Wednesday, August 1, 2012

RIPOTI : MAJESHI YA SERIKALI YA MYANMAR YANAFANYA UNYAMA DHIDI YA WAISLAMU NCHINI HUMO.

Mtoto wa Jamii ya Rohingya akiwa amelala nje ya kambi ya wakimbizi mpakani mwa nchi ya Myanmar.

MYANMAR, 
Majeshi ya serikali ya Myanmar(zamani ikiitwa Burma) yamewaua, kuwabaka na kuwakamata waislamu wa jamii ya Rohingya mara baada ya vurugu za kidini nchini humo zilizotokea mwezi juni, imeripoti taarifa ya Human Right Watch iliyotolewa Jumatano ya leo

Taarifa hiyo pia imesema mamlaka ya serikali nchini humo hazijafanya juhudi zozote kukomesha ukatili huo, huku ikiwazuia na kuwakamata  wanaharakati na wafanyakazi wa kutoa misaada kuingia katika jimbo la Rakhine ambalo ndilo eneo linapofanyika ukatili huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ukatili huo umetokana na serikali kuegemea upande mmoja wa mvutano wa kikabila na kidini kati ya Waislamu wa Rohingya na Mabudha wa Rakhine katika jimbo la Rakhine.

Katika ripoti hiyo ambayo imetokana na uchunguzi pamoja na mahojiano na wakazi wa jamii zote mbili za Rakhine na Rohingya serikali imedaiwa pia kushindwa kuzuia mapigano ya kidini kati ya pande hizo mbili kinyume na ahadi yake ya mwezi Novemba mwaka jana kuwa italinda haki za raia wa nchi hiyo.

"Majeshi ya serikali yameshindwa kuwazuia wananchi kutoka jamii ya Arakan(Rakhine) na Rohingya kushambuliana na badala yake yameongeza kampeni ya kuwashambulia wanajamii ya Rohingya"amesema  Brad Adams mkurugenzi wa Human Right Watch katika bara la Asia.Brad aliongeza kuwa jumuiya ya kimataifa na nchi za kimagharibi zimekuwa zikipotoshwa juu ya kile kinachoendelea nchini humo na Serikali kwa kuoneshwa kuwa hali ni shwari na kuna mabadiliko makubwa katika suala la haki za kibinadamu tofauti na miaka kumi iliyopita chini ya utawala wa kijeshi.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje ya Myanmar Bw.Wunna Maung Lwin  jumatatu iliyopita alipinga tuhuma kuwa serikali yake inaunga mkono unyama huo na kusema kuwa tuhuma zozote dhidi ya serikali yake ni za kisiasa na zinakuzwa kimataifa kwa kuwa serikali yake imejaribu kuondoa tofauti za kidini na kikabila nchini humo, maelezo ambayo yameonekana kupingana na hali halisi ya kinachoendelea.

CHANZO CHA UNYAMA NI NINI?
Waislamu wa Rohingya wapatao laki nane (800,000) nchini Myanmar ni jamii isiyo na taifa kusini mwa Asia kwani wamekuwa hawatambuliwi na serikali ya Myanmar katika makundi ya makabila na dini miongoni mwa jamii nchini humo, hukuBangladesh nchi jirani nayo imekuwa ikiwakataa kama jamii yake. Rais wa Myanmar alitoa msimamo wa kutokukitambua kizazi cha Rohingya kilichokuwepo kabla ya uhuru mwaka 1948 na kusema nchi yake itakitambua kizazi kilichotokea baada ya wakati huo akilitaka shirika la wakimbizi duniani UNHCR kuwachukua wanajamii waliokataliwa kama wakimbizi au kuwahamishia katika nchi nyingine za dunia ya tatu, ambapo Shirika hilo lilipinga kauli yake na kutoa msimamo wa kujihusisha na wakimbizi wanaokimbia nchi zao kwa sababu maalum tu.

Hata hivyo kumekuwa na chuki baina ya jamii ya Rohingya na Rakhine kwa miaka na miaka zikiwa katika pande mbili za kikabila na kidini ambapo warohingya ni waislamu na Rahine ni mabhudha ingawa warakhine wameonekana kuwa na haki zaidi na uungwaji mkono na serikali nchini humo.

Ni wajibu wa jumuiya za kimataifa sasa kuunganisha nguvu za pamoja kukomesha ukatili huo na kuacha kulifungia macho suala hilo ambalo ni janga la kibinadamu.

No comments:

Post a Comment