Tuesday, January 8, 2013

POLISI MBARONI KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI


KAGERA-TANZANIA,
ASKARI Polisi wawili katika Mkoa wa Kagera, wamekamatwa wakiwa na meno ya tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara ambapo pia wanatuhumiwa kwa mauaji ya faru George aliyepokewa na Rais Jakaya Kikwete katika mbuga ya Serengeti.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(Tanapa), Allan Kijazi akizungumza na gazeti hili alisema askari hao walikamatwa juzi jioni na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kushirikiana na polisi wa Kituo cha Mugumu.
Alisema askari hao walifanikiwa kuwakamata askari wenzao wakati wakipeleleza matukio ya wizi wa nyara za Serikali na kuwakuta na vipande vya meno ya tembo ambavyo vikiunganishwa yanatimia meno mazima sita.
Alisema watuhumiwa hao wa ujangili walikuwa wakisafirisha meno hayo kutoka Kijiji cha Bunchugu wilayani Serengeti kwenda Mugumu mjini kwa kutumia pikipiki mbili.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na mzigo katika pikipiki, waliwapeleka askari hao kwa matajiri waliokuwa wakipelekewa mzigo huo katika Hoteli ya Galaxy ambao walikutwa na gari ndogo ambalo pia limekamatwa.
Alisema baada ya kuhojiwa waligundulika kuwa ni askari Polisi mwenye cheo cha Koplo na Konstebo kutoka Biharamulo mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Kijazi, baada ya kufanya mawasiliano na Mkuu wa Polisi katika eneo walikotoka, alikiri kuwa ni askari wake huku akishangazwa kusikia wamekutwa katika eneo la Serengeti mkoani Mara.
“Huu mtandao ni mkubwa na sasa imebainika hata yule faru George aliyepokewa na Rais Kikwete ndio walihusika kumuua na kuchukua nyara zake…hii ni hatari kwa wenzetu polisi kushiriki katika hujuma kwa taifa lao,” alidai Kijazi.
Alisema baada ya mahojiano yanayofanyika Kituo Kikuu cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti, taarifa kamili ya watuhumiwa hao itatolewa.
“Tunaomba ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha tunalinda rasilimali zetu kwani bila ushirikiano kamwe hatuwezi kufanikiwa,” alisema Kijazi.
IGP Mwema akiri
Mkuu wa Polisi nchini IGP, Said Mwema, amethibitisha kukamatwa kwa askari hao huku akisema hatua hiyo imetokana na ushirikiano mzuri kati ya polisi na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Mwema alisema ingawa kitendo hicho kimelifedhehesha Jeshi la Polisi lakini kamwe halitakata tamaa kwa kuwaondoa kazini askari wake wanaokwenda kinyume na maadili.
“Polisi tumekuwa na ushirikiano mzuri na wenzetu wa Tanapa hata kukamatwa kwa askari hawa wawili kumetokana na ushirikiano uliopo kati ya polisi Mugumu na watumishi wa Hifadhi ya Serengeti,”alisema IGP Mwema kwa njia ya simu.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Tanapa imekuwa ikipambana na ujangili katika maeneo mbalimbali nchini na haitarudi nyuma kwa utovu wa nidhamu ambao umeoneshwa na askari hao.
“Ndani ya jeshi tuna programu ya kutoa zawadi kwa kila askari wanaofanya vizuri katika kupambana na uhalifu pia kwa wale wanaokwenda kinyume tumekuwa tukiwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.
“Mpango wa kutii sheria bila shuruti pia unawalenga askari hivyo nakuhakikishia kuwa lazima tutalisafisha Jeshi letu la Polisi na kama kuna askari anajijua hawezi kwenda na kasi hii ya sasa, ni vema ajiondoe mwenyewe,” alisema IGP Mwema.
Aliomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kupambana na uhalifu katika maeneo yao na ujangili katika hifadhi za taifa.

No comments:

Post a Comment