Friday, August 31, 2012

WALIMU WAISHUKIA SERIKALI TENA

DAR ES SALAAM-TANZANIA,
http://in2eastafrica.net/wp-content/uploads/2012/07/Gratian-Mukoba.jpgSerikali imedaiwa kupuuza amri ya  Mahakama iliyotakakuktana na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ili kujadili maslahi ya walimu chini ya mshauri ambaye ni mtaalamu wa sheria za kazi.
Akiongea na waandishi wa habari hapo jana Rais wa chama cha walimu (CWT) Bw.Gratian Mkoba amesema licha ya agizo hilo la mahakama serikali haijawa tayari kukutana na walimu kusikiliza madai yao.

Mukoba kwa niaba ya CWT ameitaka serikali kukutana na walimu kabla ya Septemba 10, siku ambayo shule zinafunguliwa vinginievyo chama chake kitachukua hatua kitakazoona zinafaa.



Mukoba alisema Agosti 2, mwaka huu chama chake kilimwandikia Katibu Mkuu  Kiongozi barua yenye kumbu namba CWT/004/IKULU/VOL.1/48  nia yao ya kukutana naye kujadili madai hayo
ambapo aliwajibu atajadiliana na wenzake kuhusu suala hilo.
ukoba aliongeza kuwa agosti 6 waliandika tena barua ingawa haijapewa majibu mpaka sasa.

“Kitendo cha serikali kukaa kimya kwa muda wa siku 27 bila ya kuonesha kujali kutekeleza kwa amri ya mahakama kunatafsiriwa na CWT kama ni kukosekana kwa nia njema ya serikali kusikiliza madai ya walimu tofauti na propaganda zilizoendelezwa wakati wa mgomo juu ya utayari wao wa kujadiliana na walimu,” alinukuliwa Mukoba.

Mukoba aliitaka pia serikali kuwarudishia madaraka walimu iliowavua madaraka na kufuta mashitaka yote dhidi ya walimu inayodai walishiriki katika mgomo.Pia rais huyo ameitaka serikali kumaliza tatizo hilo mapema ili kuwapa matuamaini walimu kala ya shule kufunguliwa.

SHAMBULIO LA RISASI LAUA WATATU MAREKANI




NEW YORK-MAREKANI 
Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Terence Tyler, (23) amewapiga na kuwaua wafanyakazi wanzake kwa risasi na kujiua mwenyewe katika duka la New Jersey wanapofanya kazi leo hii mjini nje kidogo ya Jiji la New York huko Marekani.Waliouawa wametambuliwa kuwa ni binti wa miaka 18, Cristina LoBrutto na kijana Bryan Breen mwenye umri wa miaka 24.

Terence ambaye aliwahi pia kuwa mwanajeshi wa jeshi la maji la Marekani alikuwa akifanya kazi katika duka hilo kwa muda unaokadiriwa kuwa wiki 2, na imedaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kukosana na mmoja wa wafanyakazi wenzake.Polisi wamesema Terence alikwaruzana na mfanyakazi mwenzake leo asubuhi na akatoka na baadaye kurudi na bunduki pamoja na bastola ambapo aliwapiga risasi wafanyakazi wenzake wawili kabla ya kujipiga mwenyewe.

Wafanyakazi wenzake walifunga milango wakati akirudi ingawa alifanikiwa kuwapiga risasi kupitia dirishani.

Tukio hilo ambalo limetokea kabla ya kufunguliwa duka hilo, limekuwa ni mwendelezo wa matukio ya upiganaji risasi nchini humo baada ya lile lililotokea katika jumba la makumbusho la Sikh temple ambapo watu 6 waliuawa pamoja na lile lililotokea katika filamu ya Batman ambapo watu 12 waliuawa hali inayoongeza shinikizo juu ya sheria za uuzaji wa silaha nchini Marekani.





Saturday, August 25, 2012

MLIPUKO WA KIWANDA WAUA 24 VENEZUELA.

Mlipuko katika kiwanda cha mafuta venezuela (Picha na Reuters)

FALCON-VENEZUELA
Watu wapatao 24 wamefariki akiwamo mtoto mdogo wa miaka 10 na wengine zaidi ya 54 kujeruhiwa baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Amuay kulipuka nchini Venezuela.Chanzo cha moto huo kimeripotiwa kuwa ni kuvuja kwa gesi ambayo baadae iliwaka na kulipua matangi mawili ya kuhifadhia mafuta katika kiwanda hicho.
Taarifa zinasema mlipuko ulifuatiwa na motomkubwa ambavyo kwa pamoja viliharibu vibaya nyumba zilizokuwa jirani na eneo hilo.

Kiwanda hicho ni moja ya viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta duniani ambapo kinatoa hadi mapipa 645,000 kwa siku. Moto katika eneo hilo umedhibitiwa ingawa shughuli zote za uzalishaji zimesimama huku askari wakilinda eneo hilo.


Friday, August 24, 2012

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA NORWAY AFUNGWA MIAKA 21.


http://s1.reutersmedia.net/resources/r/?m=02&d=20120824&t=2&i=645573356&w=460&fh=&fw=&ll=&pl=&r=CBRE87N0N8A00

OSLO-NORWAY,
 Mahakama nchini Norway imemkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 21 jela, mtuhumiwa wa mauaji ya watu 77 nchini Norway Bw.Anders Behring Breivik. Matuhumiwa huyo alidaiwa kuhusika na mauaji ya watu 77 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 240 wakati alipotega bomu katikati ya mji wa Oslo na baadae kuwapiga kwa risasi vijana waliokuwa katika kambi moja huko Camp Island.

Mtuhumiwa huyo alikiri kufanya makosa hayo na kukataa kuitwa mkosaji akitetea uamuzi wake kuwa ni sahihi kwa kuwa alikuwa akizuia kuenea Uislam Norway.Kesi hiyo ambayo imedumu kwa miezi kadhaa ilikuwa na mvutano ambapo licha ya kuonekana na hatia mawakili na serikali walikuwa na mvutano ikiwa mtuhumiwa huyo yupo timamu au ana matatizo ya akili hali iliyokuwa ikileta utata juu ya hukumu anayostahili, ingawa hatimaye serikali imajiridhisha kuwa mtuhumiwa huyo anastahili hukumu.

Hukumu hiyo imewekwa wazi ambapo itaweza kuongezwa kwa miaka zaidi ya 21 ikiwa mtuhumiwa huyo ataonekana bado ni hatari kwa jamii yake hata baada ya kumaliza kifungo chake.

Familia na ndugu wa Marehemu na waathirika wa tukio hilo wameridhishwa na hukumu hiyo,"Amepata anachostahili," alisema Alexandra Peltre, 18,ambaye alipigwa risasi na kujeruhiwa na mtuhumiwa huyo.Bi. Per Balch Soerensen,  ambaye binti yake aliuawa katika shambulio hilo alisema anashukuru hukumu hiyo imefika mwisho kwa sababu watakuwa na amani na utulivu tena.

Mtuhumiwa huyo akivalia sare kama za polisi alilipua bomu pamoja na kuwapiga risasi vijana waliokuwa katika kambi huko Norway, na kusababisha vifao vya watu 77 hapo mwezi Julai Mwaka jana.

MWAKYEMBE AMSIMAMISHA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA BANDARI

DAR-ES-SALAAM-TANZANIA,
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw.Ephraim Mgawe, Pamoja na wafanyakazi wengine wakiwemo wasaidizi wake wawili na meneja wa Bandari hiyo Bw.Cassian Ng'amilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe, pamoja na wizi wa vitu mbali mbali yakiwemomafuta na  makontena yanayosafirishwa kupitia bandari hiyo.

Akizungumza baada ya hatua hiyo waziri Mwakyembe amesema bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikikosa wateja ambao wameamua kusafirishia mizigo yao kupitia bandari za Msumbiji na Afrika Kusini kutokana na kukithiri kwa wizi katika bandari hiyo.Waziri huyo aliongeza kuwa serikali haiwezi kukaa na kukosa mapato kwa sababu ya wizi uliopita kiasi.

Waziri huyo pia ameunda kamati ya watu sita ingawa hakuwataja kwa majina ili kuchunguza wizi huo akiwapa maswali yenye hadidu za rejea zipatazo hamsini. Baada ya hatua hiyo Dk Mwakyembe amemteua Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi, Injinia Madeni Kipande kukaimu nafasi hiyo ya ukurugenzi wa bandari.Hatua hiyo imedaiwa kuchochewa na wizi wa makontena 40 ya vitenge yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi hivi karibuni.

Hiyo ni hatua nyingine kubwa kuchukuliwa na Waziri huyo ambaye Mwezi juni alimfukuza Kaimu mkurugenzi wa shirika la ndege la Tanzania(ATCL) Bw.Paul Chizi.

WANAMGODI WALIOUAWA AFRIKA KUSINI WAOMBEWA.

http://gdb.voanews.eu/D6665CE2-085E-4BB6-B650-D6E5CE826744_mw800_s.jpgJOHANNESBURG- AFRIKA KUSINI
  Maelfu ya ndugu,jamaa na marafiki wa marehemu waliofariki wiki iliyopita katika mapambano kati ya wachimba mgodi wa Marikana na polisi walikusanyika hapo jana katika ibada ya pamoja kuwaombea marehemu hao. Ibada hiyo imefanyika katika eneo yalipotokea mauaji hayo huko Marikana ambalo limepewa jina la "Uwanja wa mauaji wa Afrika Kusini" na wanamgodi hao.

Viongozi wa kidini na kijadi ndiyo walioongoza ibada hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali na vyama vya wafanyakazi.Moja wa viongozi wa kidini alikuwa ni Daniel Modisenyane  aliwaambia waliohudhuria kuwa jamii itajitahidi kupambana na hasara hiyo.
" Siyo rahisi kwa wafiwa kusahau kwa kuwa limekuwa tukio la kuumiza na hatujui hata tutawatuliza vipi" Alisema Modisenyane.

Viongozi wengine waliilaumus serikali kwa kuhusika na mauaji hayo na kuitaka kuchukua hatua kali kwa waliohusika.
Misa hizo zilifanyika pia katika sehemu mbalimbali nchi nzima.

Tuesday, August 21, 2012

MAHAKAMA KUU TABORA YATENGUA USHINDI WA DK.KAFUMU.

http://t3.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcQWhv8Qn16oTZNOCpQyMoURwHU0PzoCSKDF4AhDMk-ahQApWNq1aw&t=1TABORA-TANZANIA,
Mahakama kuu Kanda ya Tabora imetengua rasmi matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa kiti cha ubunge mgombea na aliyekuwa Mbunge wa Igunga kupitia chama cha Mapinduzi(CCM) Dk Peter Kafumu, katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana. 

Hukumu hiyo imefuatia kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea katika uchaguzi huo kupitia tiketi ya chama cha demokrasia na Maendeleo Profesa Abdalla Safari  aliyemshitaki mgombea, huyo, mwanasheria mkuu wa Serukali, na msimaizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Katika kesi hiyo hoja mbalimbali zilitolewa kupinga matokeo hayo ikiwemo ya  matumizi mabaya ya madaraka kwa Waziri wa Ujenzi John Magufuli kufanya mkutano wa kampeni Kata ya Igulubi wilayani Igunga na kuahidi ujenzi wa Daraja la Mbutu kama wananchi hao watampigia kura mgombea wa chama mapinduzi na kuwatisha wananchi kuwa wasipoichagua CCM watashughulikiwa.

Katika hoja nyingine mgombea huyo kupitia tiketi ya  CHADEMA akiwakilishwa na wakili wake walimshitaki Rais mstaafu Benjamini Mkapa aliyetoa ahadi kwa wananchi wa Igunga siku moja kabla ya Uchaguzi, pamoja na ile ya baraza la Waislamu (Bakwata) wilaya ya Igunga kuwakataza waumini wake wasikipigie kura chama cha CHADEMA.
 

WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA AFARIKI DUNIA

 



ADDIS ABABA-ETHIOPIA
 Waziri mkuu wa Ethiopia Bw.Meles Zenawi, 57 amefariki dunia huku Brussels Ubelgiji usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taarifa za kifo cha waziri mkuu huyo zimetangazwa na msemaji wake Bw.
 Bereket Simon amesema waziri huyo alifariki katikati ya usiku baada ya kukimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi.Kifo cha waziri mkuu huyo kilizushwa kwa muda mrefu na hali ikawa ya wasiwasi zaidi baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Africa mwezi uliopita.

Makamu waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Hailemariam Desalegn ataapishwa punde kushika wadhifa huo mpaka chama tawala kitakapomchagua mrithi wa Bw,Zenawi kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

 Umoja wa Afrika umetuma salamu zake za rambi rambi kwa Ethiopia na kuelezea kifo hicho kama pigo kubwa kwa Afrika iliyompoteza mtoto Mahiri na hodari.

Uingereza pia kupitia kwa waziri Mkuu Bw.David Cameron imeelezwa kuguswa na msiba huo ikimtaja Waziri huyo kama mmoja ya Wazungumzaji wenye ushawishi barani Afrika.
Meles aliingia madarakani mwaka 1991 akimbadili Haile Mariam aliyekuwa kiongozi wa kijeshi na alisifiwa na wengi kwa juhudi zake zilizosaidia kukua haraka kwa uchumi wa nchi hiyo masikini.

Licha ya kulaumiwa na makundi ya haki za binadamu nchini humo kwa wakati fulani, waziri huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa jirani zake Somalia hasa katika mapambano dhidi ya
waasi pamoja na makundi yanayoshirikiana na Al Qaeda hali iliyomfanya rafiki mkubwa pia wa nchi za Magharibi. 
Hata hivyo haijawekwa wazi wapi na siku gani waziri huyo atazikwa.

MGODI ULIOUA AFRIKA KUSINI WAHAIRISHA TISHIO LA KUWAFUKUZA KAZI WAFANYAKAZI WALIOGOMA.

 http://www.globalpost.com/sites/default/files/imagecache/gp3_slideshow_large/south_africa_lonmin_marikana_miners_fired_20120820.jpg
 MARIKANA-AFRIKA KUSINI,
Uamuzi wa kuwafukuza wafanyakazi waliogoma  kushinikiza kuongezwa kwa mishahara na kupinga mauaji ya wenzao katika mgodi wa Marikana nchini Afrika kusini umegonga mwamba baada ya kampuni ya Lonmin inayomiliki mgodi  kuondoa tishio hilo.Akitangaza uamuzi huo makamu rais wa kampuni hiyo Bw.Mark Munroe amesema kuwafukuza maelfu ya wafanyakazi hakutasaidia kitu na hivyo kampuni yao imeamua kuondoa tishio hilo.

Ni asilimia 33 tu ya wafanyakazi 28,000 waliokuwa wameripoti kazini mpaka leo Jumanne ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho waliopewa na mgodi huo kurudi kazini, huku asilimia 67 ya wafanyakazi wakiwa bado wamegoma hali iliyoulazimu mgodi huo kusalimu amri.
Wafanyakazi hao wapo katika mgomo kushinikiza kuongezwa kwa mishahara yao na pia wakiwa katika maombolezo ya vifo vya wenzao 34 waliopigwa risasi katika mapambano na polisi wiki iliyopita.

Serikali ya Afrika kusini imeutaka mgodi huo kuachana na uamuzi huo na kusubiri kutafutwa kwa suluhu nyingine ambayo itakuwa na msaada kwa tatizo hilo.
  Wakati huo huo Bunge la Afrika kusini ambalo litakaa siku chache zijazo pamoja na mabo mengine litajadili suala hilo na kulitolea uamuzi, viongozi wa kisiasa wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama vya siasa wameutembelea mgodi huo kujionea hali halisi ikiwa ni maandalizi ya mjadala unaotarajiwa kuwa mkali kuhusu tukio hilo.

Sunday, August 19, 2012

EID MUBARAK!!

http://hipish.free.fr/graphics/holiday_comments/eid_fitr_mubarak_saeed/eid_mubarak_002.jpg

 Anga za Kimataifa Inawatakia Waislamu na Waumini wengine wote wenye mapenzi mema na Dini ya Kiislamu heri ya Idd Mubarak !!

Saturday, August 18, 2012

KUNDI LILILOMSHAMBULIA OBAMA LINA UHUSIANO NA REPUBLICAN.

http://a.abcnews.go.com/images/Politics/abc_obl_raid_120815_704x396.jpg
Ben Smith mmoja wa wanakikundi cha OPSEC Education Fund
WASHINGTON DC-MAREKANI,
Kundi la waliowahi kuwa majasusi na makomandoo  katika jeshi la Marekani pamoja na baadhi ya raia wa kawaida waliotoa tangazo lenye kumshambulia rais Obama kuhusu rekodi yake katika mambo ya usalama limebainika kuwa na uhusiano na chama cha Republican.

