Wednesday, January 23, 2013

BARAZA LA USALAMA LAONGEZA VIKWAZO KWA KOREA KASKAZINI

PYONG YANG-KOREA KASKAZINI,
Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa UN limeagiza kuwekwa kwa vikwazo zaidi dhidi ya Serikali ya Korea Kaskazini kufuatia nchi hiyo kuendelea kukaidi maazimio ya baraza hilo kuhusu kurusha maroketi wanayodai ni ya kisayansi.
Kwenye vikwazo hivyo vipya baraza hilo limeiongeza mamlaka ya anga ya nchi hiyo, benki, makampuni ya biashara na watu wanne ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali ya Pyongyang katika kutekeleza mpango wake wa kutengeneza roketi za masafa marefu.

Mapendekezo hayo ambayo yaliwasilishwa na nchi ya Marekani, yalipitishwa bila kupingwa na nchi wanachama 15 wa kudumu wa baraza hilo na kulaani kile ambacho imekiita ni ukaidi wa taifa hilo.

Mwezi Desemba mwaka jana nchi ya Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya kombora lake la masafa marefu kuelekea angani, jaribi ambalo yenyewe imesisitiza halihusiani na utengenezaji wa silaha za masafa marefu kama inavyodaiwa na nchi za magharibi.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo Suzan Rice amelitaka baraza hilo kuchukua hatua zaidi iwapo nchi ya Korea Kaskazini itaendelea kukaidi maazimio ya Umoja huo.

Nchi za Marekani na China zimekuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali ya Pyongyang katika kujaribu kuishawishi nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kutengeneza makombora ya masafa marefu.

Licha ya vikwazo hivyo Serikali ya Pyongyang imeapa kuendelea na majaribio yake na kwamba hivi karibuni itateeleza jaribio jingine la roketi.

No comments:

Post a Comment