Monday, March 3, 2014

Mwelekeo mpya bungeni, Pinda atoa hoja .

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba.
Katika mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema: “Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano) tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu kuyatazama. “Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika misimamo inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema: “Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe.”
Katika ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na “kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri.” Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha mahakamani.

Chanzo: Mwananchi.

MAN CITY YAITWANGA SUNDERLAND NA KUCHUKUA CAPITAL ONE




‘Pandu Kificho ametusaliti’

Zanzibar. Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho amekiri kuwasilisha waraka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa na mamlaka huru, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa makada wa chama hicho ambao wamesema huo ni usaliti.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma, Kificho ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alisema kimsingi waraka huo ulilenga kuipa nguvu Zanzibar kushughulikia mambo yasiyo ya Muungano ili kujiimarisha kiuchumi.
Kauli ya Kificho inakuja wakati baadhi ya wajumbe wa CCM kutoka Zanzibar wakiitisha mkutano na kutoa tamko la kumshutumu kwa kutoa mapendekezo hayo, wakisema ni kinyume na msimamo wa chama hicho.
Kificho alionyesha kushangazwa na madai kuwa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na watu wanne ambayo ameyasaini si msimamo wa BLW.
“Tatizo lililopo ni tafsiri ya kila mmoja anapousoma waraka huo, hakuna sehemu tuliyoandika tunataka Serikali tatu, mamlaka huru maana yake kila upande uwe na uwezo wa kushughulikia mambo yake yasiyo ya Muungano na kujijenga kiuchumi, ikiwa ni pamoja Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya Kimataifa (OIC) na siyo kuunda dola,” alifafanua Spika Kificho.
Alisisitiza kuwa angependa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano yaendeshwe na Zanzibar bila ya kuwekewa vikwazo mahali popote.
Madai hayo ni dalili za wazi za mgawanyiko baina ya wajumbe wa CCM ambao wameanza kuonyesha makundi mawili yenye misimamo tofauti.
Kundi linalomshutumu Kificho, linawajumuisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Juma Ali Shamhuna, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Spika wa BWZ, Ali Abdallah Ali.
Jana, kundi hilo lilimtuhumu Kificho kuwa hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo Serikali tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema  Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Hata hivyo, mtazamo huo wa BLW unatofautiana na ule wa Kificho uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, ukipendekeza Serikali tatu.
“Kwa vile mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa hauwezi kujenga Muungano utakaohimili mabadiliko ya kisiasa na kwa vile umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa umeshindwa kujenga Muungano imara, uachwe katika kuendesha Muungano wa Tanzania,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Othman.
Jana asubuhi, zaidi ya wajumbe 10 wa Baraza la Wawakilishi akiwamo Shamhuna, Nahodha na Ali waliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtupia lawama Kificho wakisema; “Amewasaliti katika mchakato huo wa Katiba.”

Sunday, March 2, 2014

Wanamgambo wa Nigeria wauwa watu 33

NIGERIA_5e951.jpg
Mabaki ya chuo cha serikali ambapo wanafunzi 60 walichomwa moto hadi kufa Februari 25, 2014
Shambulizi hilo la Alhamis karibu na mpaka wa Cameroon lilifanyika siku moja baada ya mashahidi kuripoti kuwa takribanu wanafunzi 60 waliuwawa katika chuo cha serikali.
Mashahidi na maafisa wa ndani kaskazini mashariki mwa Nigeria wanasema kundi linalotuhumiwa la wanamgambo wa Boko Haram limeuwa watu 33 na kushambulia kwa bomu chuo cha kidini katika jimbo la Adamawa.
Jeshi ambalo mara nyingi haliamini taarifa za idadi ya vifo kutoka kwa mashahidi limesema washambuliaji sita waliuwawa katika tukio hilo pamoja na mwanajeshi mmoja na raia watatu .
Shambulizi hilo la Alhamis karibu na mpaka wa Cameroon lilifanyika siku moja baada ya mashahidi kuripoti kuwa karibu wanafunzi 60 waliuwawa katika chuo cha serikali karibu na jimbo hilo la Adamawa.
Chanzo, voaswahili. (R.M)

Chelsea yajiimarisha kileleni ligi kuu

CFC_910be.jpgTimu ya Chelsea imezidi kujiimarisha kileleni mwa ligi kuu ya England baada ya kuicharaza Fulham magoli 3-1 na kujikusanyia pointi 63.
Mabao yote matatu ya Chelsea katika mchezo huo yalifungwa na mshambuliaji wake Andre Schurrle akiyafunga katika dakika ya 52, 65 na 68, huku bao la kufutia machozi la Fulhamlikifungwa na Heitinga katika dakika ya 74.

Arsenal iliyokuwa ikifukuzana na Chelsea kwa tofauti ya pointi moja imejikuta ikiachwa pointi nne zaidi baada ya kucharazwa na Stoke goli 1-0. Arsenal imebaki na pointi 59 na kuporomoka hadi nafasi ya tatu, huku Liverpool ikipanda, nayo ikiwa na pointi 59 zikitofautiana kwa mabao ya kufunga.
Wakati Newcastle ikiididimiza Hull kwa mabao 4-1, nayo Everton iliibanjuaWest Ham bao1-0.
Msimamo wa ligi kuu ya England baada ya michezo hiyo ya Jumamosi, Chelsea inaongoza kwa pointi 63 baada ya kucheza michezo 28 ikifuatiwa na Liverpool yenye pointi 59 na Arsenal ni ya tatu ikiwa pia na pointi 59.
Mancity ni ya nne ikiwa na pointi 57 lakini ikiwa imecheza michezo 26 tu, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kwenda kileleni iwapo itashinda mechi zake mbili.
Manchester United mabingwa watetezi, iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 45 lakini imecheza michezo 27.
Mkiani kabisa ni Fulham yenye pointi 21 na mbele yake ni Cardiff yenye pointi 22.
Chanzo, bbcswahili (R.M)

Obama aeleza wasi wasi wake kuhusu Ukraine







obama_edc89.jpg
Rais Barack Obama akizungumzia kuhusu hali nchini Ukraine.


Marekani imeonya kuwa rais Barack Obama pamoja na viongozi wengine wa Ulaya wataususia mkutano wa kundi la mataifa ya G8 mjini Sochi iwapo wataona kuwa Urusi inaingilia uhuru wa Ukraine.
Obama ameeleza wasi wasi wake mkubwa kuhusiana na ripoti kuwa majeshi ya Urusi yameingia mjini Crimea, kufuatia madai yaliyotolewa na afisa wa serikali mjini Kiev kuwa uvamizi umeanza.
Maafisa waandamizi wamesema rais ameamua kujitokeza katika ikulu ya Marekani ya White Housena kutoa maelezo baada ya nchi hiyo kuamua kuwa kulikuwa na ushahidi kwamba majeshi ya Urusi ni kweli yako ndani ya Ukraine.
Vikosi vyenye silaha nzito na katika sare ambazo hazina nembo ya taifa vimeonekana kuzunguka majengo ya serikali na katika uwanja wa ndege katika mji wa Crimea wa Simferopol , wakati maafisa wa Ukraine wakiishutumu Urusi kwa kile walichokiita uvamizi wa wazi.
Majeshi ya Urusi
Mzozo huo ulianzia katika mzozo wa kisiasa na kiuchumi kufuatia kuondolewa kwa serikali inayoelemea upande wa Urusi mjini Kiev na kuingia katika mpambano wa kieneo baada ya madai ya maafisa wa Ukraine kuwa kiasi ya wanajeshi 2,000 wa Urusi wamewasili mjini Crimea.
"Tuna wasi wasi mkubwa sasa kuhusiana na ripoti za harakati za kijeshi zinazochukuliwa na shirikisho la Urusi ndani ya Ukraine," Obama amesema.
Afisa wa jeshi ameliambia shirika la habari la AFP baada ya taarifa ya rais kwamba " inaonekana kama wameingiza wanajeshi kadha nchini humo.
Afisa huyo amesema kuwa Urusi haijatoa tahadhari yoyote kabla kuhusu harakati hizo. Obama anatambua kuwa Urusi imekuwa na maslahi yake pamoja na uhusiano wa kiutamjaduni na kiuchumi na Ukraine, na imekuwa na maeneo ya kijeshi katika eneo la Crimea, eneo ambalo liliunganishwa na jamhuri ya zamani ya Kisoviet ya Ukraine katika umoja wa Kisoviet mwaka 1954.
Obama aonya
Lakini amesema ukiukaji wowote wa uhuru wa Ukraine pamoja na ardhi ya nchi hiyo utaiyumbisha kwa kiasi kikubwa Ukraine. "Marekani itasimama pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kusisitiza kuwa kutakuwa na gharama katika uvamizi wowote wa kijeshi nchini Ukraine," alisema rais Obama.
Afisa mwingine mwandamizi baadaye amedokeza kuwa gharama hizo zinaweza kujumuisha uamuzi wa Obama na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa Ulaya kususia mkutano wa nchi zenye utajiri mkubwa wa viwanda za G8 mkutano utakaofanyika katika mji wa kitalii uliofanyika michezo ya Olimpiki wa Sochi mwezi Juni.
Uwezekano mwingine wa kibiashara na kiuchumi ambao Urusi ilikuwa inataka hadi wiki hii huenda ukaingia katika hali shaka , afisa huyo amesema.
Urusi pia itavuruga nafasi yake ya kuonekana kuwa na mvuto duniani baada ya michezo ya majira ya baridi, ambayo ilimalizika mwishoni mwa juma lililopita, ameeleza afisa wa Marekani.
Chanzo, dw.de/swahili (R.M)

