 115 walikuwa wamejitenga na dunia tangu Jumanne wiki hii na tangu kipindi hicho, walikuwa wamepiga kura mara nne ambapo moshi mweusi ulijitokeza ukiashiria papa bado hajapatikana.

Theluthi mbili au sawa na makardinali 77 miongoni mwao, walikuwa wakitakiwa wawe wamemchagua mmoja miongoni mwao ili awe kiongozi wa kanisa hilo.

Kabla ya mkutano huo maalumu maarufu kama conclave kuanza, kulikuwa hakuna mtu aliyekuwa akitajwa kupewa nafasi kubwa ya kumrithi Papa Benedict XVI.

Pamoja na Papa Francis I kushika wadhifa huo, anakabiliwa na wakati mgumu katika kipindi ambacho Kanisa Katoliki limezongwa na kashfa mbalimbali pamoja na migawanyiko ya ndani.

Atatakiwa kusafisha ufisadi katika makao makuu ya kanisa yaani Vatican pamoja na kufufufua ukatoliki katika kipindi ambacho watu wanazidi kujitenga na dini.

Awali, migawanyiko na ugumu wa kumpata mtu mmoja mwenye sifa za kukabiliana na changamoto hizo kwa mujibu wa wachambuzi wengi, ulitabiriwa kuwa ungewafanya makardinali kuwa na mchakato mrefu wa kumpata papa kuliko ule wa 2005 ulioshuhudia chaguzi nne kumpata Papa Benedict XVI.

Awali, kundi la walinzi wa Kiswisi wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi ikiwamo kofia ngumu za rangi ya fedha waliandamana kuelekea katika Kanisa Kuu kwa maandalizi ya kutangazwa kwa Papa mpya huku bendi za jeshi zikiwaburudisha walioshuhudia.

No comments:

Post a Comment