 Kwa mujibu wa kumbu kumbu zilizokusanywa na ofisi za umma pamoja na wavuti mbalimbali zimeonesha uhusiano kati ya wahusika wakuu katika kundi hilo lililojitambulisha kama OPSEC Education Fund na viongozi wa vitongoji na wa kitaifa kutoka katika chama cha Republican, ambapo katika orodha hiyo wapo wapo mhasibu,mwanasheria na kampuni ya video ya  kundi hilo.


Braden, mshauri wa mambo ya kisheria wa kundi hilo la OPSEC amekiri katika mahojiano kuwa alishawahi mshauri mkuu wa kamati ya taifa ya chama cha Republican mnamo miaka ya 1980 kamati ambayo ndiyo chombo kikuu cha chama ch Republican.Licha ya kuachana na nafasi hiyo Braden amekiri kuendelea kukishauri chama cha Republican katika shughuli mbalimbali za kisiasa, ingawa pia amesema huwa anajishughulisha na wateja wengine wa kawaida katika kazi yake kama mshauri wa kisheria.

Michael Smith,huyu ni mhasibu wa kundi hilo la OPSEC ambaye amethibitika kuwahi kuwa mshauri wa Republican pamoja na rais wa kundi lililokuwa linakiunga mkono chama cha Republican mwaka 2008 kilichotambulika kwa jina la Majority America.

Greener and Hook kampuni iliyotengeneza kipande cha video hiyo, hii ni kampuni ambayo inajitambulisha katika tovuti yake kama kampuni inayohusika na utengenezaji wa vipindi mbalimbali vya televisheni ambapo imeonesha kipande cha video iliyohusika na tuhuma hizo kwa rais Obama ikijitambulisha kama mtengenezaji mkuu.Kampuni hiyo imethibitika pia kuwa na uhusiano na Republican ambapo katika orodha ya wateja wake wakuu imewataja Kamati kuu ya kitaifa ya Republican, Umoja wa mameya wa Republican, Kamati ya mikataba ya Republican, na umoja wa wanawake wa republican.

Huo ni baadhi ya ushaidi uliotolewa katika tovuti mbalimbali na takwimu za ofisi za umma ukichapishwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani kuonesha uhusiano wa wahusika wake na chama cha republican huku ushahidi mwingine ukiwa ni jengo la ofisi linalotumiwa na kudni hilo ambapo limekodiwa kutoka kutoka kwa kampuni ya The Trailblazer Group ambayo ni mshirika wa Republican ingawa kampuni hiyo imekanusha kuwa na uhusiano na kudni hilo zaidi ya upangishanaji wa jengo hilo. Pia mkanganyiko unaopatikana katika maelezo ya kundi hilo ambalo msemaji wake mkuu Bw.Chad Kolton alisema halipo kisiasa na wahusika wake hawajihusishi na siasa maelezo ambayo ni kinyume na ukweli kwani baadhi yao wameonekana kuwa walishiriki katika shughuli za kisiasa mnamo mwaka 2008 akiwemo Bw. Gabriel Gomez.

Kwa upande wa Democrats hawajajibu tuhuma hizo ingawa tayari walishatoa tuhuma kwa Republican kuhusika na kampeni hiyo ya kuwashambulia.Maafisa wa serikali ya Marekani wamesema suala hilo lilishughulikiwa kikamilifu na wahusika walichukuliwa hatua kali huku waandishi wa habari walioandika kuhusu habari za kijasusi kuhusu tukio la ukamatwaji wa Osama bin Laden wakikataa kupata habari hizo kutoka vyanzo vya Ikulu ya Marekani

Monday, August 13, 2012

RAIS WA MISRI AWAONDOA MADARAKANI VIONGOZI WA KIJESHI.



CAIRO-MISRI,
Rais Mohammed Morsi amewaondoa madarakani mkuu wa jeshi na waziri wa ulinzi nchini humo bw.Hussein Tantawi na General Sami Anan pamoja na baadhi ya maafisa wa jeshi na kubatilisha agizo la katiba lililokuwa linalipa jeshi madaraka makubwa. Katika taarifa ya rais huyo iliyosomwa na msemaji wa Bw.Yasser Alli nafasi ya bw.Tantawi imechukuliwa na Abdul-Fatah al-Sessi huku ile ya ukuu wa jeshi ikichukuliwa na Sidki Sayed Ahmed. Waziri huyo na mkuu wa jeshi wote wamepewa madaraka mapya kama washauri wa rais.

Katika mabadiliko mengine jaji mkuu wa nchi hiyo bw. Mahmoud Mekki, ameteuliwa kuwa makamu mpya wa rais.Uteuzi huo umeanza mara moja.

Katika taarifa yake rais huyo ametetea uamuzi wake wa hatua hizo na kusema amelenga uzalendo zaidi na umelenga kukipa nafasi kizazi kipya.

Uamuzi huo umeungwa mkono na kufurahiwa na wananchi wa Misri ambao wamekusanyika kwa maelfu katika viunga vya Tahrir Square leo hii na kuimba wakimsifu rais Morsi.

Uamuzi huo umeelezewa kuwa ni wa muhimu hasa kwa wakati huu ambao shinikizo kubwa lilikuwa ni nkurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo na kuruhusu hali ya kawaida baada ya kuwepo udhibiti mkubwa wa jeshi katika madaraka.






Thursday, August 9, 2012

ALIYEWAHI KUWA BALOZI WA TANZANIA ITALIA AACHIWA HURU.

DAR ES SALAAM-TANZANIA,
Aliyewahikuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, ameshinda kesi iliyokuwa inamkabili  baada ya upande wa mashitaka kuonekana hauna ushahidi wa kujitosheleza.
Prof.mahalu ambaye alikuwa akishitakiwa na serikali kwa kuisababishia hasara ya  Euro 2,065,827.60,  kwa manunuzi ya majengo ya Balozi nchini Italia kinyume cha sheria.
.https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgyPE6dhkIt_DRo2Ai3FKHDA4b37cUMxsqzg4emAjpQ6TuJ9NUOZENsMCcJl744UpZf_gH6lsXoV1a35GiPE9Qjw2wcyCn_eCTvbA3q5DDWpZNXgOMcMW5JpdOulM6Kzn9aYTzn1VGXJmCL/s1600/DSC_0139.JPG
Akisoma hukumu hiyo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu Ilvine Mugeta, amesema Profesa Mahalu  na  aliyekuwa Mkuu wa Fedha na Utawala katika ubalozi huo, Bi.Grace Martin, hawajapatikana na hatia kwa kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka haujajitosheleza na kulingana na hivyo kuwa si wa kweli.
Kwa kigezo hicho hakimu huyo amewaachia huru washitakiwa hao kwa kuwa hawana kesi ya kujibu.

Tuesday, August 7, 2012

WATU 16 WAUAWA KATIKA SHAMBULIO DHIDI YA KANISA NIGERIA



Otite-NIGERIA, 
Watu wenye silaha wamewaua watu zaidi ya 16 kwa kuwapiga risasi katika kanisa katika mji wa Otite karibu na jiji la Okene nchini Nigeria imeripotiwa.Kamanda wa jeshi la Nigeria Bw.Gabriel Olorunyom ameviambia vyombo vya habari kuwa watu hao walivamia kanisa hilo wakati waumini hao walipokuwa katika ibada na kuwafyatulia risasi ambapo Mchungaji wa kanisa hilo ni moja ya waliouawa.






Kamanda huyo amesema watu wengine wengi wamejeruhiwa ingawa haiikuwa rahisi kutaja idadi yake kwa kuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali na wengine wanadhaniwa kukimbia na kujificha.

Tukio hilo limetokea saa 24 baada ya watu 17 kukamatwa na vifaa 34 vya milipuko na mpaka sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na tukio hilo ingawa hisia kubwa ni kwa kundi la Boko Haram ambalo limekuwa likipinga elimu na dini za kimagharibi nchini humo.



Monday, August 6, 2012

WAZIRI MKUU WA SYRIA AJIUNGA NA UPINZANI

http://www.aljazeera.com/mritems/Images/2012/8/6//201286101153313734_20.jpg
Waziri mkuu aliyejiuzuru Bw.Hijab alipokuwa akiapishwa na Rais Al-Assad.

DAMASCUS-SYRIA
Waziri mkuu wa Syria Bw.Riad Farid Hijab, amejiunga na upinzani baada ya kutangazwa kufukuzwa wadhifa wake huo leo asubuhi.Waziri huyo mkuu ameripotiwa kuwasili Jordan leo na kutangaza kujiunga na upinzani,
"Natangaza kuanzia leo kuondoka katika mkondo wa kigaidi na mauaji na kuanzia leo mimi ni mwanajeshi niliyebarikiwa na ninajiunga na kundi la wanamapinduzi na wapigania uhuru" alinukuliwa Hijab katika taarifa yake iliyosomwa na msemaji wake Muhammad el-Etri.
 .
Etri alikanusha pia kuwa waziri mkuu huyo amefukuzwa akisema kuwa serikali imetoa tangazo la kumfukuza baada ya kutambua ameshaondoka nchini Syria.Etri amesema pia kuwa Hijab alikuwa na mpango huo na alikuwa akiwasiliana na jeshi la waasi la Free Syrian Army.

Katika taarifa yake hiyo waziri mkuu huyo mstaafu amewataka viongozi wengine wa Syria kuondoka na kuachana na serikali ya Bw.Al-Assad.
Bila shaka hilo litakuwa ni pigo kubwa kwa Rais Al-Assad ambaye mwezi uliopita aliwapoteza mawaziri wawili katika shambulio la bomu nchini humo.

USAIN BOLT ASHINDA TENA MEDALI YA DHAHABU.

http://www.abc.net.au/news/image/4178898-3x2-700x467.jpgLONDON-UINGEREZA,
Usain Bolt mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani ameonesha umahiri wake baada ya hapo jana kunyakua medali ya dhahabu akishika nafasi ya kwanza katika mbio za mita 100 wanaume, huku akiweka rekodi mpya ya kukimbia mita 100 kwa sekunde 9.63.
 Nafasi ya pili ilienda kwa mjamaika mwenzake Yohan Blake na ya tatu  ikachukuliwa na bingwa wa mbio hizo mwaka 2004 Justin Gatlinwa Marekani.
http://jahkno.com/wp-content/uploads/2012/08/Usain-Bolt-The-Legend-Wins-100m-London-2012-Olympic-111.jpg
 Ushindi huo wa Bolt umedhihirisha ubora wake na utawala katika riadha na kuwaondoa hofu mashabiki wake ambao walihofu angeshindwa kutokana na kuripotiwa kuwa na majeraha ya mkono.Wajamaika ambao hapo jana walikuwa pia wakisheherekea uhuru wa nchi yao wameupokea kwa shangwe ushindi huo.
Bolt sasa atalingana na mwanamichezo Carl Lewis wa Marekani ambaye naye amewahi kupata medali 2 za dhahabu katika mbio hizo za mita 100.


Wajamaica wakishangilia Ushindi huo katika jiji la kingstone -Jamaica.

"Baada ya nusu fainali nilipata ujasiri na kujiamini kwani miguu yangu ilikuwa vizuri na hicho kiliniongezea kujiamini" alisema Bolt baada ya ushindi huo.

Wednesday, August 1, 2012

RIPOTI : MAJESHI YA SERIKALI YA MYANMAR YANAFANYA UNYAMA DHIDI YA WAISLAMU NCHINI HUMO.

Mtoto wa Jamii ya Rohingya akiwa amelala nje ya kambi ya wakimbizi mpakani mwa nchi ya Myanmar.

MYANMAR, 
Majeshi ya serikali ya Myanmar(zamani ikiitwa Burma) yamewaua, kuwabaka na kuwakamata waislamu wa jamii ya Rohingya mara baada ya vurugu za kidini nchini humo zilizotokea mwezi juni, imeripoti taarifa ya Human Right Watch iliyotolewa Jumatano ya leo

Taarifa hiyo pia imesema mamlaka ya serikali nchini humo hazijafanya juhudi zozote kukomesha ukatili huo, huku ikiwazuia na kuwakamata  wanaharakati na wafanyakazi wa kutoa misaada kuingia katika jimbo la Rakhine ambalo ndilo eneo linapofanyika ukatili huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ukatili huo umetokana na serikali kuegemea upande mmoja wa mvutano wa kikabila na kidini kati ya Waislamu wa Rohingya na Mabudha wa Rakhine katika jimbo la Rakhine.

Katika ripoti hiyo ambayo imetokana na uchunguzi pamoja na mahojiano na wakazi wa jamii zote mbili za Rakhine na Rohingya serikali imedaiwa pia kushindwa kuzuia mapigano ya kidini kati ya pande hizo mbili kinyume na ahadi yake ya mwezi Novemba mwaka jana kuwa italinda haki za raia wa nchi hiyo.

"Majeshi ya serikali yameshindwa kuwazuia wananchi kutoka jamii ya Arakan(Rakhine) na Rohingya kushambuliana na badala yake yameongeza kampeni ya kuwashambulia wanajamii ya Rohingya"amesema  Brad Adams mkurugenzi wa Human Right Watch katika bara la Asia.Brad aliongeza kuwa jumuiya ya kimataifa na nchi za kimagharibi zimekuwa zikipotoshwa juu ya kile kinachoendelea nchini humo na Serikali kwa kuoneshwa kuwa hali ni shwari na kuna mabadiliko makubwa katika suala la haki za kibinadamu tofauti na miaka kumi iliyopita chini ya utawala wa kijeshi.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje ya Myanmar Bw.Wunna Maung Lwin  jumatatu iliyopita alipinga tuhuma kuwa serikali yake inaunga mkono unyama huo na kusema kuwa tuhuma zozote dhidi ya serikali yake ni za kisiasa na zinakuzwa kimataifa kwa kuwa serikali yake imejaribu kuondoa tofauti za kidini na kikabila nchini humo, maelezo ambayo yameonekana kupingana na hali halisi ya kinachoendelea.

CHANZO CHA UNYAMA NI NINI?
Waislamu wa Rohingya wapatao laki nane (800,000) nchini Myanmar ni jamii isiyo na taifa kusini mwa Asia kwani wamekuwa hawatambuliwi na serikali ya Myanmar katika makundi ya makabila na dini miongoni mwa jamii nchini humo, hukuBangladesh nchi jirani nayo imekuwa ikiwakataa kama jamii yake. Rais wa Myanmar alitoa msimamo wa kutokukitambua kizazi cha Rohingya kilichokuwepo kabla ya uhuru mwaka 1948 na kusema nchi yake itakitambua kizazi kilichotokea baada ya wakati huo akilitaka shirika la wakimbizi duniani UNHCR kuwachukua wanajamii waliokataliwa kama wakimbizi au kuwahamishia katika nchi nyingine za dunia ya tatu, ambapo Shirika hilo lilipinga kauli yake na kutoa msimamo wa kujihusisha na wakimbizi wanaokimbia nchi zao kwa sababu maalum tu.

Hata hivyo kumekuwa na chuki baina ya jamii ya Rohingya na Rakhine kwa miaka na miaka zikiwa katika pande mbili za kikabila na kidini ambapo warohingya ni waislamu na Rahine ni mabhudha ingawa warakhine wameonekana kuwa na haki zaidi na uungwaji mkono na serikali nchini humo.

Ni wajibu wa jumuiya za kimataifa sasa kuunganisha nguvu za pamoja kukomesha ukatili huo na kuacha kulifungia macho suala hilo ambalo ni janga la kibinadamu.

ZITTO KABWE ATOA MAELEZO TUHUMA ZA RUSHWA KAMATI YA NISHATI NA MADINI.

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiFcG-8Tyt4KBDmgQKIQ2LdwcRina1SI1DqK0uhIMUdxI1nqs4pGz-iIlBEKk4KUklB9qQy2MBBiObrzyKQzZfYcTpgV4mjGegTB4NHj_zSZZBuL72UA41Xjnmta_BFQSwf82_PbCSRvNWM/s1600/ZittoKabwe1.jpg

MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote  zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
  1.   Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
  2.   Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari  zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’  zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
  3.   Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-
  1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya  Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali  (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
  2. Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;
  3. Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu  kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
  4. Baada ya  tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
  5. Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.
  1. Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
  1. Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na  Madaraka  ya  Bunge kwa kina;
  1. Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
  1. Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
  1. Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
  1. Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
  1. Nafarijika na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
  1. Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
  1. Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.
  1. Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.
  1. Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
  1. Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.