Thursday, April 11, 2013
OFISI YA WAZIRI MKUU KUTUMIA TRILIONI 4.2.
DODOMA-TANZANIA,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameliomba Bunge kuidhinisha Sh4.2 trilioni ambazo ni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/14 kwa ajili ya ofisi yake pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Fedha hizo ni za matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo za ndani na nje. Pinda alitoa ombi hilo alipokuwa akiwasilisha bungeni mjini Dodoma jana mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2013/14.
Ameliomba Bunge liidhinishe Sh123.4 bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, Sh114.5 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh8.8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Aliziombea ofisi za wakuu wa mikoa Sh193.8 bilioni na kati ya fedha hizo, Sh143.7 bilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh50 bilioni za miradi ya maendeleo. “Halmashauri naziombea kiasi cha Sh3.6 trilioni na kati ya hizo, Sh2.9 trilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh640.5 bilioni ni za miradi ya maendeleo,” alisema Pinda.
Katika hotuba hiyo, Pinda aligusia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa daftari la wapigakura ambao unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu kwa awamu ya kwanza. “Uboreshaji huo utawezesha kuchapishwa kwa daftari la wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” alisema Pinda. Pia alizungumzia suala la nchi kutoka katika mfumo wa analojia kwenda dijitali na kupigilia msumari akieleza kuwa Serikali itaendelea na mabadiliko hayo kama ilivyo sasa kuliko kusubiri na kujikuta iko nyuma na nje ya mstari. “Natoa wito kwa Watanzania wote kuyaona mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya na kuyakubali kama hatua kubwa sana ya maendeleo ya teknolojia nchini,” alisema Pinda na kuongeza: “Katika mazingira ya sasa sisi kama taifa siyo vyema kubaki kama kisiwa wakati tumeunganishwa na mifumo ya teknolojia.” Pia alisema Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha halmashauri mpya 31 ili kuongeza huduma karibu na wananchi.(MWANANCHI)
Labels:
habari mpya,
tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment