Tuesday, April 9, 2013

BUNGE LA BAJETI KUANZA LEO.

 
DODOMA-TANZANIA, Mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti unaanza leo mjini Dodoma, huku kukiwa na mabadiliko kadhaa ya taratibu za uendeshaji wa Bunge.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Bunge (Habari), Deogratius Egidio ilieleza kuwa Bunge litaanza vikao vyake leo na kukamilika Juni 28, mwaka huu.
Kutokana na mabadiliko hayo, leo asubuhi Bunge litapokea Azimio la Marekebisho ya Kanuni za Bunge ambalo linatarajia kuwasilishwa na Naibu Spika, Job Ndugai.
Egidio alisema katika mkutano huo, mambo kadhaa yanaonekana kubadilishwa ikizingatiwa na utaratibu uliozoeleka tangu mwanzo wa kusoma kwanza Bajeti ya Serikali na baadaye kumalizia na bejti za wizara mbalimbali.
Aliyataja mabadiliko hayo kuwa ni utaratibu mzima jinsi ya uwasilishaji bajeti za wizara, kwa mwaka huu itaanza Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo itajadiliwa kwa siku tano. “Siku zote tumezoea kuona Bajeti ya Serikali ndiyo inayotangulia kuanza kuwasilisha bajeti yake, utaratibu huo umeonekana siyo mzuri kutokana na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG), hivyo tunaanza na wizara zingine ili fedha wawe mwisho,” alisema Egidio.
Hata hivyo, taarifa za zilizopatika kutoka ndani zinadai kanuni nyingi zinatarajia kubadilishwa na kwamba, iwapo zitapitishwa zitapunguza meno ya Bunge dhidi ya kusimamia Serikali.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kesho itakuwa siku maalumu kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwasilisha bajeti yake, ambayo itajumuisha wizara zote zilizo chini yake na inatarajia kujadiliwa kwa muda wa siku tano.
Mabadiliko mengine ni kuwasilishwa mezani kwa taarifa ya CAG kwa mwaka 2011/12 bila kujadiliwa na wabunge kama ilivyozoeleka.
Hata hivyo, Egidio hakueleza sababu za kutojadiliwa kwa ripoti hiyo, akisema hawezi kujua katika mikutano ya baadaye ya Bunge iwapo inaweza kupangiwa kujadiliwa. 

No comments:

Post a Comment