Wednesday, February 12, 2014

WAKAZI 200 DAR WAITAKA TANESCO ISHUSHE BEI YA UMEME

tanesco31_e316c.jpg

UMOJA wa wakazi zaidi ya 200 wa Dar es Salaam wametoa siku kumi kwa Shirika la Umeme nchini(TANESCO), pamoja na vyombo vingine vya maamuzi, kubatilisha maamuzi yake juu ya bei mpya ya umeme na irejeshwe bei iliyokuwepo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenzake, Kiongozi wa Hoja hiyo, Sheikh Rashid Kayumbo alisema kuwa bei hiyo imekuwa ikiwaumiza watanzania wengi.
Alisema ongezeko la bei ya umeme limesababisha kupanda bei ya bidhaa mbalimbali nchini, hivyo kuchochea zaidi ukali na ugumu wa maisha.
"Tunawasihi watanzania wote wawe na subira na wawe na amani kabisa juu ya hoja hii, pia watuunge mkono kwa asilimia 100 kwa ujumla wao, juu ya pingamizi hili na wawe tayari kuelekezwa cha kufanya juu ya pingamizi letu," alisema.
Alisema baada ya siku kumi kumalizika, bila utekelezaji wowote kama walivyotaka, Februari 21 watafanya mkutano mkubwa wenye sura ya kitaifa, ukijumuisha viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na wabunge kupitisha azimio lao.
"Azimio letu litakuwa ni kususia umeme hadi itakaporejeshwa bei ya zamani, hii ni kuliko maandamano ya aina yoyote," alisema.
Alisema walifikiri kwamba kupandishwa kwa bei hiyo, huduma zitaboreshwa, lakini hadi sasa huduma za TANESCO ni za ubabaishaji na shirika hilo halina uhalali wa kupandisha bei ya umeme.
“Sisi wakazi wa jiji la Dar es Salaam wa wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni kwa niaba ya Watanzania wote nchi nzima, tunatoa siku kumi kwa Tanesco pamoja na vyombo vingine vya maamuzi katika suala hili kubatilisha maamuzi yake juu ya bei mpya ya umeme, na irejeshwe bei yetu iliyokuwepo kabla ya sasa”, alisema.
CHANZO:MJENGWA BLOG.

No comments:

Post a Comment