Saturday, April 13, 2013

YANGA NA OLJORO KIBARUANI LEO.

 
DAR ES SALAAM-TANZANIA,
VINARA wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam leo wanatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa kuwakabili maafande JKT Oljoro katika mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu.

Wakati Yanga wakikabiliana na JKT Oljoro, maafande wengine Tanzania Prisons watakuwa wakipigana kuepuka ukanda wa hatari kushuka daraja dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Yanga wenye pointi 49 watakuwa na kibarua kizito kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kuzidisha tofauti ya pointi na Azam FC wanaokamata nafasi ya pili kwa pointi 46, baada ya juzi kuishinda African Lyon kwa mabao 3-1.
Awali Yanga na JKT Oljoro zilikuwa ziumane juzi kabla ya mechi hiyo kuahirishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutoa nafasi kuoneshwa ‘live’ na kituo cha runinga cha Super Sport.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya alisema vijana wao wako fiti na waliokuwa nje kutokana na majeraha hali zao zimetengemaa.
Matuzya aliwataja wachezaji waliokuwa nje kwa majeraha kuwa ni Nizar Khalfan, Shadrack Nsajigwa, Juma Abdul, Omega Seme, Jerryson Tegete pamoja na Stephen Mwasyika ambao wameanza mazoezi na wenzao.

Ligi hiyo itaendelea kesho, ambako Azam FC watashuka dimbani kuikabili Simba ambayo tayari imepoteza mwelekeo kutetea taji lake kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment