Wednesday, February 12, 2014

Sheria ya ndoa sasa kupigiwa kura ya maoni

Bagamoyo. Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki amesema kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 iko kwenye mchakato wa kurekebishwa kutokana na utata unaokinzana na sheria nyingine za masuala ya kijinsia.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa warsha ya siku moja ya waandishi wa habari na sheria na sera zinazohusu ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na Taasisi ya Champion na Engender Health wilayani Bagamoyo juzi, Kairuki alikiri kuwepo kwa utata wa sheria hiyo jambo linaloendelea ukatili hasa kwa wanawake.
“Utata wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ulijadiliwa katika Baraza la Mawaziri na walishafika mbali. Lakini ilionekana kwa kuwa masuala ya ndoa na mirathi yanagusa mila, desturi, dini na tamaduni za watu, ilionekana siyo rahisi kutunga sheria haraka,” alisema Kairuki na kuongeza:
“Wapo wanaosema mtoto hawezi kuolewa akiwa na miaka 14 na wapo wanaosema anaweza. Baraza la Mawaziri liliamua kuwa kuwe na kura ya maoni (white paper).”
Hata hivyo alisema kuwa wakati mchakato huo ukikaribia kuanza uliingiliana na mabadiliko ya Katiba. Hivyo alisema kura hiyo ya maoni itafanyika baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya.
Awali akifungua warsha hiyo, Kairuki alisema kuwa Serikali imechukua hatua za kukabiliana na ukatili wa kijinsia ikiwa pamoja na kuanzisha dawati la jinsia na watoto kupitia Jeshi la Polisi na timu za ulinzi na usalama wa watoto kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii.
Akitoa mada katika warsha hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya Engender Health, Dk Monica Mhoja alisema Serikali ya Tanzania inasifika kwa kuridhia sheria na mikataba ya kimataifa kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini hazitekelezwi ipasavyo.
“Tunapokuwa kwenye majukwaa ya kimataifa, Tanzania tunasifika kwa kuridhia sheria na sera nyingi, wanapotuhoji kuhusu utekelezaji inakuwa shida,” alisema Dk Mhoja.
Chanzo:Mwananchi.

No comments:

Post a Comment