Rais Barack Obama akizungumzia kuhusu hali nchini Ukraine. |
Marekani imeonya kuwa rais Barack Obama pamoja na viongozi wengine wa Ulaya wataususia mkutano wa kundi la mataifa ya G8 mjini Sochi iwapo wataona kuwa Urusi inaingilia uhuru wa Ukraine.
Obama ameeleza wasi wasi wake mkubwa kuhusiana na ripoti kuwa majeshi ya Urusi yameingia mjini Crimea, kufuatia madai yaliyotolewa na afisa wa serikali mjini Kiev kuwa uvamizi umeanza.
Maafisa waandamizi wamesema rais ameamua kujitokeza katika ikulu ya Marekani ya White Housena kutoa maelezo baada ya nchi hiyo kuamua kuwa kulikuwa na ushahidi kwamba majeshi ya Urusi ni kweli yako ndani ya Ukraine.
Vikosi vyenye silaha nzito na katika sare ambazo hazina nembo ya taifa vimeonekana kuzunguka majengo ya serikali na katika uwanja wa ndege katika mji wa Crimea wa Simferopol , wakati maafisa wa Ukraine wakiishutumu Urusi kwa kile walichokiita uvamizi wa wazi.
Majeshi ya Urusi
Mzozo huo ulianzia katika mzozo wa kisiasa na kiuchumi kufuatia kuondolewa kwa serikali inayoelemea upande wa Urusi mjini Kiev na kuingia katika mpambano wa kieneo baada ya madai ya maafisa wa Ukraine kuwa kiasi ya wanajeshi 2,000 wa Urusi wamewasili mjini Crimea.
"Tuna wasi wasi mkubwa sasa kuhusiana na ripoti za harakati za kijeshi zinazochukuliwa na shirikisho la Urusi ndani ya Ukraine," Obama amesema.
Afisa wa jeshi ameliambia shirika la habari la AFP baada ya taarifa ya rais kwamba " inaonekana kama wameingiza wanajeshi kadha nchini humo.
Afisa huyo amesema kuwa Urusi haijatoa tahadhari yoyote kabla kuhusu harakati hizo. Obama anatambua kuwa Urusi imekuwa na maslahi yake pamoja na uhusiano wa kiutamjaduni na kiuchumi na Ukraine, na imekuwa na maeneo ya kijeshi katika eneo la Crimea, eneo ambalo liliunganishwa na jamhuri ya zamani ya Kisoviet ya Ukraine katika umoja wa Kisoviet mwaka 1954.
Obama aonya
Lakini amesema ukiukaji wowote wa uhuru wa Ukraine pamoja na ardhi ya nchi hiyo utaiyumbisha kwa kiasi kikubwa Ukraine. "Marekani itasimama pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kusisitiza kuwa kutakuwa na gharama katika uvamizi wowote wa kijeshi nchini Ukraine," alisema rais Obama.
Afisa mwingine mwandamizi baadaye amedokeza kuwa gharama hizo zinaweza kujumuisha uamuzi wa Obama na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa Ulaya kususia mkutano wa nchi zenye utajiri mkubwa wa viwanda za G8 mkutano utakaofanyika katika mji wa kitalii uliofanyika michezo ya Olimpiki wa Sochi mwezi Juni.
Uwezekano mwingine wa kibiashara na kiuchumi ambao Urusi ilikuwa inataka hadi wiki hii huenda ukaingia katika hali shaka , afisa huyo amesema.
Urusi pia itavuruga nafasi yake ya kuonekana kuwa na mvuto duniani baada ya michezo ya majira ya baridi, ambayo ilimalizika mwishoni mwa juma lililopita, ameeleza afisa wa Marekani.
Chanzo, dw.de/swahili (R.M)
No comments:
Post a Comment