Saturday, February 8, 2014

Raia waanza kuhamishwa Syria.

homs_02492.jpg
Raia wakiwa wamebeba mizigo yao wanaondoka kwenye mji wa Homs.
Awamu ya kwanza ya raia wa Syria waliokuwa wamenasa kwenye maeneo yanayoshikiliwa na waasi mjini Homs imehamishwa huku serikali na waasi wakikubaliana kusitisha mapigano kwa muda kupisha huduma za kibinaadamu.
Televisheni ya taifa imeonesha picha za wafanyakazi wa Shirika la Hilali Nyekundu wakiwasaidia wazee waliodhoofu wakiwa wamefunikwa mablanketi ndani ya basi, huku mwanamke mmoja akiwa kwenye kiti cha maringi akisubiri zamu yake.

Televisheni ya serikali ilisema raia hao walikuwa wakitumika kama "ngao" na "makundi ya kigaidi" - jina linalotumiwa na serikali kuwaita waasi wanaopigania kuing'oa madarakani serikali ya Assad.
Wafanyakazi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa wakiwa na vizibao vya buluu ndio waliosimamia uhamishwaji wa raia hao na gari yenye alama ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa ilionekana kuegeshwa karibu na eneo hilo.
Serikali ilikubaliana na kile kilichoitwa "mapumziko ya kibinaadamu" na wanaharakati wa upinzani mjini Homs walisema waasi nao walikubali kusitisha mapigano kwa siku nne.
Jeshi lilianzisha mkururo wa mashambulizi kuyachukua tena maeneo ya Mji Mkongwe mwanzoni mwaka 2012, huku mabomu ya takribani kila siku yakiuwa maelfu ya watu.
Mji huo wa tatu kwa ukubwa nchini Syria na uliopewa jina la "makao makuu ya mapinduzi" na waasi, umekuwa kituo kikuu cha mapambano tangu mwanzoni mwa takribani ya miaka mitatu ya upinzani dhidi ya Rais Bashar al-Assad.
Vyombo vya habari vya serikali vimesema kufikia jioni ya Alhamisi (tarehe 7 Februari), mabasi yalikuwa yameondoka Homs na jumla ya raia 60, wengi wao wanawake, watoto na wazee.
Mwandishi wa shirika la habari la AFP alisema kiasi cha raia 12 walishuka kwenye basi la kwanza kutoka mji huo ulio kwenye mikono ya waasi na ambao umekuwa ukizingirwa na jeshi kwa zaidi ya siku 600.
Hali mbaya ya kibinaadamu
Gavana wa Homs, Talal Barazi, aliiambia AFP kuwa kiasi cha raia 200 walikuwa "tayari kuokolewa jana" (Ijumaa) kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa na Umoja wa Mataifa.
Kuhamishwa kwa watu hao ni sehemu ya makubaliano ya kushangaza kati ya pande hizo mbili yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa baada ya miezi kadhaa za mazungumzo.
Makubaliano hayo pia yanajumuisha kufikishwa kwa misaada wakati wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinaadamu.
Hata hivyo, Barazi alisema shehena ya kwanza ya chakula na madawa haitaweza kufikishwa kwa raia hadi Jumamosi (8 Februari).
Wanaharakati wamekuwa wakiripoti mara kwa mara juu ya upungufu mkubwa wa chakula ambapo kiasi cha watu 3,000 - wakiwemo wanawake, watoto na wazee 1,200 - walionasa huko, wanaishi kwa kula mazaituni na majani tu.
Mwanaharakati mmoja, Yazan, ameiambia AFP kupitia mtandao wa Intaneti kwamba wale wanaoondoka wana hisia mchanganyiko. "Kwa upande mmoja, wanafurahia kunusurika lakini pia wanahofia kitakachotokea baadaye, kwani wanaogopa kuwa watakamatwa na kuwekwa ndani na serikali."
Barazi alisema walioruhusiwa kuondoka ni watoto walio chini ya miaka 15, watu wazima wanaume walio na umri wa zaidi ya miaka 55 na wanawake, akiita operesheni hiyo iliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuwa na mafanikio.
"Kulikuwa na ugumu awali kwa raia kutoka kwenye maeneo yaliyoshikiliwa na waasi kwenye Mji Mkongwe, lakini alhamdulillah kwamba hatimaye waliweza kuondoka," alisema.
Chanzo, dw.de.com/swahili

No comments:

Post a Comment