Monday, July 8, 2013

USAFIRI DAR KITENDAWILI

DAR ES SALAAM, Abiria  waliokuwa wasafiri kwenda mikoani na nchi jirani, wamekwama katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo kutokana na uchache wa mabasi.

Mwananchi jana ilishuhudia mamia ya abiria wakisubiri mabasi yalikuwa njiani  kurejea Dar es Salaam ili na wao waweze kusafiri kwa mabasi hayo.

Katika kituo hicho ambacho kwa kawaida huwa na mabasi mengi, kwa siku ya jana muda wa saa nne hadi tano ni mabasi matatu tu ya Shabiby Line, Hood na Simba One ndio yalikuwa yakipakia abiria kuelekea Morogoro na Dodoma,huku kukiwa hakuna basi lolote la kuelekea mikoa ya Kaskazini.

Abiria hao wengi wakiwa ni wanafunzi walikuwa wakirejea shuleni kwa ajili ya muhula mpya wa masomo unaotarajiwa kuanza leo.

Wakizungumza na Mwananchi walisema wanadhani uhaba wa mabasi umetokana na uwapo wa wanafunzi wengi ambao wanarudi shule baada ya kumaliza likizo za katikati ya mwaka.

“Sisi tumekata tiketi tangu jana ya kwenda Dodoma, tunakwenda Msalato Sekondari,lakini leo tumefika hapa asubuhi na tulitakiwa kuondoka na basi la saa nne lakini mpaka saa tano hii tunaambiwa tusubiri basi liko njiani linakuja”walisema wanafunzi ambao hawakutaka kutaja majina.(MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment