Friday, March 29, 2013

GHOROFA LAANGUKA DAR ES SALAAM-WATATU WAFA,MAMIA WAKWAMA CHINI.

DAR ES SALAAM-TANZANIA,
Mamia ya wafanyakazi wa ujenzi wanahofiwa kukwama ndani ya jengo lenye ghorofa kumi na mbili lililoanguka mapema leo mjini Dar es Salaam.
"Nilidhani lilikuwa tetemeko la ardhi, na kisha nikasikia mayowe,". "
- shuhuda
Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, watu walisikika wakipiga mayowe kutaka msaada.

"nilidhani lilikuwa tetemeko la ardhi, na kisha nikasikia mayowe,'' alisema shahidi mmoja.

Jengo hilo liko katikati mwa Dar es Salaam na lilianguka saa tatu kasorobo asubuhi kwa saa za afrika mashariki.
Mamia ya watu wanaaminika kuwa ndani ya jengo hilo huku wengine wakiwa nje wakati wa ajali hiyo . Hata hivyo idadi kamili ya watu hao bado haujulikani.











Thursday, March 28, 2013

POLISI WANAFUGA UHALIFU VURUGU ZA KIDINI-PENGO

DAR ES SALAAM-TANZANIA, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku akisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”
“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”". "
- Polycarp Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.

“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na kuongeza:

“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”

Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”
Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la amani.”
Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.

Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.

“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.

“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.

Polisi wanena
Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.

Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.

Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Mwanakwerekwe.

Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.(MWANANCHI).

Wednesday, March 27, 2013

SIRI YA MPANGO WA MAUAJI YA ZITTO KABWE-DR.SILAHA AHUSISHWA







DAR ES SALAAM-TANZANIA,
TISHIO la kuuawa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, sasa limechukua sura mpya, baada ya kuibuika kwa madai mapya kuwa Bosi wake, Dk. Willbrod Slaa, alipanga njama za kumuangamiza, MTANZANIA Jumatano linaripoti.

Duru za habari zinaeleza kuwa Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, anadaiwa alitaka kuuawa kwa sumu na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa, ambaye alimtumia kada na Mjumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Ben Saanane, kutekeleza mpango huo.

Habari zinadai kuwa tukio hilo lilipangwa kutekelezwa Mei mwaka jana, katika Hoteli ya Lunch Time, iliyoko Mabibo External, jijini Dar es Salaam.

Kwamba Zitto alilengwa kuuawa kwa kuwekewa sumu kwenye kinywaji chake wakati akiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya makada vijana wa chama hicho katika Hoteli ya Lunch Time.

Mmoja wa watu waliokuwa katika tukio hilo amelieleza MTANZANIA Jumatano kuwa Zitto alinusurika baada ya aliyetumwa kumuwekea sumu hiyo kuidondosha na hivyo kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo.

Anamtaja mtu aliyetumwa kumuua Zitto kuwa ni Ben Saanane, ambaye aliangusha karatasi ya nailoni iliyokuwa na ungaunga unaosadikiwa kuwa sumu na kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo, akiwemo Zitto mwenyewe pamoja na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano, Shonza alikiri kutokea kwa tukio hilo kwa kueleza kuwa yeye na Mwampamba walihoji kilichokuwa ndani ya nailoni ile, ambacho kilionekana wazi kuwa ni unga unga ni nini, ambapo Saanane alikiri kuwa ilikuwa sumu ambayo alipewa na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto.

Shonza alidai kuwa siku ya tukio, yeye na Zitto walikuwa wamekaa meza moja na Saanane ambaye mkono wake wa kushoto ulikuwa umefungwa bandeji aliyowaeleza kuwa aliifunga kutokana na maumivu ya mkono.

Alisema wakiwa katika maongezi, huku Saanane akionyesha kuzidiwa na kilevi alichokuwa amekunywa, alitoa bahasha ya kaki yenye fedha ili alipie gharama za vinywaji vya wote ambayo ilidondoka na ndani yake ikatoka karatasi ndogo ya nailoni  ikiwa na unga mwekundu.

Kwa mujibu wa Shonza, Saanane alipobanwa aeleze unga ule ulikuwa nini, awali  alidai ni kilevi aina ya kuberi, huku akiwataka wasiifungue nailoni hiyo, jambo ambalo Mwampamba alilikataa na kulazimisha ifunguliwe pale pale.

“Kwa hasira Ben alitaka arudishiwe ile karatasi, lakini, Mwampamba aliondoka nayo, usiku huo huo Saanane alimtafuta Mwampamba hadi nyumbani kwake akidai apewe mzigo wake.

“Mwampamba alimwambia atampa mzigo wake kwa sharti moja tu la kusema ukweli kuhusu kilichomo ndani ya nailoni hiyo na hapo ndipo Ben alipokiri kuwa alipewa mzigo huo ambao una unga unga wenye sumu na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto kwa sababu amekuwa akimsakama ndani ya vikao vya chama.

“Huo ndiyo ukweli ambao nitausema popote, sasa kama Ben alitudanganya kwa kumsingizia Dk. Slaa hiyo ni juu yao wenyewe,” alisema Shonza.

Shonza alisema hali hiyo iliwaogofya na kuanza kuwa makini katika mapito yao na kuongeza kuwa Zitto bado yuko Chadema kwa sababu ana roho ngumu, mvumilivu na mkomavu wa kisiasa, anayeweza kukabiliana na mambo ya hatari.

Dk. Slaa alipoulizwa na MTANZANIA Jumatano kuhusu madai hayo, alisema hilo ni kosa la jinai, ambalo kama anatuhumiwa kulifanya anapaswa kushtakiwa kwenye vyombo vya dola badala ya tarifa hizo kupelekwa katika vyombo vya habari.

“Usipende kutumiwa na watu, lakini aliyekutuma anajua amekutuma kwa sababu gani. Sasa nitakujibu, hivi suala la kuua si ni jinai? Sasa suala la jinai linapelekwa kwenye vyombo vya dola au kwenye vyombo vya habari? Huyo aliyesema yuko Chadema au yuko wapi? Aliyesema hakwenda polisi? Aliyetaka kuuawa hakwenda pia? Sasa ninyi media mmekuwa nani?

“Wa kumuuliza suala hili ni Saanane mwenyewe au Shonza, wangekuwa na nia njema wangekwenda polisi au Zitto mwenyewe angekwenda polisi kushitaki kwa kutaka kuuawa,” alisema Dk. Slaa.

Naye Saanane ambaye amefanya mahojiano na MTANZANIA Jumatano kuhusiana na mambo mbalimbali mabaya ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake, akizungumzia madai hayo alisema madai hayo hayana ukweli wowote, bali yanaibuliwa sasa na mahasimu wake kisiasa kwa lengo la kutaka kumshusha baada ya majaribio mengi dhidi yake kushindwa.

“Kwanza siku ambayo wanasema tulikuwa wote mimi sikuwa huko, nashangaa na haiingii akilini kwamba mimi niende hadi Temeke (kwa Mwampamba) tena usiku wa manane kwa ajili ya kufuata sumu ya kuulia panya.

“Hizi ndizo siasa halisi za maji taka, kuliko nipange njama za kuua mtu kwa malengo ya kisiasa, ni bora niache siasa. Ni mwendawazimu pekee atakayeweza kuamini tetesi hizi za ovyo kabisa zinazofanywa na vijana walioshindwa kujenga hoja za maana kwenye majukwaa,” alisema Saanane.

