Polisi wanamshikilia mganga wa jadi kutoka Kijiji cha Matera,
Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza kwa tuhuma za kumnyonga
mwanafunzi wa darasa la kwanza, Fausta Geofrey (8) na kukata viungo
vyake na kuvibanika ili kupata dawa ya uganga.
Anadaiwa kufanya mauaji hayo Mei 21 katika Kijiji cha Bisole, Kata ya Muhutwe, wilayani Muleba.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumkata mikono yote, masikio, ngozi ya mgongoni na sehemu za siri na kuvibanika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga
alisema mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wawili saa 1:30 asubuhi alipita
karibu na nyumba ya mganga wakielekea shuleni. Mayunga alisema mganga
huyo alimwita na kumkaba shingo na mdomo ili asipige kelele kabla ya
kumpeleka ndani ya nyumba alikomnyonga.
Baada ya kukata viungo vyake, mtuhumiwa anadaiwa kuchimba shimo chini ya kitanda chake na kuuzika mwili.
“Baada ya kumnyonga alikata mikono yote, masikio,
sehemu za siri na sehemu nyingine kwenye mwili na kuanza kuvibanika ili
vikauke aweze kutengeneza dawa ya uganga kwa wateja wake,” alisema
Mayunga.
Aidha, Mayunga alisema kuwa mganga huyo amekuwapo kijijini hapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Alisema wazazi wa mwanafunzi huyo waliingiwa na hofu baada ya kufika saa 10:00 jioni bila kurejea nyumbani.
“Baada ya kumsaka bila mafanikio, waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi ili kuomba msaada zaidi,” alisema Kamanda Mayunga.
Katika msako uliofanyika Jumapili Mei 22, polisi
na wananchi walimtilia shaka mganga huyo baada ya kumhoji alikiri
kufahamu alipo mtoto huyo na kuwaeleza kuwa alikuwa tayari amekufa.
Kamanda Mayunga alisema mganga huyo aliwapeleka hadi nyumbani na kuwaonyesha vifaa alivyotumia kwenye mauaji.
“Alituonyesha vifaa na alipomfukia mtoto huyo pamoja na viungo vilivyokuwa katika hatua ya ukaushwaji.”