Tuesday, January 29, 2013

WAZIRI MKUU WA SOMALIA ANUSURIKA KATIKA SHAMBULIO LA BOMU


 

SOMALIA,
Mtu mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga nchini Somalia ambapo mshambuliaji amejilipua karibu na ofisi za waziri mkuu
Mlinzi mmoja aliyeshuhudia shambulio hilo alisema kuwa polisi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa.

Lakini kwa mujibu wa maafisa wa utawala, watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea karibu na makao ya Rais mjni Mogadishu.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Sheikh mjini Nairobi anasema kuwa maafisa wakuu wanaelezea kuwa lengo la mshambuliaji lilikuwa kulipua ofisi ya waziri mkuu Abdi Farah Shirdon.
Lakini wanajeshi waliokuwa wanashika doria walisema walimzuia kufika katika ofisi hiyo.
Aidha maafisa walidokeza kwamba mshambuliaji alijilipua alipokuwa anahojiwa katika kizuizi kimoja cha polisi karibu na ofisi hiyo.
Mshambuliaji alijilipua karibu na ukuta unaotenganisha ubalozi wa Ethiopia na makao ya waziri mkuu.

Majengo hayo mawili yako ndani ya eneo ambalo pia linahifadhi makaazi ya rais.
Idadi ya washambuliaji wa kujitoa mhanga imekuwa ikipungua tangu wanamgambo wa Al Shabaab kuondoka Mogadishu kuanzia Agosti 2011 lakini hili li dhihirsiho la changamoto inayowakabili maafisa wa usalama katika kupambana na wanamgambo hao.(BBC)

SUMAYE KUNYANG'ANYWA SHAMBA

 


PWANI-TANZANIA,
SHAMBA la Frederick Sumaye lililoko Kisarawe mkoani Pwani, liko hatarini kuchukuliwa na halmashauri ya wilaya hiyo na kuligawa upya, kutokana na Waziri Mkuu huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza.

Habari zilizothibitishwa na viongozi kadhaa wa Wilaya ya Kisarawe, zimeeleza kuwa shamba la Sumaye lililoko eneo la Vikurunge Kata ya Kiluvya, ni miongoni mwa mashamba yaliyoko kwenye orodha ya kunyang’anywa na kugawiwa upya.

Hata hivyo mwenyewe amesema kuwa hana taarifa ya mpango huo wa halmashauri kuwanyang’anya watu mashamba.

“Sijui chochote na nipo kanisani, Sijui hata hiyo notisi ya halmashauri kutaka kunyang’anya mashamba,” alisema na kukata simu.

Chanzo cha habari kilisema “Huu ni mpango wa halmashauri na tayari imeshatoa tangazo tangu mwaka jana. Ilitoa siku 60 tangu Desemba 30 mwaka jana kwa wamiliki wake kuyaendeleza mashamba hayo, baada ya hapo yatanyang’anywa,” chanzo cha habari kilieleza na kuendelea;

“Mheshimiwa Sumaye ni miongoni mwa wamiliki hao, yeye shamba lake lina zaidi ya ekari 40 na lipo eneo la Vikurunge Kata ya Kuluvya. Ameshindwa kuliendeleza kwa kipindi cha miaka mitano sasa.”

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makurunge, Jocline Mfuru alikiri Sumaye kumiliki eneo kubwa eneo hilo, lakini alisema taarifa zaidi zipo halmashauri ndio ambao wanajua zaidi kwani hata yeye mwenyewe ni mgeni katika nafasi hiyo ana mwezi mmoja tu tangu awepo hapo baada ya mtendaji wa awali kuondolewa.

“Sina muda mrefu katika nafasi yangu na ninatambua notisi ya siku 60 ya wale ambao hawajaendeleza mashamba lakini siwezi kuzungumzia zaidi kwani sina taarifa za kutosha,” alisema Mfuru.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe, Yona Maki alithibitisha kutekelezwa kwa operesheni hiyo na kusema kuwa sasa wapo katika hatua ya kufanya tathamini.
Akiwa amekwepa kuthibitisha kama shamba la Sumaye nalo litanyang’anywa, Maki alisema, “Ni kweli Sumaye anamiliki eneo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na amejenga nyumba ya kuishi.”

Aliendelea “Lakini, kujenga nyumba hakutoshi kueleza kuwa shamba hilo limeendelezwa. Tunapitia nyaraka zinazohusu umiliki wake na kuona kama lipo kwenye mpango huo au la.”
Maki alisema uchunguzi unaofanyika dhidi ya Sumaye ni pamoja na kujua aliomba kumilikisha eneo hilo kwa ajili ya shughuli gani na kuangalia iwapo kile alichoombea ndicho anachokitekeleza.

“Nipe muda niweze kujua alimilikishwa kwa ajili ya utekelezaji wa jambo gani na kama hicho alichoombea ndicho anachokifanya,” alisema Maki.

Maki alifafanua kuwa hatua ya kupitia upya umiliki wa mashamba wilayani humo na uendelezwaji wake, inafanyika kwa mujibu wa sheria ya vijiji na miji namba 4 na 5 ya mwaka 1999.(MWANANCHI)

Wednesday, January 23, 2013

UHABA WA MADAKTARI BINGWA WAIKUMBA MUHIMBILI

DAR ES SALAAM-TANZANIA,

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inakabiliwa na upungufu wa madaktari  bingwa wa upasuaji, hususan katika kitengo cha watoto wanaougua maradhi ya saratani (cancer surgeons).

Upungufu huo unaelezwa umetokana na baadhi ya madaktari bingwa waliokuwapo awali kufariki dunia mwaka jana, baadhi kuacha kazi na wengine kustaafu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini madaktari bingwa wawili walifariki dunia mwaka jana, ambao ni Dk. Enock Sayi na Dk. Profesa Primo Carneiro, wakati Dk. Catherine Mng’ong’o anaelezwa kuacha kazi, huku Dk. Petronella Ngiloi akistaafu kwa mujibu wa sheria.
Habari zilizopatikana hospitalini hapo na kuthibitishwa na mamlaka husika, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinasema mbali na hospitali hiyo Kuu ya Taifa kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa, inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa mashine za oksijeni za kisasa za ukutani.

Mashine za oksijeni zilizopo zinadaiwa kufanya kazi chini ya kiwango kinachotakiwa.
Lakini msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja,  pamoja na kukiri kuwapo kwa upungufu huo wa madaktari bingwa, amesema hilo haliwezi kuathiri shughuli za tiba katika kitengo hicho cha magonjwa ya watoto.
Aidha, anasema hospitali hiyo imesheheni vifaa vya kisasa, zikiwamo mashine hizo za oksijeni, zinazotumika kumsaidia mgonjwa kupumua.

Uchuguzi uliofanywa na gazeti hili katika Jengo la Watoto na kwenye baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini pia kuwapo kwa vichwa vya mashine za mitungi ya oksijeni vikiwa vimezungushiwa plasta kuzuia uvujaji hovyo wa hewa hiyo, hali inayohatarisha afya za wagonjwa wanaolazwa katika wodi zenye mashine hizo.
“Hayo mambo yanashughulikiwa na Bodi ya Muhimbili pamoja na Mkurugenzi wake. Kama masuala hayo unayouliza yatahitajika kufika wizarani, ndipo hapo na sisi tunaweza kutolea ufafanuzi, lakini ninavyojua Muhimbili kuna vifaa vyote vya kisasa na ndiyo maana imeitwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili,” alisema  Mwamwaja.

Mmoja wa madaktari bingwa wa Muhimbili, ameliambia gazeti hili kwamba tangu walipofariki madaktari bingwa wenzake; Dk. Sayi na Profesa Carneiro mwaka jana, nafasi zao hadi sasa hazijajazwa.
Aidha, daktari bingwa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa sababu zilizo wazi kabisa, amethibitisha kuwapo kwa tatizo la madaktari bingwa katika kitengo cha saratani, baada ya Dk.  Ngiloi kustaafu.

Alisema awali baada ya Dk. Ngiloi kustaafu, Dk. aliyechukua nafasi yake hiyo katika kitengo hicho  alikuwa Dk. Mng’ong’o, lakini kwa sasa anadaiwa kuacha kazi hospitalini hapo.

BARAZA LA USALAMA LAONGEZA VIKWAZO KWA KOREA KASKAZINI

PYONG YANG-KOREA KASKAZINI,
Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa UN limeagiza kuwekwa kwa vikwazo zaidi dhidi ya Serikali ya Korea Kaskazini kufuatia nchi hiyo kuendelea kukaidi maazimio ya baraza hilo kuhusu kurusha maroketi wanayodai ni ya kisayansi.
Kwenye vikwazo hivyo vipya baraza hilo limeiongeza mamlaka ya anga ya nchi hiyo, benki, makampuni ya biashara na watu wanne ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali ya Pyongyang katika kutekeleza mpango wake wa kutengeneza roketi za masafa marefu.

Mapendekezo hayo ambayo yaliwasilishwa na nchi ya Marekani, yalipitishwa bila kupingwa na nchi wanachama 15 wa kudumu wa baraza hilo na kulaani kile ambacho imekiita ni ukaidi wa taifa hilo.

Mwezi Desemba mwaka jana nchi ya Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya kombora lake la masafa marefu kuelekea angani, jaribi ambalo yenyewe imesisitiza halihusiani na utengenezaji wa silaha za masafa marefu kama inavyodaiwa na nchi za magharibi.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo Suzan Rice amelitaka baraza hilo kuchukua hatua zaidi iwapo nchi ya Korea Kaskazini itaendelea kukaidi maazimio ya Umoja huo.

Nchi za Marekani na China zimekuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali ya Pyongyang katika kujaribu kuishawishi nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kutengeneza makombora ya masafa marefu.

Licha ya vikwazo hivyo Serikali ya Pyongyang imeapa kuendelea na majaribio yake na kwamba hivi karibuni itateeleza jaribio jingine la roketi.

Tuesday, January 22, 2013

LULU AIOMBA MAHAKAMA IMWACHIE HURU.


DAR ES SALAAM- TANZANIA,
 MSANII wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imwachie huru kwa dhamana.

Lulu kupitia kwa wakili wake aliwasilisha ombi hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na Ijumaa jaji anayeisikiliza kesi hiyo anatarajia kutoa uamuzi.


Tangu kilipotokea kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba, Aprili 7, mwaka jana Lulu amekuwa akisota mahabusu na dhamana yake ikawa imezuiwa kwa mujibu wa kesi za mauaji.

Hata hivyo baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia hivyo kumuweka katika mazingira ya kupatiwa dhamana. Habari zilizopatikana mahakamani hapo jana zilisema kuwa tayari maombi hayo ya dhamana yamepangwa kusikilizwa na Jaji Zainabu Muruke, Januari 25 ,2013.


Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake linadhaminika.


Katika hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona yanafaa.

Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama hii tukufu.”

Alidai kuwa akiwa wakili wa mwombaji, anatambua kuwa mwombaji anao wadhamini wa kuaminika ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.

Wakili Kibatala katika hati yake hiyo ya kiapo anadai kuwa akiwa wakili wa mshtakiwa, ikiwa mshtakiwa huyo atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.

Aliendelea kudai kwamba kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo amepata fursa kubwa ya kufahamiana na mwombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo anajua kuwa mwombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.


“Mwombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake ambao wako tayari kuhakikisha kuwa anatimiza masharti na kuhakikisha kuwa anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote’, alisema.

“Mwombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam na hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa masharti yoyote ya dhamana,” anasisitiza Wakili Kibatala na kuongeza:

MKAPA AJITOSA MJADALA WA GESI.

DAR ES SALAAM-TANZANIA,RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameelezea kufedheheshwa kwake na mgogoro wa gesi, huku akiwataka wananchi na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mtwara kusitisha harakati za maandamano na mihadhara.
Mkapa alitaka wakazi hao kuacha kulumbana na Serikali kuhusu suala hilo, badala yake wajiandae kukaa meza moja nayo kutafuta mwafaka kwa njia ya amani.
Katika tamko lake alilolitoa Dar es Salaam jana, Mkapa alisema: “Fujo, vitisho, kupimana nguvu na malumbano siyo masharti ya maendeleo.
“Nikiwa kama mwana - Mtwara na raia mwema, mpenda nchi, nimefedheheshwa sana na matukio haya ya siku za karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara, kusitisha harakati hizi na maandamano na mihadhara.
“Badala yake wajipange kukaa pamoja katika meza moja,  kupitia historia, kutathmini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji wake, hatimaye kufikia mwafaka wa ujia wa maendeleo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.”
Mkapa alisema mwenendo wa mazungumzo, maandamano na mikutano ya hadhara inayoendelea mkoani Mtwara, inaelekea kuashiria kuvunjika kwa amani hali aliyosema kuwa inajenga kutokuelewana kati ya viongozi wa vyama vya siasa na Serikali, wananchi na vyama vya siasa na wananchi na viongozi wa Serikali.
“Mtafaruku huu haufai kuachwa na kutishia usalama, mipango ya maendeleo siyo siri, mikakati na mbinu za utekelezaji wake siyo siri,” alisema Mkapa na kuongeza:
“Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo rasilimali zinawanufaisha wananchi wa eneo zilimo na taifa zima.”
Mkapa alisema hali hiyo ni tishio kwa wawekezaji wa ndani na nje, kwani mara zote hawapendi vurugu, fujo na vitisho.
Kauli hiyo ya Mkapa imekuja siku kadhaa tangu kuwapo kwa maandamano na vurugu zinazofanywa na baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanaopinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.
Tayari viongozi kadhaa akiwamo Rais Jakaya Kikwete wametoa tamko juu ya suala hilo wakionya kuwa halikubaliki kwa kuwa rasilimali hiyo si kwa ajili ya wana Mtwara pekee.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyalaani maandamano hayo akisema walioyaandaa wamelenga kuigawa nchi vipandevipande, Chadema kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumbana waziri huyo ili aondoe udhaifu uliopo katika sekta ya nishati.
Desemba mwaka huu, maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyoratibiwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo, zikiwamo Tandahimba na Newala  yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara Mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.(MWANANCHI).

Monday, January 21, 2013

RATIBA NA BAADHI YA MATOKEA YA KOMBE LA MATAIFA 2013


 

Group A:

1. Angola | P: 1 | Pointi: 1

2. Cape Verde | P: 1 | Pointi:1

3. Morocco | P: 1 | Pointi: 1

4. South Africa | P: 1 | Pointi: 1

Matokeo ya mechi za kundi A

19/01/2013 Afrika Kusini 0 Cape Verde 0
19/01/2013 Angola 0 Morocco 0
________________________________________
23/01/13:
  • Afrika Kusini dhidi ya Angola (Saa Kumi na mbili Jioni)
  • Morocco dhidi ya Cape Verde (Saa Tatu za Usiku)
27/01/13:
Afrika Kusini dhidi ya Morocco (Saa Mbili za Usiku)
Cape Verde dhidi ya Angola (Saa Mbili za Usiku)

Group B

1. Mali | P: 1 | Pointi: 3

2. DR Congo | P: 1 | Pointi: 1

3. Ghana | P: 1 | Pointi:1

4. Niger | P: 1 | Ponti: 0

Matokeo ya mechi za kundi B

20/01/2013 Ghana 2 DRC 2
20/01/2013 Mali 1 Niger 0
_________________________________________________________
24/01/13:
  • Ghana dhidi ya Mali (Saa Kumi na Mbili za Jioni)
  • Niger dhidi ya DR Congo (Saa Tatu za Usiku)
28/01/13:
Ghana dhidi ya Niger (Saa Mbili za Usiku)
DR Congo dhidi ya Mali (Saa Mbili za Usiku)

Group C

1. Zambia | P: 0 | Pointi: 0

2. Nigeria | P: 0 | Pointi: 0

3. Ethiopia | P: 0 | Pointi: 0

4. Burkina Faso | P: 0 | Pointi: 0

_________________________________________________________

21/01/13:
Zambia v Ethiopia (Saa Kumi na Mbili Jioni)
Nigeria v Burkina Faso (1 (Saa Tatu za Usiku)
25/01/13:
  • Zambia dhidi ya Nigeria (Saa Kumi na Mbili za Usiku)
  • Burkina Faso dhidi ya Ethiopia (Saa tatu za Usiku)
29/01/13:
  • Zambia dhidi ya Burkina Faso (Saa Mbili za Usiku)
  • Ethiopia dhidi ya Nigeria (Saa Mbili za Usiku)

Group D

1. Ivory Coast | P: 0 | Pointi: 0

2. Algeria | P: 0 | Pointi: 0

3. Tunisia | P: 0 | Pointi: 0

4. Togo | P: 0 | Pointi: 0

_________________________________________________________
22/01/13:
  • Ivory Coast dhidi ya Togo (1500) ()
  • Tunisia dhidi ya Algeria (1800) ()
26/01/13:
  • Ivory Coast dhidi ya Tunisia (1500) ()
  • Algeria dhidi ya Togo (1800) ()
30/01/13:
  • Ivory Coast dhidi ya Algeria (Saa Mbili za Usiku)
  • Togo dhidi ya Tunisia (Saa Mbili za Usiku)

ROBO FAINALI

02/02/13:
  • Mshindi wa kundi B kupambana na timu ya pili kundi A (Saa Kumi na Mbili za Usiku)
  • Mshindi wa kundi A kumbana na timu ya pili kundi B (Saa tatu na nusu za Usiku)
03/02/13:
Mshindi wa kundi D dhidi ya timu ya pili kundi C (Saa Kumi na mbili jioni)
Mshindi wa kundi C dhidi ya timu ya pili kundi D ( (Saa tatu na nusu za Usiku)

NUSU FAINALI

06/02/13:
Mshindi wa robo fainali ya pili dhidi ya mshindi wa robo fainali ya tatu saa (Saa Mbili za Usiku)
Mshindi wa robo fainali ya nne dhidi ya mshindi wa robo fainali ya kwanza (Saa tatu na nusu za Usiku)

MSHINDI WA TATU

09/02/13:
Timu itakayoshindwa katika mechi ya nusu fainali (Saa tatu Usiku)

FAINALI

10/02/13:
Washindi wa mechi ya nusu fainali (Saa Tatu za Usiku)

Thursday, January 17, 2013

PEP GUARDIOLA ATUA BAYERN MUNICH

_65329389_guardiola_empics2

BAYERN MUNICH-UJERUMANI,
Miamba ya soka nchini Ujerumani, klabu ya Bayern Munich, imetangaza rasmi kuwa, Pep Guardiola, atachukua mikoba ya kuiongoza klabu yao kuanzia msimu ujao wa ligi ya soka nchini humo maarufu kama Bundesliga, pamoja na michuano mbalimbali ambayo watakuwa wakishiriki.


Kocha huyo wa zamani wa Barcelona, alikuwa akisemekana pia kutakiwa na vilabu vya Uingereza vya Manchester City, Chelsea na hata United, ambao ilielezwa kuwa walikuwa wakiangalia uwezekano wa yeye kuchukua nafasi ya mkongwe SAF, ambaye inajulikana kuwa ataachia ngazi kwa mashetani hao wakati wowote.
Kocha huyo ambaye alikuwa kwenye mapumziko marefu baada ya kuachia ngazi Barcelona, alikonyakua vikombe 14, atachukua mikoba hiyo toka kwa kocha wa sasa wa Bayern, Jupp Heynckes, ambaye atakuwa anastaafu baada ya msimu huu kumalizika.
“Tunayo furaha kubwa sana kuwa tumeweza kumshaweishi mtaalamu huyu wa soka kujiunga nasi, katika wakati huu ambapo alikuwa pia akitupiwa macho na vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya” amenukuliwa mtendaji mkuu wa Bayern Karl-Heins Rummenigge akitamka.
“Yeye ni miongoni mwa makocha walio katika daraja la juu kimafanikio, na tuna imani kuwa sio tu kuwa atakuwa na manufaa makubwa kwa Bayern Munich pekee, bali pia kwa soka la Ujerumani kwa ujumla” ameongeza mtendaji huyo.
Miamba hao ambao kwa sasa wako pointi tisa nyuma ya vinara wa Bundesliga kwa sasa, wanatarajiwa kuumana na Arsenal katika mechi ya Ligi ya Mabingwa baadae mwaka huu, na kocha wa sasa tayari alishawaeleza viongozi wake kuwa asingeongeza mkataba wake utakapofikia mwisho wa msimu.(JUKWAA HURU)

MRADI WA MABASI DAR WAIVA-KUTOA AJIRA 80,000


BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia (WB), imeidhinisha Dola za Marekani 100 milioni kwa ajili ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (BRT) jijini Dar es Salaam.


Taarifa ya benki hiyo iliyopatikana Dar es Salaam jana imeeleza kuwa mradi huo utakaozalisha ajira 80,000 kwa Watanzania, utasaidia abiria 300,000.

“Ajira hizo 80,000 zitapatikana hadi mwaka 2015 na zitatokana na kazi zinazotarajiwa kuwapo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, vituo vya abiria, vituo vidogo na vituo vya kuratibu barabara hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier alisema kiasi hicho cha fedha kimelenga kukamilisha awamu ya pili ya mradi huo.

Dongier ambaye pia ni msimamizi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Uganda na Burundi, alisema mradi huo utagharimu jumla ya Dola za Marekani 290 milioni.

“Dar es Salaam inakuwa kwa kasi, msongamano wa magari ni tatizo kwa ukuaji wa uchumi kwa sababu unapunguza uzalishaji kwa kupoteza muda wa watumiaji wa barabara. Hali hiyo inatishia ukuaji wa baadaye wa mji na nchi kwa jumla na unaongeza uharibifu wa mazingira,” ilisema taarifa ya WB na kuongeza:

“Mfumo wa BRT utasimamiwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa Dola za Marekani 40.9 milioni ukihusisha wasimamizi binafsi wawili wa mabasi na mkusanya nauli mmoja. Mfumo huo mpya utatekelezwa kwa mabasi yapatayo 148 yatakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 140 kila moja kwa safari za haraka na za kawaida.

“Mabasi mengine 100 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja yatatembea katika barabara ndogo. Kutakuwa na kilometa 20.9 zitakazokuwa na njia za waendesha baiskeli na wapita kwa miguu kila upande na vituo vya mabasi kwa kila umbali wa wastani wa mita 500.”

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema hana taarifa za benki hiyo kuidhinisha fedha hizo, lakini akasema atafuatilia ili kujua idadi ya ajira, hasa zitakazowanufaisha wazawa.

“Kwa kweli hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia kwako, labda unipe muda nizifuatilie ili nije na majibu ya uhakika. Lakini kama kawaida, ajira za kampuni kama hizo huwa na wataalamu wa nje na wa ndani, kwa hiyo tutahakikisha kuwa sheria zinalindwa,” alisema Kabaka.

Mtaalamu wa usafiri katika Benki ya Dunia, Yonas Mchomvu alisema: “Tunafurahishwa na kasi ya utekelezwaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi, hasa kwa kuwa makandarasi wote wanaotakiwa wameshapewa fedha na ujenzi unaendelea,” alisema Mchomvu.

Daladala wachekelea
Licha ya taarifa hiyo kueleza kuwa mradi huo utasababisha kuondolewa kwenye mzunguko daladala 1,800, bado wamiliki wa magari hayo wamepokea mradi huo kwa furaha.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema hiyo ni fursa kubwa kwao ambayo hawako tayari kuikosa.

“Siyo kwamba mradi huo utatuathiri na siyo daladala 1,800 tu zitakazoondolewa, ni daladala 3,000. Sisi ndiyo walengwa wa mafanikio hayo kwani hayo mabasi yanayokwenda haraka tutamilikishwa. Hapa ndipo tunahimizana kujiunga ili tujue tutayamiliki vipi,” alisema Mabrouk.BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia (WB), imeidhinisha Dola za Marekani 100 milioni kwa ajili ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (BRT) jijini Dar es Salaam.


Taarifa ya benki hiyo iliyopatikana Dar es Salaam jana imeeleza kuwa mradi huo utakaozalisha ajira 80,000 kwa Watanzania, utasaidia abiria 300,000.

“Ajira hizo 80,000 zitapatikana hadi mwaka 2015 na zitatokana na kazi zinazotarajiwa kuwapo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, vituo vya abiria, vituo vidogo na vituo vya kuratibu barabara hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier alisema kiasi hicho cha fedha kimelenga kukamilisha awamu ya pili ya mradi huo.

Dongier ambaye pia ni msimamizi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Uganda na Burundi, alisema mradi huo utagharimu jumla ya Dola za Marekani 290 milioni.

“Dar es Salaam inakuwa kwa kasi, msongamano wa magari ni tatizo kwa ukuaji wa uchumi kwa sababu unapunguza uzalishaji kwa kupoteza muda wa watumiaji wa barabara. Hali hiyo inatishia ukuaji wa baadaye wa mji na nchi kwa jumla na unaongeza uharibifu wa mazingira,” ilisema taarifa ya WB na kuongeza:

“Mfumo wa BRT utasimamiwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa Dola za Marekani 40.9 milioni ukihusisha wasimamizi binafsi wawili wa mabasi na mkusanya nauli mmoja. Mfumo huo mpya utatekelezwa kwa mabasi yapatayo 148 yatakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 140 kila moja kwa safari za haraka na za kawaida.

“Mabasi mengine 100 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja yatatembea katika barabara ndogo. Kutakuwa na kilometa 20.9 zitakazokuwa na njia za waendesha baiskeli na wapita kwa miguu kila upande na vituo vya mabasi kwa kila umbali wa wastani wa mita 500.”


Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema hana taarifa za benki hiyo kuidhinisha fedha hizo, lakini akasema atafuatilia ili kujua idadi ya ajira, hasa zitakazowanufaisha wazawa.

“Kwa kweli hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia kwako, labda unipe muda nizifuatilie ili nije na majibu ya uhakika. Lakini kama kawaida, ajira za kampuni kama hizo huwa na wataalamu wa nje na wa ndani, kwa hiyo tutahakikisha kuwa sheria zinalindwa,” alisema Kabaka.

Mtaalamu wa usafiri katika Benki ya Dunia, Yonas Mchomvu alisema: “Tunafurahishwa na kasi ya utekelezwaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi, hasa kwa kuwa makandarasi wote wanaotakiwa wameshapewa fedha na ujenzi unaendelea,” alisema Mchomvu.

Daladala wachekelea
Licha ya taarifa hiyo kueleza kuwa mradi huo utasababisha kuondolewa kwenye mzunguko daladala 1,800, bado wamiliki wa magari hayo wamepokea mradi huo kwa furaha.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema hiyo ni fursa kubwa kwao ambayo hawako tayari kuikosa.

“Siyo kwamba mradi huo utatuathiri na siyo daladala 1,800 tu zitakazoondolewa, ni daladala 3,000. Sisi ndiyo walengwa wa mafanikio hayo kwani hayo mabasi yanayokwenda haraka tutamilikishwa. Hapa ndipo tunahimizana kujiunga ili tujue tutayamiliki vipi,” alisema Mabrouk.

Friday, January 11, 2013

TAIFA STARS KUPAMBANA NA ETHIOPIA LEO

    
  
ADDIS ABABA-ETHIOPIA,  Mechi ya kirafiki ya kimataifa baina ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) na wenyeji Ethiopia itapigwa kuanzia saa 11:30 jioni, taarifa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ilisema jana.

Stars itashuka dimbani leo ikiwa na lengo la kujiongezea heshima kwa kuendeleza kichapo dhidi ya wenyeji ambao wamefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2013) zitakazoanza Janauri 19 nchini Afrika Kusini; ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kupata ushindi usiotarajiwa wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia "Chipolopolo" katika mechi yao nyingine ya kirafiki iliyochezwa Desemba 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Addis Ababa uliopo katika mji huo mkuu wa Ethiopia.

"Mechi itachezwa kesho (leo) Addis Ababa Stadium kuanzia saa 11.30 jioni (Tanzania na Ethiopia hatupishani saa)," taarifa hiyo ilisema.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa timu iliwasili salama na kufikia katika hoteli ya Hilton na kwamba ilitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa kwa saa moja jana kuanzia saa 11.30 jioni.

Katika mechi yao iliyopita dhidi ya Zambia, goli pekee la Stars lililofungwa na Mrisho Ngassa lilitosha kuwashangaza nyota wakubwa wa Chipolopolo, akiwamo nahodha Christopher Katongo ambaye alikuwa ndiyo kwanza ametokea kushinda tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika 2012.

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na Ethiopia kutaka kupima nafasi yao kuelekea kwenye fainali za Mataifa ya Afrika huku Stars ikiitumia kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi 22.
Tanzania yenye pointi tatu inashika nafasi ya pili katika Kundi C la kuwania kufuzu kwa safari ya Brazil nyuma ya vinara Ivory Coast wenye pointi nne baada ya mechi mbili. Morocco ni ya tatu ikiwa na pointi mbili wakati Gambia inashika mkia ikiwa na pointi 1. Timu moja tu katika kila kundi (makundi 10) ndiyo inayosonga mbele kwa hatua inayofuata ya mechi za mtoano. Timu tano zitaenda Brazil.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema baada ya mechi hiyo, Stars inatarajia kucheza mechi nyingine angalau moja ya kimataifa kabla ya kuwavaa Morocco.

Wachezaji waliopo katika kambi ya Stars kwa ajili ya mechi ya leo ni pamoja na nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam FC), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), na Shomari Kapombe (Simba).

Wengine ni Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu  (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ) na Mrisho Ngasa (Simba)
.

TANGA KUGAWANYWA NA KUWA MIKOA MIWILI.


 
TANGA-TANZANIA, Kamati ya ushauri mkoa wa Tanga RCC imepitisha pendekezo la kuugawa mkoa wa Tanga na kuwa mikoa miwili na kuiagiza sekretarieti ya mkoa kulifanyia kazi pendekekezo hilo.
Katika pendendekezo hilo lililotolewa na Afisa Mwandamizi wa serikali za mitaa Yohana Paul mkoa wa Tanga utabaki na wilaya za Tanga, Muheza, Mkinga na Pangani
Aidha mkoa mpya utakuwa na wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto na Korogwe.
Bwana Paul amebainisha kuwa lengo hasa la kuugawa mkoa huo ni kusogeza huduma karibu kwa wananchi kutokana jiografia ya mkoa wa Tanga ulivyo.
Ambapo baadhi ya wananchi wanaoishi mbali na makao makuu ya mijini na wilaya hawanufaiki na huduma za kijamii zinazotolewa na serikali.(CHANZO:FREE AFRICA)

Wednesday, January 9, 2013

baadhi ya Wajumbe wa Umoja wa Mataifa waunga mkono kutumika kwa ndege za upelelelezi Congo.



Waasi wa M23 wanaohatarisha usalama wa Mashariki mwa Congo

DRC CONGO,
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,UN wameunga mkono pendekezo la kuanza kutumika kwa Ndege maalum za upelelezi mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC ili kulinda usalama wa Raia.

 Mkuu wa Operesheni za Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous amesema kuwa amewasilisha ombi maalumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha mpango wa kutumika kwa ndege maalumu zenye uwezo wa kuona hata wakati wa usiku kwenye maeneo ya Mashariki na Mpakani mwa DRC na Rwanda.
 
Pendekezo hilo limepingwa vikali na nchi ya Rwanda, huku baadhi ya Mataifa yakionesha wasiwasi wao iwapo ndege hizo zitaidhinishwa kutumika kuongezea nguvu vikosi vya MONUSCO katika kuimarisha usalama nchini humo.

Iwapo Baraza la Usalama litaidhinisha mpango huo itakuwa ni maraya kwanza kwa UN kupitisha mpango kama huo nchini DRC mpango utakaosaidia pia kukabiliana na Waasi.(CHANZO:RFI)

UJERUMANI YATUMA WANAJESHI NA MAKOMBORA UTURUKI








Wanajeshi wa Ujerumani wakiiandaa mitambo ya kuzuia makombora, maarufu kama Patriot.

BERLIN-UJERUMANI,
Jeshi la Ujerumani hapo jana (08.01.2013) limetuma wanajeshi wa kwanza nchini Uturuki, kama sehemu ya makubaliano ya Jumuiya ya Kujimhami NATO, kuilinda nchi hiyo dhidi ya makombora kutoka Syria.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere. 
Wanajeshi hao karibu 40 wameungana na wenzao kutoka Uholanzi, nchi nyingine inayomiliki mitambo ya Patriot, inayotumika kuzuia makombora. Mitambo ya Patriot ya Ujerumani pia inasafirishwa leo kuelekea nchini Uturuki.
  
  
Serikali ya Ujerumani imekuwa ikisisitiza mara kwa mara: kwamba kupelekwa kwa wanajeshi wake katika mpaka wa Uturuki na Syria si kwa nia ya kushiriki mapambano. Imesema wanajeshi hao hawatajihusisha na mgogoro unaoendelea nchini Syria, na hili ndio jambo ambalo waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere amelipa umuhimu katika ufafanuzi wa mpango huu. "Harakati hizi ni makhsusi kwa ulinzi na hatua za tahadhari katika eneo la NATO, na hapa kwa ajili ya kulinda mipaka ya Uturuki," amesema waziri De Maziere.
Uturuki  ikiwa ni mwanachama wa NATO  iliwaomba washirika wake kuisadia na sasa ombi hilo limejibiwa. Wanajeshi wa kwanza  wa Ujerumani wanawasili nchini humo na watafanya kazi na wanajeshi wa Uholanzi kuandaa eneo itakapowekwa mitambo hiyo ya Patriot. Mitambo ya Ujerumani inasafirishwa leo kwa njia ya bahari kutoka bandari ya Travemünde kuelekea nchini Uturuki. Awamu nyingine ya wanajeshi wa Ujerumani yenye jumla ya wanajeshi 350 watapelekwa nchini Uturki wiki ijayo.
Dhamira hii ni ishara muhimu ya mshikamano na Uturuki, amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle na kuongeza kuwa: "Tusisahau kuwa kuna mauaji yamefanyika nchinin Uturuki kutokana na mashambulizi kutoka Syria. Hili ndiyo hasa linaloipa wasi wasi Uturuki, kwa sababu hakuna anayejua utawala wa Syria bado unaweza kufanya nini."Katika  kuilinda Uturuki, mitambo hiyo ya Patriot inaweza kuzuia mashambulizi ya roketi, makombora ya masafa marefu na hata kuyadungua baadhi yake. Lakini mitambo hiyo haiwezi kuzuia kitisho kikubwa kama vile mashambulizi ya mizinga. Kwa hivyo hatua hii inapaswa kueleweka kuwa ni ya kiishara zaidi, na kazi yake hasa ni kuzuia, amesema waziri wa ulinzi Thomas de Maziere.
Uwezo wa mitambo ya Patriot
Ujerumani itaiweka mitambo yake katika eneo la Kahramanmaras, karibu kilomita 100 kutoka mpaka wa Syria. Hii ndiyo operesheni ya kwanza ya kweli kwa mitambo ya patriot kutumika baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Bunge la Ujerumani lilipiga kura kwa wingi katikati ya mwezi Disemba kuruhusu kupelekwa kwa mitambo hiyo, na imeruhusiwa kukaa huko hadi mwezi Februari mwaka 2014.Gharama za operesheni hiyo kwa serikali ya Ujerumani zinakadiriwa kuwa euro milioni 25. (CHANZO:DW)




MEMBE NA BASHE NGOMA NZITO CCM


DAR ES SALAAM -TANZANIA,
MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.
Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.

Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.

“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.

Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania.

“Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi.
Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.

Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo.
“Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.
Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”

Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.

Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”

Mgororo ulikoanzia
Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.(CHANZO:MWANANCHI).

Tuesday, January 8, 2013

POLISI MBARONI KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI


KAGERA-TANZANIA,
ASKARI Polisi wawili katika Mkoa wa Kagera, wamekamatwa wakiwa na meno ya tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara ambapo pia wanatuhumiwa kwa mauaji ya faru George aliyepokewa na Rais Jakaya Kikwete katika mbuga ya Serengeti.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(Tanapa), Allan Kijazi akizungumza na gazeti hili alisema askari hao walikamatwa juzi jioni na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kushirikiana na polisi wa Kituo cha Mugumu.
Alisema askari hao walifanikiwa kuwakamata askari wenzao wakati wakipeleleza matukio ya wizi wa nyara za Serikali na kuwakuta na vipande vya meno ya tembo ambavyo vikiunganishwa yanatimia meno mazima sita.
Alisema watuhumiwa hao wa ujangili walikuwa wakisafirisha meno hayo kutoka Kijiji cha Bunchugu wilayani Serengeti kwenda Mugumu mjini kwa kutumia pikipiki mbili.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na mzigo katika pikipiki, waliwapeleka askari hao kwa matajiri waliokuwa wakipelekewa mzigo huo katika Hoteli ya Galaxy ambao walikutwa na gari ndogo ambalo pia limekamatwa.
Alisema baada ya kuhojiwa waligundulika kuwa ni askari Polisi mwenye cheo cha Koplo na Konstebo kutoka Biharamulo mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Kijazi, baada ya kufanya mawasiliano na Mkuu wa Polisi katika eneo walikotoka, alikiri kuwa ni askari wake huku akishangazwa kusikia wamekutwa katika eneo la Serengeti mkoani Mara.
“Huu mtandao ni mkubwa na sasa imebainika hata yule faru George aliyepokewa na Rais Kikwete ndio walihusika kumuua na kuchukua nyara zake…hii ni hatari kwa wenzetu polisi kushiriki katika hujuma kwa taifa lao,” alidai Kijazi.
Alisema baada ya mahojiano yanayofanyika Kituo Kikuu cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti, taarifa kamili ya watuhumiwa hao itatolewa.
“Tunaomba ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha tunalinda rasilimali zetu kwani bila ushirikiano kamwe hatuwezi kufanikiwa,” alisema Kijazi.
IGP Mwema akiri
Mkuu wa Polisi nchini IGP, Said Mwema, amethibitisha kukamatwa kwa askari hao huku akisema hatua hiyo imetokana na ushirikiano mzuri kati ya polisi na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Mwema alisema ingawa kitendo hicho kimelifedhehesha Jeshi la Polisi lakini kamwe halitakata tamaa kwa kuwaondoa kazini askari wake wanaokwenda kinyume na maadili.
“Polisi tumekuwa na ushirikiano mzuri na wenzetu wa Tanapa hata kukamatwa kwa askari hawa wawili kumetokana na ushirikiano uliopo kati ya polisi Mugumu na watumishi wa Hifadhi ya Serengeti,”alisema IGP Mwema kwa njia ya simu.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Tanapa imekuwa ikipambana na ujangili katika maeneo mbalimbali nchini na haitarudi nyuma kwa utovu wa nidhamu ambao umeoneshwa na askari hao.
“Ndani ya jeshi tuna programu ya kutoa zawadi kwa kila askari wanaofanya vizuri katika kupambana na uhalifu pia kwa wale wanaokwenda kinyume tumekuwa tukiwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.
“Mpango wa kutii sheria bila shuruti pia unawalenga askari hivyo nakuhakikishia kuwa lazima tutalisafisha Jeshi letu la Polisi na kama kuna askari anajijua hawezi kwenda na kasi hii ya sasa, ni vema ajiondoe mwenyewe,” alisema IGP Mwema.
Aliomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kupambana na uhalifu katika maeneo yao na ujangili katika hifadhi za taifa.