Saturday, March 16, 2013

ZITTO ATIKISA KAMATI ZA BUNGE

https://zittokabwe.files.wordpress.com/2012/04/zkwasanii2.jpg?w=490&h=320
DAR ES SALAAM-TANZANIA,MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ameonekana kuwa tisho kubwa ndani ya Kamati za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tishio la Zitto, lilionekana wazi jana, wakati wa uchaguzi wa kuwapata wenyeviti na makamu wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, baada ya kumbwaga Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tangu mwaka 2005.

Katika uchaguzi huo, ulioongozwa na kanuni za Bunge, Zitto aliibuka na ushindi wa kura 13 dhidi ya 4 za Cheyo, kati ya kura 17 za wajumbe.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa PAC kwa kuibuka na ushindi wa kishindo wa kura 13 na kumshinda mpinzani wake, Zainabu Vullu, ambaye aliambulia kura 4.
Akizungumzia ushindi huo, Zitto alisema: “Nimekabidhiwa majukumu mazito mno, hizi ni kamati mbili ndani ya kamati moja, nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote.

“Lakini ushindi huu, umekuja sababu naamini wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakubanwa kama ilivyokuwa zamani, demokrasia imeachwa imechukua mkondo wake zaidi,” alisema Zitto.

Akitangaza matokeo hayo, katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa kanuni za Bunge na kwamba uchaguzi huo unakamilisha ngwe ya pili ya uhai wa Bunge uliosalia hadi mwaka 2015.

Hata hivyo, Kamati ya Bajeti ya Bunge inatarajiwa kuendelea na uchaguzi siku ya Jumatatu, baada ya jana kamati hiyo kushindwa kumpata makamu mwenyekiti kutokana na kura za wajumbe kufungana. Mwenyekiti wa kamati hiyo ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), ambaye aliteuliwa moja kwa moja na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Akizungumzia kamati hiyo, Joel alisema: “Spika alimteua Mbunge wa Bariadi Magharibi kuwa mwenyekiti wa kamati hii kutokana na uzoefu alionao, hasa katika masuala ya uongozi na utumishi wake ambao aliwahi kuupata akiwa serikalini,” alisema na kuongeza:

“Hii Kamati ya Bajeti ni roho ya Bunge na kutokana na umuhimu wake pamoja na kupata uzoefu kutoka katika mabunge ya Jumuiya ya Madola, mara nyingi Spika hupewa nafasi ya kuteua mwenyekiti ambaye ana uzoefu, hasa katika masuala ya uongozi, ambao ameupata kutokana na mara nyingi anatoka chama tawala.

“Kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Spika Makinda, alimteua Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa kamati hii, huku wajumbe wa kamati wakipewa kazi ya kuchagua makamu mwenyekiti. Hata hivyo kutokana na kuwa na upinzani mkali, kura zilipigwa mara mbili ambapo hakuna aliyeibuka mshindi, hali iliyowafanya wajumbe wakubaliane kurudia siku ya Jumatatu,” alisema Joel.

Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) ambaye hakugombea nafasi hiyo. Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi (CCM), amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Alisema Kamati ya Fedha na Uchumi, aliyechaguliwa ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahamud Mgimwa (CCM), huku makamu wake akiwa ni Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula (CCM).

Kuhusu Kamati ya Huduma za Jamii, aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jenista Mhagama, ametetea nafasi yake, huku Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wake, akichukua nafasi ya Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia.

Kamati ya Nishati na Madini iliyokuwa imevunjwa kabla ya muda wake na Spika Anne Makinda kutokana na wajumbe wake kukumbwa na tuhuma za rushwa, imepata viongozi wapya.

Viongozi hao, ni Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti, huku Mbunge wa Lulindi, Jorome Bwanausi akichaguliwa kuwa makamu.

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli pamoja na makamu wake Abdukarim Shah, walipita bila kupigwa, huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ametetea nafasi yake baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu na Makamu Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya.

Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imechukuliwa na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangalla (CCM), huku makamu wake akiwa Mbunge wa Manyoni Magharibi, Paul Lwanji. Kamati ya Ukimwi aliyekuwa mwenyekiti wa awali, Lediana Mng’ong’o alifanikiwa kuitetea vema nafasi hiyo pamoja na makamu wake, Diana Chilolo, wote wabunge wa Viti Maalumu (CCM).

Alisema Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, aliyechaguliwa ni Anna Abdallah na makamu wake ni Mohamed Seif Khatib na Kamati ya Mambo ya Nje aliyechaguliwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), huku Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu akichaguliwa kuwa makamu wake.

Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala, Pindi Chana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na aliyekuwa Waziri wa Naishati na Madini, William Ngeleja, akiibuka kidedea kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambapo Kamati ya Maadili, aliyechaguliwa ni Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi na makamu wake ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati.

Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na Makamu wake, Said Nkumba.

Ratiba ya Bunge kubadilika

Joel alisema hatua ya Bunge kubadili ratiba ya vikao vyake vya Bunge la bajeti, imekuwa wakati muafaka ambapo hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri kwa upande wa Bunge na Serikali kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment