Friday, April 12, 2013

RAIS OMAR AL BASHIR KUZURU SUDAN KUSINI LEO.


JUBA-SUDAN KUSINI,Rais wa Sudan Omar Hassan Al Bashir anatarajiwa kuzuru nchini Sudan Kusini ijumaa hii na tayari maandalizi makubwa kwa ajili ya mapokezi yake yamekwishafanyika. Al Bashir anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Rais Salva Kiir na ziara hii itakuwa ni sehemu ya kumaliza mgogoro uliozuka baina ya pande hizo mbili.

Miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele katika mazungumzo ya viongozi hao ni suala la usalama ambalo limekuwa tete tangu nchi hizo zigawanyike mwezi Julai mwaka 2011.Muafaka kati ya viongozi hawa wawili unatajwa kuwa huenda ukawa chanzo cha kupunguza uhasama na hata kurahisisha utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya mataifa hayo.

Mpango wa Al Bashir kuzuru Juba uliwekwa wazi siku moja tu baada ya viongozi wa mataifa haya mawili ya Sudan kuafikiana kuanza upya biashara ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta.

Ziara ya Bashir mjini Juba itakuwa ni ya kwanza tangu kiongozi huyo alipohudhuria sherehe za uhuru julai 9 2011 kufuatia kura ya maoni iliyoamua Kusini ijitegemee baada ya miaka 22 ya machafuko.

No comments:

Post a Comment