Aliwaonya watu wanaohasimiana naye kisiasa kuacha kumchafua Dk. Slaa kwa kutumia jina lake katika mambo wanayomtuhumu, kwa kile alichoeleza kuwa ni dhambi kubwa kutunga uongo na kuusambaza ili kutafuta huruma ya umma wa Watanzania.

“Nadhani lengo lao hapa ni kumchafua Dk. Slaa kwa tuhuma hizi za uongo zilizotolewa kwa mara ya kwanza na vijana waliotimuliwa Chadema kwa kukisaliti chama na baadaye kuhongwa na makada na viongozi wa CCM ambao wamejiunga nao sasa.

“Sasa kwa tuhuma hizo, kwa nini wasiripoti polisi, inaingiaje akilini mtu kupanga njama kubwa kiasi hicho halafu ukae kimya tu,” alisema Saanane.(CHANZO:MTANZANIA)


Tuesday, March 26, 2013

ZAIDI YA WANAFUNZI 4,800 HAWAJUI KUSOMA NJOMBE

NJOMBE-TANZANIA,
ZAIDI ya wanafunzi 4,800 wa darasa la nne hadi la saba, katika shule za msingi mkoani Njombe hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu. Hayo yalielezwa na Ofisa Elimu Takwimu mkoani hapa, Sandagila Mgaya, alipotoa taarifa ya elimu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na watendaji mbalimbali wa mkoa, Mgaya alisema hali hiyo ni mbaya na inahatarisha maendeleo ya elimu katika mkoa huo mpya.

Alisema kati ya wanafunzi hao wasiojua kusoma, kuhesabu wala kuandika, wapo 19 wanaosoma kidato cha pili na tatu katika shule za sekondari katika mkoa huo.

Utafiti uliofanywa umebainisha kuwa idadi ya wanafunzi hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu imeongezeka jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu katika mkoa huo, alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi alikiri kuwa hali ya elimu mkoani humo ni mbaya na kuwataka wadau wa kikao hicho kujadili uwezekano wa kutatua tatizo hilo.

Alisema lazima kuhakikisha mkoa huo unapata njia ya kuwasaidia wanafunzi hao waweze kusoma, kuandika na kuhesabu ili kukuza kiwango cha elimu mkoani.

“Hali ya elimu ni mbaya kwa matokeo ya kidato cha nne mpaka cha sita, lakini cha ajabu zaidi wapo wanafunzi wengi wa darala la nne hadi la saba, ambao hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu jambo ambalo ni hatari,” alisema.

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Philemon Luhanjo, aliutaka mkoa huo kutilia mkazo elimu ya watu wazima kuwapa elimu ya stadi za maisha wanafunzi wanaomaliza bila kujua kusoma, kuhesabu na kuandika.

Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wadau wa elimu walisema kutojua kusoma, kuandika na kuhesabau kwa wanafunzi hao kunasababishwa na baadhi ya shule kutokuwa na walimu wa kutosha.

Waliitaka Serikali kupunguza idadi ya masomo kwa wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na la pili ili watiliwe mkazo kusoma, kuandika na kuhesabu peke yake.

Suala la kushuka kiwango cha elimu nchini limekuwa gumzo kubwa nchini hivi sasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walishindwa.

Jambo hilo liliibua mjadala mzito katika kikao cha Bunge kilichopita, hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi ambayo pamoja na mambo mengine alitaka iundwe kamati ya bunge kuchunguza mfumo mzima wa elimu nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekwisha kuunda tume inayochunguza kushindwa kwa kiwango kikubwa kiasi hicho kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana

MAJESHI YA KOREA KASKAZINI YAJIWEKA TAYARI KUSHAMBULIA KUSHAMBULIA KAMBI ZA JESHI LA MAREKANI MJINI HAWAI NA GUAM.

 

PYONGYANG-KOREA KASKAZINI,
Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuviweka tayari vikosi vyake kwenye mstari wa mapambano tayari kwa mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani za mjini Hawaii na Guam pamoja na Kora Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa shirika la utangazaji wa Korea Kaskazini, imesema kuwa amri imetolewa na kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo ambayo inawataka wanajeshi wote kuwa mstari wa mbele tayari kwa kusubiri amri ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani.


Tangazo hilo la Serikali ya Korea Kaskazini linakuja wakati ambapo nchi ya Korea Kusini na Marekani zimemaliza mazoezi ya pamoja ya kijeshi ambayo Korea Kaskazini ilidai kuwa ni uchokozi dhidi ya taifa lao.


Hii si mara ya kwanza kwa Korea Kaskazini kutangaza kutishia kuishambulia nchi ya Marekani ambapo imeapa kutumia silaha za Nyuklia kutekeleza mashambulizi yake dhidi ya maadui zake.

Picha za video zimemuonesha kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un akitembelea kambi za wanajeshi wa nchi hiyo ambao wamekuwa kwenye mazoezi ya kijeshi kujiweka tayari kuilinda nchi yao.

Monday, March 25, 2013

RAIS WA CHINA KUIHUTUBIA DUNIA KUTOKA TANZANIA LEO


DAR ES SALAAM-TANZANIA, Rais wa China, Xi Jinping ambaye aliwasili nchini jana saa 10:05 akitumia ndege Boeng 747 ya Shirika la Ndege la China . Anatarajiwa kuihutubia dunia kuhusu sera za China kwa bara la Afrika leo hii  akitumia jukwaa la Tanzania. 

Jinping atatoa hotuba yake kwenye jengo jipya la kisasa la Mwalimu Nyerere ambalo limejengwa na Serikali ya China likiwa na uwezo wa kuchukua watu 1,800 kwa mara moja lilipo jijini. 

Rais huyo ambaye ameambatana na mkewe pamoja na maofisa mbalimbali wa Serikali yake,anatajiwa kutambulisha sera kwa Bara la Afrika huku wachunguzi wa mambo wakisema kuwa hotuba yake hiyo huenda itazingatia juu ya uimarisha uhusiano mwema baina ya pande zote mbili. 

China ndiyo dola inayotajwa kuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika na katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kiwango cha ufanyaji biashara baina ya pande hizo mbili kinatajwa kukua kwa asilimia 70. China pia ndiyo mshirika pekee kwa Afrika ambaye misaada yake inaambatana na masharti nafuu.

Hata hivyo ushawishi wa China barani Afrika unakosolewa na baadhi ya nchi za Magharibi zinazoituhumu China kwamba inazinyonya nchi za Afrika.
     
"Ziara ya Rais Xi kwa Tanzania imeonesha kuwa China haina malengo ya muda mfupi na Afrika, bali ya muda mrefu pamoja na kujenga urafiki wa karibu.". "
- Frans-Paul van der Putten, Mkuu wa kitengo cha utafiti chuo cha Uhusiano wa kimataifa Uholanzi
Alipowasili jana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa  Mwalimu Nyerere,

 Rais huyo alipokewa na mwenyeji wake Rais Jakaya
 Kikwete na kisha alipigiwa mizinga 21 na baadaye 
alikagua gwaride.
 Baada ya mapokezi hayo ya uwanjani, Rais Jinping
 na mwenyeji wake walioogoza kwenda jijini ambapo
 jioni ya jana walikuwa na mazungumzo ya faragha na
 baadaye walijumuika na halaika kwa ajili ya kushiriki dhifa ya taifa. 

Wakati wa mapokezi vikundi vya ngoma vya utamaduni vilipendezesha mapokezi hayo kutokana na burudani ya kusisimua iliyotolewa. Hata hivyo baadhi ya wapiga picha walijikuta kwenye wakati mgumu baada ya Maofisa Usalama wa China waliokuwa wakiwatimua wapiga picha hao. 

Katika ziara yake, Rais wa China na Tanzania zitatiliana saini mikataba 17 inayohusu maendeleo na uimarishwaji uhusiano wa kidiplomasia. Waziri wa Mambo ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe alisema kuwa China inakusudia kuipiga jeki Tanzania katika maeneo ya miundo mbinu, soko la kibiashara na sekta ya habari na mawasiliano.

“ Pamoja na kwamba leo Rais Jinping atazungumzia sera yake kuhusu Afrika, lakini pia anatazamia kukabidhi rasmi funguo za jengo la Mwalimu Nyerere kwa Rais Kikwete ambalo Serikali ya China imejenga. Jengo hili lina uwezo wa kuchukua watu 18,000 na kwetu sisi ni fahari kubwa” alisema Waziri Membe.

Hii ni ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu alipochukua wadhifa huo wiki tatu zilizopita. Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kutembelewa na kiongozi huyo ambaye pia serikali yake imehaidi kujenga bandari mpya ya Bagamoyo.

Baada ya kutoa hutuba yake kwenye ukumbi mpya wa Mwl. Nyerere Jinping atatembelea makaburi ya wataalamu wa China na baadaye ataelekea Afrika Kusin ambako kesho atashiriki mkutano unaoshirikisha nchi tano zilizopiga hatua kimaendeleo Brics. Nchi zinazounda umoja wa huo ni pamoja na China, Brazil, Urusi na Afrika Kusini.

Thursday, March 21, 2013

OBAMA KUZULU PALESTINA LEO.


 


Ramalla-Palestina,
Baada ya kuwasili Israel hapo jana Rais wa Marekani Barack Obama atakuwa na ziara ya nchini Palestina leo na kufanya mazungumzo na rais wa Palestina Bw.Mahmoud Abbas.Mazungumzo ya Obama na Abbas yataangazia zaidi mzozo wa amani kati Palestina na Israel ambao kwa muda mrefu haujapata suluhu.

Obama anazuru Ramalla kwa saa kadha kabla ya kurejea Bethlehem kutoa hotuba kwa raia wa Israel kuhusu uhusiano kati ya Israel na Palestina na mchango wa Marekani kuhakikisha kuwa amani inadumu katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, raia wa Palestina wanasema hawaoni umuhimu wa ziara ya Obama katika Mamlaka hiyo kwa kile wanachokisema kuwa tangu rais huyo wa Marekani alipoingia madarakani hajawafanyia chochcote .

Ziara ya Obama inakuwa ni ziara yake ya kwanza kwenye eneo la Mashariki ya kati tangu kuchaguliwa kwake kwa muhula wa pili kama kiongozi wa taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.

Obama amemwambia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa ,Marekani haina rafiki wa dhati kama Israel na itaendelea kujenga uhusiano thabiti kati ya mataifa hayo mawili.

Kuhusu Iran rais Obama amesema kuwa nchi hiyo ina nafasi ya kujirekebisha kuhusu mpango wake wa Nyuklia kupitia njia za kidiplomasia kuepuka nguvu za kijeshi kutumiwa dhidi yake.

Tuesday, March 19, 2013

MAREKANI YARUSHA NDEGE ZA B52 KOREA KUSINI-NI TISHIO KWA KOREA KASKAZINI.


b52h-strategic-bomber
Ndege aina ya B52 ikiwa hewani

Kabla ya kuruka

SEOUL-KOREA KUSINI,
Marekani imerusha ndege zenye uwezo wa kuzuia mabomu ya Nyuklia na kubeba silaha nzito katika kile ilichoelezea kama itikio kwa vitisho vya Korea ya Kaskazini ambayo hivi karibuni imetishia kuishambulia.
"Tunaonesha uwezo kuwa tumepanua uwezo ambo ni muhimu dhidi ya tishio la Korea Kaskazini" Alisema msemaji wa Pentagon Bw. George Little.

Marekani imeonekana kutilia maanani tishio la hivi karibuni la Korea Kaskazini, ambapo hivi karibuni ilipitisha bajeti ya zaidi ya trilioni 1.5 kuboresha mitambo yake ya kutungua makombora makubwa yakiwemo ya Nyuklia huko iliyopo katika ardhi yake kama kinga dhidi ya shambulizi lolote, hali ambayo ni changamoto kwa Korea Kusini na Japan ambao pia ni maadui wa Korea Kaskazini.

Saturday, March 16, 2013

ZITTO ATIKISA KAMATI ZA BUNGE

https://zittokabwe.files.wordpress.com/2012/04/zkwasanii2.jpg?w=490&h=320
DAR ES SALAAM-TANZANIA,MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ameonekana kuwa tisho kubwa ndani ya Kamati za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tishio la Zitto, lilionekana wazi jana, wakati wa uchaguzi wa kuwapata wenyeviti na makamu wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, baada ya kumbwaga Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tangu mwaka 2005.

Katika uchaguzi huo, ulioongozwa na kanuni za Bunge, Zitto aliibuka na ushindi wa kura 13 dhidi ya 4 za Cheyo, kati ya kura 17 za wajumbe.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa PAC kwa kuibuka na ushindi wa kishindo wa kura 13 na kumshinda mpinzani wake, Zainabu Vullu, ambaye aliambulia kura 4.
Akizungumzia ushindi huo, Zitto alisema: “Nimekabidhiwa majukumu mazito mno, hizi ni kamati mbili ndani ya kamati moja, nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote.

“Lakini ushindi huu, umekuja sababu naamini wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakubanwa kama ilivyokuwa zamani, demokrasia imeachwa imechukua mkondo wake zaidi,” alisema Zitto.

Akitangaza matokeo hayo, katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa kanuni za Bunge na kwamba uchaguzi huo unakamilisha ngwe ya pili ya uhai wa Bunge uliosalia hadi mwaka 2015.

Hata hivyo, Kamati ya Bajeti ya Bunge inatarajiwa kuendelea na uchaguzi siku ya Jumatatu, baada ya jana kamati hiyo kushindwa kumpata makamu mwenyekiti kutokana na kura za wajumbe kufungana. Mwenyekiti wa kamati hiyo ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), ambaye aliteuliwa moja kwa moja na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Akizungumzia kamati hiyo, Joel alisema: “Spika alimteua Mbunge wa Bariadi Magharibi kuwa mwenyekiti wa kamati hii kutokana na uzoefu alionao, hasa katika masuala ya uongozi na utumishi wake ambao aliwahi kuupata akiwa serikalini,” alisema na kuongeza:

“Hii Kamati ya Bajeti ni roho ya Bunge na kutokana na umuhimu wake pamoja na kupata uzoefu kutoka katika mabunge ya Jumuiya ya Madola, mara nyingi Spika hupewa nafasi ya kuteua mwenyekiti ambaye ana uzoefu, hasa katika masuala ya uongozi, ambao ameupata kutokana na mara nyingi anatoka chama tawala.

“Kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Spika Makinda, alimteua Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa kamati hii, huku wajumbe wa kamati wakipewa kazi ya kuchagua makamu mwenyekiti. Hata hivyo kutokana na kuwa na upinzani mkali, kura zilipigwa mara mbili ambapo hakuna aliyeibuka mshindi, hali iliyowafanya wajumbe wakubaliane kurudia siku ya Jumatatu,” alisema Joel.

Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) ambaye hakugombea nafasi hiyo. Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi (CCM), amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Alisema Kamati ya Fedha na Uchumi, aliyechaguliwa ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahamud Mgimwa (CCM), huku makamu wake akiwa ni Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula (CCM).

Kuhusu Kamati ya Huduma za Jamii, aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jenista Mhagama, ametetea nafasi yake, huku Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wake, akichukua nafasi ya Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia.

Kamati ya Nishati na Madini iliyokuwa imevunjwa kabla ya muda wake na Spika Anne Makinda kutokana na wajumbe wake kukumbwa na tuhuma za rushwa, imepata viongozi wapya.

Viongozi hao, ni Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti, huku Mbunge wa Lulindi, Jorome Bwanausi akichaguliwa kuwa makamu.

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli pamoja na makamu wake Abdukarim Shah, walipita bila kupigwa, huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ametetea nafasi yake baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu na Makamu Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya.

Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imechukuliwa na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangalla (CCM), huku makamu wake akiwa Mbunge wa Manyoni Magharibi, Paul Lwanji. Kamati ya Ukimwi aliyekuwa mwenyekiti wa awali, Lediana Mng’ong’o alifanikiwa kuitetea vema nafasi hiyo pamoja na makamu wake, Diana Chilolo, wote wabunge wa Viti Maalumu (CCM).

Alisema Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, aliyechaguliwa ni Anna Abdallah na makamu wake ni Mohamed Seif Khatib na Kamati ya Mambo ya Nje aliyechaguliwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), huku Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu akichaguliwa kuwa makamu wake.

Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala, Pindi Chana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na aliyekuwa Waziri wa Naishati na Madini, William Ngeleja, akiibuka kidedea kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambapo Kamati ya Maadili, aliyechaguliwa ni Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi na makamu wake ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati.

Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na Makamu wake, Said Nkumba.

Ratiba ya Bunge kubadilika

Joel alisema hatua ya Bunge kubadili ratiba ya vikao vyake vya Bunge la bajeti, imekuwa wakati muafaka ambapo hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri kwa upande wa Bunge na Serikali kwa ujumla.

Friday, March 15, 2013

PAPA FRANCIS AFANYA MAAJABU KATIKA SIKU YAKE YA KWANZA.

 

VATCAN-ITALIA,
PAPA Francis I ameonesha maajabu katika siku yake ya kwanza ya upapa, baada ya jana kwenda katika hoteli aliyofikia kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa wa 266 katika historia ya Kanisa Katoliki duniani, kuchukua mizigo yake na kulipa bili yeye mwenyewe.

Hali hiyo, iliashiria kuachana na staili za watangulizi wake, ambao wamezoea kufanyiwa shughuli kama hizo na watumishi wao, huku wenyewe wakijifungia ndani ya nyumba za gharama ambazo kuta zake zimenakishiwa kwa dhahabu za mjini Vatican.

Jambo la pili ambalo lilionekana kuwavutia wengi, ni pale alipoachana tena na desturi za mapapa waliopita, uchaguzi wa mavazi ya kipapa ya Francis I ulijidhihirisha kwa kuvalia vazi la kawaida lisilotofautiana na lile la zama zake za uaskofu.

Askofu huyo wa zamani wa Buenos Aires, Argentina, Kardinali Jorge Bergoglio, alianza siku yake ya kwanza kwa kufanya ziara kwa kutumia gari la kawaida la Vatican kuelekea Basilica la Roman ili kufanya maombi kwa Bikira Maria, akilenga kulileta kanisa karibu na watu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, alihudhuria misa ya maombi katika Kanisa la Santa Maria Maggiore mjini Roma, ili kuanza kazi yake kama mkuu wa Wakatoliki bilioni 1.2 kote duniani.

Papa huyo wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, alipokea ujumbe na salamu mbalimbali kutoka duniani kote kumtakia heri.

Miongoni mwao, ni Rais wa Marekani, Barack Obama, aliyemtaja Bergoglio kuwa mtetezi wa masikini na wanyonge, huku Makamu wake, Joe Biden akitarajia kuongoza ujumbe wa nchi hiyo katika sherehe za kumsimika zitakazofanyika Jumanne wiki ijayo.

Aidha Waziri Mkuu wa Australia, Julia Gillard, alisema kuchaguliwa Papa kutoka ‘ulimwengu mpya’ ni tukio ambalo lina umuhimu wa kihistoria.

Viongozi wengine, waliotuma pongezi ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Rais wa Argentina, Cristina Kirchner.

Francis, ambaye ndiye Papa wa kwanza asiyetoka Ulaya katika kipindi cha takribani miaka 1,300, aliitumia ibada yake ya kwanza kumwombea mtangulizi wake, Benedict VXI na kutoa wito wa kuwepo udugu miongoni mwa waumini wa Kikatoliki.

Lakini Muargentina huyo, pia anakabiliwa na mlolongo wa changamoto ngumu zinazolikabili kanisa hilo.

Kanisa hilo, limekumbwa na migawanyiko mikubwa ya ndani na kashfa zilizowakumba makasisi za kuwadhalilisha watoto kingono na tuhuma za ufisadi na kuvuja kwa nyaraka za siri.

Awali alikuwa ameuambia umati wa watu 100,000 uliofurika katika kiwanja cha Mtakatifu Petro kwamba amepanga kumwomba Bikira Maria ili auangalie mji mzima wa Rome.

Aliwaambia makardinali kwamba atamtembelea Papa mstaafu Benedict XVI, lakini Vatican ilisema ziara hiyo itafanyika siku chache zijazo.

Ratiba kuu ya Papa Francis I, jana ilikuwa kuzindua ibada ya jioni katika Kanisa dogo la Sistina, ambako makardinali juzi usiku walimchagua kuwa kiongozi wa kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2.

Anatarajia kutumia zaidi Kiitaliano na kuachana na utamaduni wa Benedict ambaye alijikita zaidi katika Kilatini.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, anayesemekana kushika nafasi ya pili nyuma ya Papa Benedict XVI alipochaguliwa mwaka 2005, alichaguliwa katika raundi ya tano kumrithi papa huyo wa kwanza kujiuzulu kipindi cha miaka 600. Soma zaidi makala kuhusu Papa huyu mnyenyekevu ukurasa wa 26.

SILAHA AZUNGUMZIA KUKAMATWA KWA LWAKATARE


DAR ES SALAAM-TANZANIA,
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, ameibua madai mazito dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa, baada ya kudai kuna maofisa watatu wa ngazi za juu wa idara hiyo wanahusika na mipango ya kudhoofisha chama hicho.

Dk. Slaa, alisema maofisa hao, ambao aliwataja majina hadharani jana, ndio wanaodaiwa kupanga mikakati ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alidai mpango wa kukamatwa kwa Lwakatare uliandaliwa na maofisa watatu wa ngazi za juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.


Alisema mpaka sasa, chama hicho kimefanikiwa kupata majina ya maofisa hao ambao wanaaminika kupanga mikakati ya kutaka kudhoofisha mipango na maendeleo ya chama hicho.

Lwakatare alikamatwa juzi akihusishwa na tuhuma za kupanga mikakati mbalimbali ya kushambulia na kudhuru watu mbalimbali, wakiwamo waandishi wa habari.

Alisema mkakati wa kumkamata Lwakatare na wabunge wengine wa chama hicho, ulianza tangu mwaka jana, baada ya kuwapo na barua nyingi feki zilizokuwa zikibuniwa na kuonekana zimesainiwa na Lwakatare, Dk. Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Nilipata taarifa Machi 11, mwaka huu kutoka kwa mmoja wa maofisa Usalama wa Taifa, Lwakatare atakamatwa, katika hili sasa imedhihirika kile tulichoambiwa na wasiri wetu ndicho kimetokea.

“Bahati nzuri gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), limesema Lwakatare anatuhumiwa kupanga njama za kumdhuru Mhariri wa gazeti hilo, na kwamba amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, sasa sisi hatujui walitoa taarifa hizo wapi.

“CHADEMA tunafurahia kama utaratibu huu, utafuata sheria na kuanika ukweli wa tukio hilo, kwani linafanana na kutekwa kwa Kibanda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka,” alisema Dk. Slaa.

“Chadema tunasema, aliyekuwa anamhoji Lwakatare akamatwe ili kila mtu amjue na picha zake zinazoonyeshwa kwenye mtandao ili kuondokana na upuuzi huu,” alisema.

“Mpaka sasa, Lwakatare bado anashikiliwa na polisi na hata chakula tulichopeleka asubuhi kimekataliwa kupokelewa…tunasisitiza tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kumpa dhamana pindi tutakaporuhusiwa.

“Tunarudia kusema mara zote, tumekuwa tukimshauri Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi, lakini ameendelea kuwa kimya, leo tunarudia kusema hatuna imani na tume za polisi kwani ni moja ya kundi linalohusishwa na matukio ya kuteka na kutesa.

“Tunapenda kuwaambia Watanzania na dunia nzima, CHADEMA hakina nia ya kuzuia polisi wasifanye kazi zao, tunataka wafuate sheria na taratibu zilizowekwa, katika hili la kutaka kutudhoofisha na kuminya uhuru wa vyombo vya habari hatutalivumilia liendelee.

“Tunasema ifike wakati propaganda za Serikali ziachwe na haki itendeke kwa manufaa ya taifa, itakumbukwa chama hiki na wanachama wake, kimekuwa kikisumbuliwa hata bungeni wabunge wameondolewa katika kamati na zingine kuvunjwa, bila kambi ya upinzani kuhusishwa,” alisema.

Pamoja na mambo mengi na historia ya matukio ya utekeji, kuuawa na kujeruhiwa, Dk. Slaa alimuomba Rais Kikwete kuwaeleza Watanzania juu ya kauli aliyoitoa Adis Ababa nchini Ethiopia, wakati wa mkutano wa Mpango wa Kujitathmini katika Utawala Bora (APRM) kwamba gazeti la Mwanahalisi lilifungiwa kutokana na kuandika habari za uchochezi.

Dk. Slaa, alimuomba Rais Kikwete kutumia mamlaka aliyonayo kulifungulia gazeti la Mwanahalisi, kwani ni haki ya kila Mtanzania kupata habari.

Vile vile alisema wakati umefika watuhumiwa wote waliotajwa katika matukio mbalimbali ya kuteka, kupiga, kujeruhiwa na kuua kuchukuliwa hatua katika vyombo vya sheria.

Lwakatare alikamatwa juzi na maofisa watatu wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupanga mikakati mbalimbali ya kudhuru watu, wakiwamo waandishi wa habari ambapo hadi jana, alikuwa akishikiliwa na polisi.

Hatua ya kushikiliwa Lwakatare, imekuja baada ya kuonekana kwenye CD iliyorekodiwa, akionekana akipanga mikakati hiyo.

Inadaiwa CD hiyo ilirekodiwa Desemba 28, mwaka jana na inaonekana kwa muda wa dakika saba tu.

Thursday, March 14, 2013

PAPA MPYA APATIKANA-MATUKIO KATIKA PICHA

Papa Mpya Jorge Bergoglio





Papa Francis akijitokeza mbele ya umati wa waumini Vatican na kuwabariki.



ROME-ITALIA,
HATIMAYE Kanisa Katoliki duniani, limemchagua Kardinali Jorge Bergoglio kuwa Papa mjini Rome nchini Italia jana. Papa huyo kutoka Argentina, alichaguliwa jana baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kutokana na aliyekuwa akiishikilia, Papa Benedict XVI kujizulu nafasi hiyo, Februari 28 mwaka huu.

Dalili za kupatikana kwa papa huyo, zilitanguliwa na moshi mweupe uliofuka kutoka mnara wa paa la Kanisa dogo la Sistina, Vatican mjini Rome Italia jana usiku ukiitangazia dunia kwamba makardinali waliokusanyika ndani ya kanisa hilo wamemchagua papa mpya wa kuliongoza kanisa hilo. Umati wa watu ukiwa na miavuli, uliujaza uwanja huku ukipeperusha bendera za mataifa mbalimbali duniani.
Baada ya saa kadhaa za kukabiliana na baridi kali na mvua kubwa, umati mkubwa ulipaza sauti za kushangilia tukio hilo ‘Habemus Papam’ na ‘Tuna papa’ huku kengele za Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na za makanisa mengine ya mjini Rome zikilia.

Ndani ya saa moja baadaye mrithi wa Papa Benedict XVI akafahamika kuwa ni Askofu Mkuu wa Buenos Aires nchini Argentina, Jorge Mario Bergoglio, ambaye amechagua jina la Papa Francis I.

Uchaguzi wa papa huyo mpya wa 266 mwenye umri wa miaka 76 na ambaye anakuwa papa wa kwanza asiyetoka barani Ulaya na wa tatu asiye Muitaliano, ulipokelewa kwa shangwe kubwa na makumi kwa maelfu ya Wakatoliki katika viwanja hivyo vya Mtakatifu Petro.

Alipojitokeza katika kibaraza cha kanisa hilo, papa mpya alianza hotuba yake kwa utani, akisema kaka zake makardinali wamekusanyika kumchagua Askofu wa Rome na kwamba wameshamchagua mmoja wao kutoka mbali ambaye ni yeye.

Kisha akasali kumuombea mtangulizi wake ambaye bado yu hai yaani Papa Benedict XVI.

Katika maneno yake, alisema, “Kwanza kabisa napenda kumuombea Papa wetu mstaafu Benedict XVI, kwamba Kristo na Bikira Maria wawe naye.

“Tuwe katika safari hii pamoja, safari hii kwa Kanisa la Roman Katoliki ni safari ya urafiki na upendo na imani baina yetu, tuombeane kila mmoja wetu, tuwaombee wote duniani,” alisema Papa Francis.

Baada ya kusema hayo, akautaka umati kukaa kimya kwa muda na kumuombea wakati akikubali kupokea wadhifa huo mpya kwake.

“Naomba mniombee kwa Mungu ili anibariki,” Papa Francis alisema, akiongoza sala ya kimya kimya, akifuatiwa na vifijo kutoka kwa umati wa watu.

Pia alisema dunia inapaswa kuonyesha njia ya upendo na mtangamano na wakati akiondoka aliuambia umati huo, kwamba usiku mwena na ninawatakia mapumziko ya amani.

Papa Francis anazungumza kwa ufasaha lugha za Kijerumani, Kihispania na Kiitaliano.

Makardinali 115 walikuwa wakikutana kwa siku ya pili jana kumchagua mrithi wa Papa Benedict XVI, ambaye uamuzi wake wa mwezi uliopita wa kutangaza kujiuzulu uliwashangaza wengi baada ya kushikilia wadhifa huo kwa miaka minane.

Uamuzi huo pia ulimfanya Papa Bebedict XVI aweke rekodi ya kuwa papa wa kwanza kujiuzulu katika miaka 600 ya historia ya Kanisa Katoliki.

Makardinali 115 walikuwa wamejitenga na dunia tangu Jumanne wiki hii na tangu kipindi hicho, walikuwa wamepiga kura mara nne ambapo moshi mweusi ulijitokeza ukiashiria papa bado hajapatikana.

Theluthi mbili au sawa na makardinali 77 miongoni mwao, walikuwa wakitakiwa wawe wamemchagua mmoja miongoni mwao ili awe kiongozi wa kanisa hilo.

Kabla ya mkutano huo maalumu maarufu kama conclave kuanza, kulikuwa hakuna mtu aliyekuwa akitajwa kupewa nafasi kubwa ya kumrithi Papa Benedict XVI.

Pamoja na Papa Francis I kushika wadhifa huo, anakabiliwa na wakati mgumu katika kipindi ambacho Kanisa Katoliki limezongwa na kashfa mbalimbali pamoja na migawanyiko ya ndani.

Atatakiwa kusafisha ufisadi katika makao makuu ya kanisa yaani Vatican pamoja na kufufufua ukatoliki katika kipindi ambacho watu wanazidi kujitenga na dini.

Awali, migawanyiko na ugumu wa kumpata mtu mmoja mwenye sifa za kukabiliana na changamoto hizo kwa mujibu wa wachambuzi wengi, ulitabiriwa kuwa ungewafanya makardinali kuwa na mchakato mrefu wa kumpata papa kuliko ule wa 2005 ulioshuhudia chaguzi nne kumpata Papa Benedict XVI.

Awali, kundi la walinzi wa Kiswisi wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi ikiwamo kofia ngumu za rangi ya fedha waliandamana kuelekea katika Kanisa Kuu kwa maandalizi ya kutangazwa kwa Papa mpya huku bendi za jeshi zikiwaburudisha walioshuhudia.

Wednesday, March 13, 2013

MCHAKATO WA KUMPATA PAPA-MAKADINARI WASHINDWA KUKUBALIANA SIKU YA KWANZA


Jopo la makadinari huko Vatcan.


Moshi mweusi ukitoka katika paa huko Vatcan.
 ROME-ITALIA,
Moshi mweusi umetokea kwenye dari la hekalu ya Sistine mjini Roma, kumaanisha kuwa makadinali walioko ndani ya hekalu wameshindwa kuafikiana juu ya Papa mpya anayetarajiwa kuchaguliwa.
Moshi mweupe utaashiria kupatikana kiongozi mpya wa kanisa Katoliki la Roma.
Makadinali hao wanatarajiwa kupiga kura mara nne kwa siku hadi pale thuluthi mbili ya makadinali wote watakapoafikiana juu ya Papa mpya.

Walipiga kura yao ya kwanza ambayo haikuleta maafikiano hapo usiku wa Jumanne. Yeyote atakayeteuliwa kuliongoza kanisa hilo katoliki anakabiliwa na wakati mgumu, ambapo kanisa limezongwa na kashfa mbali mbali pamoja na migawanyiko ya ndani.

Papa aliyeondoka Benedikt wa Kumi na sita aliwashangaza wengi alipotangaza kujiuzulu wadhifa huo miaka minane tu tangu kuchaguliwa. Yeye ndiye Papa wa kwanza kujiuzulu katika miaka 600 ya historia ya kanisa hilo.
Alitoa sababu kuwa amezeeka na afya yake imedhoofika kwa hivyo haoni kuwa anaweza kutekeleza wajibu wake kikamilifu kama Papa wa kanisa.

Tuesday, March 12, 2013

MCHAKATO WA KUMPATA PAPA MPYA WAANZA ROME-ITALIA


 











                                Mji wa Rome-Italia

ROME-ITALIA,
Makadinali wa Kanisa katoliki duniani wamekutana mjini Roma nchini Italia kuanza zoezi la kumchagua papa mpya wa kanisa hilo atakayeziba pengo lililoachwa na Papa Benedicto wa kumi na sita aliyejiuzulu rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita. Asubuhi hii Makadinali 115 watashiriki katika misa ya pamoja kabla ya kuanza mchakato wa kumtafuta kiongozi mpya kuanzia jumanne hii. Makadinali hao watapiga kura mara nne kila siku hadi theluthi mbili watakapo kubaliana kuhusu ni nani atakayekuwa kiongozi wao. Wakati wote wa uchaguzi huo Makadinali hao watajifungia katika chumba maalum hadi pale makadinali 77 watakapoafikiana kuhusu Papa mpya. Zoezi hili huenda likachukua siku kadhaa na papa atakayechaguliwa atakuwa papa wa 266 wa kanisa hilo na kuwaongoza wakatoliki takribani bilioni 1 nukta mbiili duniani kote. Papa Mpya atachukua nafasi ya Papa Emeritus zamani akifahamika kama Benedicto wa kumi na sita aliyejiuzulu mwezi uliopita kwa sababu ya umri mkubwa wa miaka 85 na sababu za kiafya. 

Wafanyakazi zaidi ya 90 watakuwepo kuwasaidia makadinari hao, wakiwemo wafanya usafi, madereva, madaktari, na wahudumu wengineo.

CHADEMA YALIWEKEA NGUMU BUNGE- IPO TAYARI WABUNGE WAKE WAFUKUZWE NA SIYO KUHOJIWA


MARA-TANZANIA,
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kiko tayari wabunge wake wafukuzwe ubunge lakini hawatahojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kama ilivyotangazwa.
Msimamo wa CHADEMA unakuja zikiwa ni siku mbili tangu ofisi ya Bunge itumie Jeshi la Polisi kuwataarifu baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa wanahitajika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na kamati hiyo.
Akitangaza msimamo wa CHADEMA jana mjini Musoma katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa suala hapa si wabunge wa CHADEMA, bali wawakilishi wa wananchi.

Katika tamko hilo maalumu kama ‘Tamko la Musoma’, Mbowe alisisistiza kuwa kamwe wabunge wao hawatakwenda kuhojiwa kwenye hiyo kamati ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM).
Alisema kuwa kama ni kuwafukuza ubunge, wako tayari na kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, ajaribu kufanya hivyo.
Wabunge wengi wa chama hicho pamoja na wengine wa NCCR-Mageuzi walidaiwa na Spika wa Bunge kuwa walifanya vurugu wakati wa kikao pale walipogomea uamuzi wa Naibu Spika, Job Ndugai, kuhusu hatua yake ya kuhitimisha kibabe hoja binfsi ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia.
Pia wabunge hao wanadaiwa kukwamisha kwa muda shughuli za Bunge katika kikao kilichofuata baada ya kusimama na kupinga uamuzi wa Ndugai wa kuiondoa hoja binafsi ya mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Mbowe aliwaambia maelfu ya wafuasi wa chama hicho kuwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge namba 113 (7), inayozungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge, uhai wake unaishia mkutano wa kumi wa Bunge ambapo inakuwa ni nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge lenyewe.

“Kwa hiyo kamati hiyo inayowaita wabunge wa CHADEMA, iliisha uhai wake siku Bunge la Kumi lilipoahirishwa, yaani Februari 8, 2013,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mbunge wa Hai.
Aliongeza kuwa kanuni ya 113 (10), inazungumzia nafasi ya mwenyekiti, kwamba uenyekiti wa kamati ya Bunge unakoma mkutano wa 10 ambapo inakuwa ni nusu ya uhai wa Bunge, kwa hiyo uhai wa Ngwilizi kama mwenyekiti uliisha Februari, siku ile Bunge lilipoahirishwa.
“Hivyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge kamati hiyo haipo na mwenyekiti wake alishamaliza muda wake,” alisisitiza Mbowe.
Alisema kuwa wamewaita wabunge wa CHADEMA kwa sababu ya vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, 2013, wakati wanajua kuwa kamati hiyo tayari ilishalifanyia kazi jambo hilo, ikatengeneza tuhuma, ikaendesha mashtaka, ikatoa hukumu, ikiwataja hata wahusika.
Wahusika waliotajwa ni Tundu Lissu, John Mnyika, Paulina Gekul (Viti Maalum) na Joshua Nassari.

Mbowe aliongeza kuwa watambue kuwa kamati hiyo inapokaa huwa ni sawa na mahakama, kwa kawaida kisheria na kikanuni, mahakama/kamati hiyo inapokuwa imeshaamua jambo haiwezi tena kamati hiyo hiyo kulikalia na kulifanyia kazi jambo hilo hilo.
“Mbele ya Watanzania wote, Tanzania nzima na dunia nzima ikisikia, kamati ile iliwahukumu wabunge wa CHADEMA bila hata kuwasikiliza itakuwa kichekesho; dunia nzima inajua hivyo, sasa wanataka kusikiliza nini tena, wakosaji wanajulikana, walihukumiwa bila hata kufuata taratibu,” alisema.
Kuhusu maandamano ya kumshinikiza Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, kuachia ngazi kutokana na matokeo mabovu ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni, Mbowe alisema yatafanyika Machi 25 mwaka huu katika majiji manne.
Aliyataja majiji hayo kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi mitaani kushiriki maandamano hayo.
Mbowe aliwataka wenye baiskeli, bajaj, pikipiki, magari kujitokeza kwa wingi mitaani huku akilionya Jeshi la Polisi kutothubutu kuingilia kuvuruga maandamano hayo.
CHADEMA kupitia kwa Mbowe ilitoa siku 14 kwa waziri na naibu wake kuachia ngazi tangu Februari 18 mwaka huu, kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni.

Alisema kuwa viongozi hao ndio walichangia matokeo hayo mabaya kutokana na kutowajibika ipasavyo hivyo lazima wahakikishe wanaondoka hata kwa kulazimishwa.
Mbowe alisema Kawambwa na Mulugo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

Katika matokeo hayo, Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.
Katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la pili 6,453, la tatu 15,426, la nne 103,327 na daraja sifuri wako 240,903.

Monday, March 11, 2013

FIFA YATISHIA KUIFUNGIA TANZANIA



 
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MTUHUMIWA MKUU WA UBAKAJI INDIA AJINYONGA GEREZANI

Mwili wa Singh ukitolewa gerezani .
Ram Singh 
DELHI-INDIA, Mtuhumiwa  katika kesi ya ubakaji wa msichana mmoja wa chuo kikuu ambaye baadaye alifariki nchini India, amekutwa akiwa  amefariki ndani ya gerezanila Tahir nchini India  alipokuwa akishikiliwa.

Kwa mujibu wa polisi wamesema kuwa Ram Singh, alijinyonga akiwa ndani ya gereza la Tihar mjini Delhi's Tihar, ingawa mawakili wa utetezi wanadai kuwa huenda alinyongwa.
Ram Singh, aliyekua na umri wa miaka 33, alikuwa mmoja wa washukiwa katika kesi ya ubakaji wanaozuiliwa na polisi kwa madai ya mauaji ya msichana waliyembaka.
Wote walikanusha madai hayo.

Shambulizi dhidi ya mwanafunzi huo, lililofanyika Desemba mwaka jana, lilizua mjadala mkali nchini India kuhusu udhalilishwaji na ukatili dhidi ya wanawake.

Washukiwa wengine wa ubakaji bado wanazuiliwa katika gereza hilo.Kesi ya mshukiwa wa sita inaendeshwa katika mahakama ya watoto.

Mwandishi wa BBC Sanjoy Majumder,mjini Delhi,amesema kuwa kifo cha bwana Singh kinakuja kama aibu kubwa kwa maafisa ambao wanakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu kesi hiyo.
Msemaji wa jela hiyo Sunil Gupta, aliambia BBC kuwa Ram Singh alijinyonga kwa banketi usiku wa kuamkia leo.(CHANZO:BBC)

VURUGU ZAANZA KENYA-MWANASHERIA MKUU MSTAAFU KUMTETEA ODINGA


 
   NAIROBI-KENYA,
  Polisi wa kutuliza ghasia juzi walilazimika kutumia mabomu ya machozi Mjini Kisumu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga kutangazwa kwa matokeo ya urais ambayo mgombea wao, Raila Odinga alianguka.
Vurugu hizo ziliibuka, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.
Maelfu ya vijana wamekuwa wakirandaranda kwenye maeneo kadhaa ya Kisumu wakichoma majengo na kufunga barabara, huku wakiimba: “Bila Raila, hakuna amani.”
Vurugu hizo zilizoanza juzi jioni zimesababisha maduka kufungwa huku makundi ya vijana wenye hasira wakiendelea kurandaranda mitaani wakipambana na polisi ambao walifanya jitihada za kuwatuliza na kurejesha amani.
Ilielezwa kwamba, muda mfupi tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi, zaidi ya vijana 100 waliibuka na kuanza kuwarushia mawe polisi na muda mfupi baadaye idadi ya vijana hao iliongezeka na kusambaa katika maeneo karibu yote ya Kisumu.
Odinga ambaye alikuwa mgombea wa Muungano wa Cord, amewataka wafuasi wake kuwa watulivu kwa kuwa anahitaji kufuata mkondo wa sheria kupinga matokeo hayo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa juzi, yalimpa ushindi Kenyatta aliyesimama kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee, wa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 43 alizopata Raila.
Raila atinga mahakamani
Muungano wa Cord, leo utawasilisha vielelezo mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ametajwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la wanasheria watakaopinga ushindi wa Kenyatta.
Jopo hilo la wanasheria linaongozwa na mwanasheria mkongwe, George Oraro na baadhi ya mawaziri wakiwamo; Mutula Kilonzo, James Orengo na Ababu Namwamba ambao ni washauri wakuu wa jopo.
Oraro alimtetea aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Henry Kosgei wakati alipokabiliwa na kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, The Hague.
Wengine wanaounda timu hiyo ni Gitobu Imanyara, Pheroze Nowrojee, Chacha Odera, Ambrose Rachier na Paul Mwangi.
Cord imepanga kufungua kesi ikitaka Mahakama itengue hatua ya kutangazwa kwa Kenyatta kuwa Rais wa Kenya kwa kuwa taratibu za ukusanyaji matokeo zilikiukwa.
Tangu juzi, jopo hilo la wanasheria lilikuwa na vikao mfululizo kuandaa ushahidi wa kesi hiyo ikiwamo kukusanya vielelezo watakavyosimamia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu namba 163 cha Katiba ya Kenya.
Mfuasi wa Uhuru afariki
Shamrashamra za kushangilia ushindi wa Kenyatta ziliingia doa kwenye Mji wa Nyeri baada ya lori lililobeba mashabiki wa mgombea huyo kutumbukia kwenye korongo na kuua mtu mmoja. Katika ajali hiyo watu 30 walijeruhiwa lakini wakiwa katika hali mbaya.
Mwili wa mtu aliyefariki ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Nyeri wakati wengine waliojeruhiwa wamelazwa kwenye hospitali hiyo.(MWANANCHI)






Thursday, March 7, 2013

UCHAGUZI KENYA: RAILA ODINGA ATAKA KUSIMAMISHWA ZOEZI LA KUHESABU KURA.



NAIROBI-KENYA

Mgombea mweza wa Waziri Mkuu Raila Odinga, na Makamu wa Rais anayemaliza muda wake Kalonzo Musyoka ametoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchini Kenya IEBC kusitisha zoezi la kuhesabu kura za Urais baada ya kubainika kwa kasoro katika baadhi ya maeneo.


,Musyoka kutoka muungano wa kisiasa wa CORD amesema wana uthibitisho kuwa kumekuwa na udanganyifu katika zoezi hilo kwani katika baadhi ya maeneo kura za jumla zimekuwa zikizidi idadi ya wapiga kura waliojisajili hapo awali.
Licha ya kutoa kauli hiyo, Musyoka amewataka wananchi wa Kenya kuwa watulivu wakati huu kwani tuhuma hizo alizozitoa hazina lengo la kuhimiza maandamano ama vurugu kwani muungano wao unajiendesha kwa misingi ya sheria.

Maswali kadhaa yameendelea kuibuka baada ya mfumo wa uhesabuji kura wa kielekroniki wa IEBC kupata hitilafu na kulazimika zoezi la uhesabuji wa kura kuanza upya kwa njia ya kawaida.
Wakati hayo yanajiri IEBC imekuwa ikiendelea na uhesabuji wa kura hizo za Urais na imesema itatoa matokeo ya mwisho ifikapo siku ya Ijumaa asubuhi.
Licha ya IEBC kushindwa kutoa matokeo ndani ya saa arobaini na nane kama ilivyoahidi hapo awali kumekuwa na utulivu wakati wananchi wakiendelea kusubiri kinachoendelea kutoka Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi ambapo matokeo rasmi yanaendelea kutolewa.
Kwa matokeo ya hivi sasa mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa Jubilee Uhuru Kenyatta anaongoza akifuatiwa na Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye ni mgombea wa muungano wa CORD.

MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI "ABSALOM KIBANDA" APELEKWA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU









Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahahariri na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd,Absalon Kibanda akipakiwa kwenye ndege ya Kampuni ya Flightlink tayari kwa safari ya kwenda nchini Afrika Kusini kwa Matibabu baada ya kuvamiwa usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya,alipokuwa akirudi nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

MWILI WA RAIS HUGO CHAVEZ WAAGWA-KUZIKWA IJUMAA

Mwili wa Marehemu Hugo Chavez katika gari.






Maelfu ya raia wa Venezuela wakiusindikiza mwili wa aliyekuwa rais wao.






Mwili wa Chavez umelazwa katika kituo cha mafunzo ya kijeshi mjini Caracas na marais wa nchi jirani walifika kutoa heshima zao za mwisho akiwemo Rais wa Bolivia Evo Morales na mwenzake wa Argentina Cristina Fernandez de Kirchner.
Add caption




Mwili wa aliyekuwa rais wa VEnezuela Bw. Hugo Chavez, Umepitishwa kwenye umati mkubwa wa wafuasi wake katika mitaa ya mji mkuu Caracas kuagwa na wafuasi na wananchi wa nchi hiyo.Kwa sasa  mwili huo umelazwa katika kituo cha mafunzo ya jeshi katika mji mkuu Caracas.
Watu wengi waliangua kilio huku wakichukua picha za kiongozi wao aliyefariki dunia .Mama yake na watoto wake walikusanyika mbele ya jeneza kutoa heshma zao .
Katika shughuli hiyo iliyoongozwa na makamu wa rais wa nchi hiyo Bw.Nicolas Maduro.


Mwili wa rais Chavez umepelekwa katika chuo cha kitaifa cha mafunzo ya kijeshi ambapo utazikwa kesho Ijumaa.
Bwana Chavez alifariki akiwa umri wa miaka 58 baada ya kuugua Saratani kwa zaidi ya miaka miwili.
Maelfu ya watu awali walikwenda barabarani mjini Caracas kutoa heshima zao za mwisho kwa Chavez wakifuatana na gari lililokuwa limebeba jeneza lake kuelekea katika chuo cha mafuzno ya jeshi.
Mazishi ya kitaifa ya Chavez yatafanyika Ijumaa.
Mkuu wa ulinzi wa Rais alinukuliwa akisema kuwa alikuwa na bwana Chavez alipofariki.
Generali Jose Ornella, alisema kuwa Chavez alifariki kutokana na mshtuko wa moyo na katika siku zake za mwisho kabla ya kifo cha ealisema angependa kuendelea kuishi.
Jeneza lake lililokuwa limefunikwa bendera ya nchi hiyo uliwekwa katika ukumbi ambao ni kumbukumbu ya waliopigania uhuru wa watu wa Amerika ya Kusini
Maelfu ya watu walipanga foleni kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Chavez, wakiwemo maafisa wa serikali na viongozi wa Amerika ya Kusini,kama Rais wa Bolivia Evo Morales na Rais wa Argentina Cristina Fernandez de Kirchner.

Wednesday, March 6, 2013

UCHAGUZI KENYA-MITAMBO YALETA KIZAA ZAA, KENYATTA BADO ANAONGOZA

Kenyan authorities are trying to guard against fraud and violence when they hold a presidential election on March 4. Here, voters register on biometric equipment last December in Nairobi. (Image credit: AFP/Getty Images)NAIROBI-KENYA,
Kufikia sasa asilimia 42 ya kura za urais nchini Kenya zimehesabiwa na kuwasilishwa rasmi kwa tume ya uchaguzi IEBC kupitia mitambo ya electroniki.
Hata hivyo kumekuwepo malalamishi kuhusu kucheleweshwa kwa shughuli ya kujumlisha kura kutokana na hitilafu ya mitambo.

Uhuru Kenyatta, anayekabiliwa na kesi katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC, angali anashikilia uongozi huku kura za urais zikiwa bado zinahesabiwa.Huu ni uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika tangu ghasia za baada ya mwaka 2007/2008 kufuatia matokeo yaliyozua utata.

Kenya iliendelea kuwa mbele kwa hesabu ya matokeo ya mwanzo dhidi ya mpinzani wake waziri mkuu Raila Odinga katika siku ya pili ya shughuli ya kuhesabu kura zaidi ya masaa 36 baada ya shughili ya upigaji kura kukamilika.

Raila Odinga alidai kuibiwa ushindi wake mwaka 2007 wakati matokeo yalizua ghasia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki moja huku maelfu wakiachwa bila makao.

Wakati mamilioni ya wakenya walijitokeza kupiga kura kwa amani siku ya Jumatatu,watavyopokea matokeo ya mwisho ya kura ndio itakuwa ishara ya uthabiti wa nchi hiyo.

Ni asilimia arobaini na moja ya kura zilizohesabiwa huku kukiwa na vituo zaidi ya elfu thelathini ambako kura zilipigiwa.
Ni zaidi ya kura milioni tano zilizohesabiwa kutoka kwa wapiga kura milioni 14.3 waliokuwa wamesajiliwa.

RAIS WA VENEZUELA HUGO CHAVEZ AFARIKI DUNIA

 
CARACAS-VENEZUELA,
Katika taarifa kwa taifa, makamu wa rais wa Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez ametoweka katika hadhira ya nchi hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa mara ya kwanza tangu maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali ya kijeshi kuendelea kupokea matibau. Hata hivyo maelezo zaidi hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu  mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao.
Bwana Chavez amekua uongozini nchini Venezuela kwa miaka 14 na anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha ya raia wa pato la chini.

Ujumbe wa Jeshi

Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa wataendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.

Wasifuwa Chavez

Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini.

Chavez na jamii ya kimataifa
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.