Friday, August 24, 2012

MWAKYEMBE AMSIMAMISHA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA BANDARI

DAR-ES-SALAAM-TANZANIA,
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw.Ephraim Mgawe, Pamoja na wafanyakazi wengine wakiwemo wasaidizi wake wawili na meneja wa Bandari hiyo Bw.Cassian Ng'amilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe, pamoja na wizi wa vitu mbali mbali yakiwemomafuta na  makontena yanayosafirishwa kupitia bandari hiyo.

Akizungumza baada ya hatua hiyo waziri Mwakyembe amesema bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikikosa wateja ambao wameamua kusafirishia mizigo yao kupitia bandari za Msumbiji na Afrika Kusini kutokana na kukithiri kwa wizi katika bandari hiyo.Waziri huyo aliongeza kuwa serikali haiwezi kukaa na kukosa mapato kwa sababu ya wizi uliopita kiasi.

Waziri huyo pia ameunda kamati ya watu sita ingawa hakuwataja kwa majina ili kuchunguza wizi huo akiwapa maswali yenye hadidu za rejea zipatazo hamsini. Baada ya hatua hiyo Dk Mwakyembe amemteua Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi, Injinia Madeni Kipande kukaimu nafasi hiyo ya ukurugenzi wa bandari.Hatua hiyo imedaiwa kuchochewa na wizi wa makontena 40 ya vitenge yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi hivi karibuni.

Hiyo ni hatua nyingine kubwa kuchukuliwa na Waziri huyo ambaye Mwezi juni alimfukuza Kaimu mkurugenzi wa shirika la ndege la Tanzania(ATCL) Bw.Paul Chizi.

No comments:

Post a Comment