Friday, July 12, 2013

CCM VS CHADEMA -VITA KALI.

 
DAR ES SALAAM,Siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuponda mpango wa Chadema kuanzisha kambi kwa ajili ya mafunzo ya ulinzi kuwalinda viongozi na wanachama wake,  chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeibuka na kusema kuwa kinaendelea na mpango huo na kambi hizo zitaanza rasmi wiki ijayo.
Kimesema hakitishwi na kauli ya Jeshi la Polisi kukionya juu ya  uanzishwaji wa mafunzo hayo,  kwamba jeshi hilo linatakiwa kuanza kukizuia Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kwanza, kwa maelezo kuwa chama hicho tawala pia kina kikundi cha ulinzi ‘Green Guards’ ambacho kinafanya mafunzo ya kijeshi, huku kikitumia silaha za moto.
“CCM ndiyo wataipeleka nchi hii pabaya, wanawafundisha vijana huku wakiwabebesha  bunduki, wanajenga taifa la aina  gani, bunduki ni silaha ya kivita sasa wanaandaa watu kupigana na nani” alisema Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira jana wakati akizungumza na wanahabari huku akionyesha picha za mafunzo ya CCM, zinazoonyesha vijana wakiwa wamebeba silaha (hata hivyo ni mbao zilizotengenezwa kwa mfano wa bunduki).
Wakati Chadema wakieleza hayo, CCM kimeshtushwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa nchi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Martin Shigela alisema ni vyema Chadema kikawaambia wananchi wawalinde, kuliko kuanzisha mafunzo huku akimtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa kulitizama kwa kina suala hilo.
Akifunga Kongamano  la Amani lililoandaliwa  na Kituo cha Demokrasia  Tanzania (TCD), Dar es Salaam Julai 10, mwaka huu, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa pia alikosoa kitendo cha Chadema kususia kongamano hilo alisema, “Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati hawapendi tuzungumze wanataka watu wauane, wapigane.”
Mbali na Rais Kikwete, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SSP Advera Senso juzi alikionya chama hicho kuhusu mpango huo akisema kuwa kitendo cha chama chochote cha siasa kikiwemo Chadema, kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume na sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli ya jana ya Chadema ni mwendelezo wa ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe Julai 9, mwaka huu, ambapo alisema  kimechukua hatua hiyo baada ya Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kushindwa kufanyia kazi malalamiko yao kuhusu mauaji, vitisho na matukio ya kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wao.
Katika ufafanuzi wake Kigaila alisema Chadema hakianzishi vikundi vya kijeshi, bali mafunzo ya  kuwafundisha walinzi wa chama hicho  ‘Red Brigade’, jinsi ya kujilinda.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki kwa raia yeyote kujilinda, Chadema ni taasisi ni haki yetu kuilinda taasisi yetu ndiyo maana tumesajili kikundi chetu cha ulinzi, sasa nani anatutisha, tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao katika mafunzo yao  wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yataanza rasmi wiki ijayo, huku akisita kutaja siku yatakayoanza, wala mikoa yatakayofanyika na kusisitiza kuwa hayo yatatangazwa wiki ijayo wakati vijana wakienda katika mafunzo.(MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment