Tuesday, January 8, 2013

VIJANA CHADEMA WAFUKUZANA.




DAR ES SALAAM-TANZANIA, BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha), limesema limemvua uanachama Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo, Juliana Shonza baada ya kubainika alikuwa akifanya vikao vya siri kukisaliti chama hicho akishirikiana na viongozi wa CCM.

Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema Shonza alikuwa akiwashawishi wenzake kuitisha mikutano na waaandishi wa habari kumkashifu Katibu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa.
“Aende CCM hapa tumemg’oa kwa sababu alikuwa kirusi hatari kwa chama, alikuwa Chadema huku akifanya kazi na CCM, tuna ushahidi wa picha, mikanda ya video na ujumbe wa simu za mikononi,” alisema Heche.

Licha ya kumfuta uanachama Shonza, baraza hilo pia limewavua uanachama Habib Machange aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini na Mtela Mwampamba aliyegombea ubunge Jimbo la Mbozi Mashariki.

Heche alisema makamu wake amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya baraza, chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko.

“ Pia, amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM, akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni ili kuikashifu Chadema na viongozi wake wakuu,” alisema Heche.

Kuhusu Mchange, Heche alisema huyo amevuliwa uanachama kwa kutoa tuhuma za uongo ikiwamo mauji, kinyume na maadili ya wanachama na kuunda vikundi vinavyojulikana kama masalia na PM7-Pindua Mbowe.

Alisema Mchange alituhumiwa na kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na kuwatukana viongozi kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha siasa cha Chauma.
Kwa upande wa Mwampamba, alisema alikuwa akitoa tuhuma nzito za uongo hadharani ikiwamo za mauaji.

Alisema mwanachama huyo kama alivyo mwenzake alishiriki vikao vya kuanzisha chama cha siasa cha Chaumma akiwa Chadema.

Naye Ben Saanane, Heche alisema huyo alipewa onyo kali baada ya kukiri kujiunga na vikundi vya masalia na PM7 na kwamba, amepewa miezi 12 ya uangalizi ili ajirekebishe.
Kipindi kama hicho kimetolewa kwa Gwakisha Mwakasendo anayedaiwa kutenda makosa ya kushiriki vikao na vikundi hivyo na kwamba, alikiri kosa na kupewa onyo kali. Pia, atakuwa kwenye uangalizi kwa miezi 12.

No comments:

Post a Comment