JK: HARAKISHENI SHERIA USALAMA MITANDAONI

 

Rais Jakaya Kikwete, akibofya kitufe kuzindua mtambo wa kuhakiki takwimu za mawasiliano kwenye Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha mchakato wa Sheria ya Usalama kwenye mitandao unakamilika na kuanza kutumika, ili kudhibiti wanaotoa siri za nchi kwa kisingizio cha uhuru wa habari.
Hayo aliyasema jana kwenye hafla ya uzinduzi wa mtambo maalumu wa usimamizi na uhakiki wa Mawasiliano ya Simu, (TTMS), iliyofanyika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Dar es Salaam.

Rais Kikwete alisema hakuna nchi yoyote duniani ambayo haitunzi siri zake, kwa kuwa jambo hilo ni muhimu kiusalama, hata kwa mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutetea uhuru wa vyombo vya habari.
Alisisitiza kwa kumtolea mfano aliyekuwa Jasusi wa Marekani, Edward Snowden, anatuhumiwa kuvujisha siri za nchi hiyo kwenye mtandao, ambaye sasa amekimbilia mafichoni Urusi. Aliwapongeza TCRA kwa hatua hiyo, akieleza kuwa inawezesha uchumi wa nchi kupata kichocheo cha kukua kwa kuwa sasa kutakuwa na udhibiti wa mawasiliano hasa ya simu za nje ya nchi na kuongeza kipato kwa taifa.
Awali Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema kufungwa kwa mitambo hiyo, kunakwenda pamoja na kuwapo kwa kanuni mpya za mawasiliano ya usimamizi na uhakiki wa mawasiliano ya simu (TTMS, Regulation 2013), ambapo imewezesha Serikali kupata senti 7 kati ya 25 zinazotozwa kwa kila dakika na nyingine zinagawanywa kwa kampuni husika.
"TCRA imefanikiwa kuilipa Hazina mgawo wa mwezi Oktoba, kwa mujibu wa Sheria ya TMMS Sh1.6 bilioni, leo tutakabidhi malipo ya Sh1.6 bilioni malipo ya Novemba hatimaye mwezi Machi tutalipa ya Desemba," alisema Nkoma.
Chanzo, mwananchi (R.M)