Thursday, January 17, 2013

PEP GUARDIOLA ATUA BAYERN MUNICH

_65329389_guardiola_empics2

BAYERN MUNICH-UJERUMANI,
Miamba ya soka nchini Ujerumani, klabu ya Bayern Munich, imetangaza rasmi kuwa, Pep Guardiola, atachukua mikoba ya kuiongoza klabu yao kuanzia msimu ujao wa ligi ya soka nchini humo maarufu kama Bundesliga, pamoja na michuano mbalimbali ambayo watakuwa wakishiriki.


Kocha huyo wa zamani wa Barcelona, alikuwa akisemekana pia kutakiwa na vilabu vya Uingereza vya Manchester City, Chelsea na hata United, ambao ilielezwa kuwa walikuwa wakiangalia uwezekano wa yeye kuchukua nafasi ya mkongwe SAF, ambaye inajulikana kuwa ataachia ngazi kwa mashetani hao wakati wowote.
Kocha huyo ambaye alikuwa kwenye mapumziko marefu baada ya kuachia ngazi Barcelona, alikonyakua vikombe 14, atachukua mikoba hiyo toka kwa kocha wa sasa wa Bayern, Jupp Heynckes, ambaye atakuwa anastaafu baada ya msimu huu kumalizika.
“Tunayo furaha kubwa sana kuwa tumeweza kumshaweishi mtaalamu huyu wa soka kujiunga nasi, katika wakati huu ambapo alikuwa pia akitupiwa macho na vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya” amenukuliwa mtendaji mkuu wa Bayern Karl-Heins Rummenigge akitamka.
“Yeye ni miongoni mwa makocha walio katika daraja la juu kimafanikio, na tuna imani kuwa sio tu kuwa atakuwa na manufaa makubwa kwa Bayern Munich pekee, bali pia kwa soka la Ujerumani kwa ujumla” ameongeza mtendaji huyo.
Miamba hao ambao kwa sasa wako pointi tisa nyuma ya vinara wa Bundesliga kwa sasa, wanatarajiwa kuumana na Arsenal katika mechi ya Ligi ya Mabingwa baadae mwaka huu, na kocha wa sasa tayari alishawaeleza viongozi wake kuwa asingeongeza mkataba wake utakapofikia mwisho wa msimu.(JUKWAA HURU)

No comments:

Post a Comment