ARUSHA-TANZANIA,Kushikiliwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kumeendelea kuibua sokomoko baina ya polisi kwa upande mmoja na wafuasi wa Chadema na familia yake kwa upande mwingine.
\Lema aliyekamatwa usiku wa manane kuamkia Ijumaa wiki hii, alihojiwa kwa saa tatu mfululizo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Arusha lakini alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba kuachiwa kwake kungehatarisha amani.
Akizungumza na gazeti hili kabla ya kujisalimisha kwa askari hao usiku huo wa kuamkia juzi, Lema alithibitisha kuwapo kwa polisi nje ya nyumba yake:
“Wapo nje ya nyumba yangu, wanatishia kupiga mabomu kama nisipotoka nje, lakini wanajadiliana na walinzi wangu na mimi nimewataka wanipe hati ya kunikamata,”alisema.
Wakili wa Lema, Humphrey Mtui alisema mahojiano ya mteja wake na polisi yalidumu kwa zaidi ya saa tatu kuanzia saa 7:50 mchana hadi saa 11:15 jioni, na kwamba walitaka ufafanuzi kwenye hoja tatu walizodai kwamba zilijengwa kwenye kauli alizotoa Lema wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA).
Maneno hayo yanayotafsiriwa na polisi kuwa ni uchochezi ni pamoja na “Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni woga” na “Nimepata taarifa kuwa ndani ya dakika 15 Mkuu wa Mkoa atafika, asipofika ndani ya muda huo nitawaongoza kwenda kudai haki yenu ya msingi ya kupatiwa ulinzi.”
Kauli nyingine ni “Hawa ndio viongozi wetu (akimaanisha mkuu wa mkoa), tunaowategemea wanakuja kwenye matatizo wakijivuta utafikiri wanakwenda kwenye send-off.”()
Lema anadaiwa kutamka maneno hayo baada ya Mulongo kugoma kuzungumza na wanafunzi kisha kurejea ndani ya gari akitaka viwepo vipaza sauti, kitendo kilichowafanya wanafunzi kuanza kumzomea kabla polisi kuanza kulipua mabomu ya machozi na kumwondoa eneo la tukio mkuu huyo wa mkoa.
Lema na Mulongo wote walikwenda IAA kutokana na tukio la kuuawa kwa kuchomwa kisu kwa aliyekuwa mwanafunzi wa taasisi hiyo, Henry Kago.
Baada ya vurugu hizo Mulungo alimtuhumu Lema kuandaa mazingira ya yeye kuzomewa .
Wakati hayo yakiendelea, askari katika kituo anakoshikiliwa Lema jana asubuhi walivutana vikali na ndugu wa mbunge huyo pamoja na uongozi wa Chadema Mkoa wa Arusha baada ya kumpa dakika moja kunywa chai aliyoletewa na kukataa asipewe dawa ya meno kutoka kwa mkewe, Neema.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata zinasema kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chadema ulilazimika kumtuma wakili wa Lema, Method Kimomogoro kwenda Kituo cha Kati cha Polisi Arusha kujua sababu za polisi kufanya hivyo. (MWANANCHI)