Friday, March 9, 2012

MGOMO WA MADAKTARI MOTO! - Pinda ahairisha Ziara Mwanza.

  Mmoja wa wagonjwa Bi. Fatuma Rashid akiondoka eneo la hospitali ya 
Temeke baada ya kukosa Huduma (Picha kwa hisani ya IPP Media)






Dar es Salaam, Mgomo wa madaktari ulioanza kwa kasi ndogo hapo juzi umeanza kushika kasi baada ya hapo jana idadi ya Hospitali zilizoripotiwa kuwa na mgomo huo kuongezeka kutoka zile za awali za Bugando na Amana mpaka Muhimbili, Temeke na Hospitali nyingine za Rufaa Mikoani huku Hospitali ya Muhimbili  hapo jana ikitangaza rasmi kuifunga Kliniki yake ya Wagonjwa wa nje kutokana na Uchache wa madaktari , hali hiyo imedaiwa kumlazimu Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda Kuhairisha ziara yake ya siku kumi mkoani Mwanza ili kushughulikia tatizo la hilo mara moja. Kwa Mujibu wa Vyanzo vya ndani Waziri mkuu amehairisha ziara yake hiyo hadi hapo itakapotangazwa tena.

Idadi ndogo ya wagonjwa Imeripotiwa katika Hospitali za Serikali kutokana na mgomo huo ambapo katika baadhi ya Hospitali ikiwemo Muhimbili wagonjwa waliolazwa wameondolewa na ndugu na jamaa zao kwenda kwenye hospitali binafsi na Wengine nyumbani, mmoja wa ndugu aliyetambulika kwa jina  Marwa Chacha  alisema ameamua kumuhamisha mama yake mzazi kutoka Muhimbili kwenda Hospitali ya Regency kutokana na kuzorota kwa huduma katika hospitali hiyo, nae Filbert Tarimo aliyekuja Muhimbili kutoka Morogoro kwa matibabu ya Moyo aliambiwa arudi nyumbani mpaka atakapopewa taarifa tena.
  Huko Mwanza katika Hospitali ya Rufaa ya bugando madaktari hapo jana waliendelea na Mgomo wao kwa siku ya pili na kusababisha usumbufu mkubwa kwa Wagonjwa, huku mmoja wa Madaktari wa Hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake akisema madaktari hao pia wamegomea Kikao kilichoitishwa na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo hapo jana mchana.
. “Leo tuliitwa kwenye kikao na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini tulikubaliana tusifike kwenye kikao hicho hivyo hatutakwenda,” alieleza mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kuandikwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa sasa sio wakati wa kuandikana majina kwenye vyombo vya habari.  Huduma katika hospitali hiyo jana zilianza kuzorota kwani licha ya baadhi ya madaktari wa kidini ambao sio waajiriwa wa Wizara ya afya kutogoma hali ilikuwa mbaya kutokana na  kuzidiwa kwa madaktari hao.

Iringa - katika hospitali ya rufaa ya Iringa kumeripotiwa pia  kuwepo kwa mgomo ambapo licha ya madaktari  kuwepo katika mazingira ya hospitali hiyo hawakutoa huduma yoyote kwa wagonjwa waliofika kupata huduma hiyo, Wakati Mkoani Tanga katika Hospitali ya Bombo hali kama hiyo pia ikiripotiwa.

Chama cha wafanyakazi TUGHE kupitia kwa katibu wake kimesema mgomo huo ni matokeo ya kutoaminiana kati ya serikali na Madaktari hao huku akiitaka serikali kushughulikia suala hilo kama chombo cha umma, akisisitiza Umuhimu wa pande zote mbili kukaa na kufikia makubaliano tena ili kunusuru maisha ya watanzania.
Wananchi wengi waliotoa maoni wamepeleka lawama zao kwa Serikali na madaktari hao huku wengine wakitaka kuwajibishwa au kuwajibika kwa mawaziri hao.

Hadi hapo jana serikali ilikuwa kimya na hakuna tamko rasmi tangu lile la Waziri Mkuu kabla ya kuanza kwa mgomo huo na wananchi wengi wanasubiri kwa hamu kujua hatua gani serikali itaichukua kunusura hali zao.

No comments:

Post a Comment