Tuesday, May 14, 2013

MAGUFULI AWASILISHA BAJETI YA TRILIONI 1.226 BUNGENI

DODOMA-TANZANIA,
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, jana aliwasilisha bajeti yake iliyosheheni utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwamo barabara, madaraja na nyumba za Serikali. Dk. Magufuli aliliomba Bunge kuidhinisha Sh trilioni 1.226 kwa ajili ya wizara yake, kwa mwaka ambapo kati ya hizo Sh bilioni 845 ni kwa ajili ya maendeleo na Sh bilioni 381 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Alisema katika bajeti yake, Serikali imetenga Sh bilioni 314 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu na za mikoa, huku Sh bilioni 21 zikitengwa kwa ajili ya ujenzi wa madaraja.

Bajeti hiyo ambayo imegusa kila pembe ya nchi katika ujenzi wa barabara na madaraja, pia imelenga kupunguza tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Katika bajeti hiyo, Serikali imetenga Sh bilioni 4.4 kwa ajili ya ununuzi wa kivuko kipya kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo ambacho kitasaidia kupunguza tatizo la usafiri.

Fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya kununulia boti ya uokoaji pamoja na mashine za kisasa za kukatia tiketi kwa ajili ya kivuko cha Magogoni.

Alisema Sh bilioni 20.5 zimetengwa kwa ajili ya upanuzi wa Barabara mpya ya Bagamoyo kutoka makutano ya Barabara ya Kawawa na Ali Hassan Mwinyi hadi Tegeta kilomita 17.

“Lengo la mradi huu ni kupanua barabara hii kuanzia eneo la Morocco hadi Tegeta kutoka njia mbili hadi njia nne, ili kupunguza msongamano wa magari wa magari katika barabara hiyo,” alisema Dk. Magufuli.

Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka (DART) kutoka Kimara hadi Kivukoni, Fire hadi Kariakoo na Magomeni hadi Morocco.

Kuhusu Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, alisema katika mwaka huu wa fedha, bodi hiyo ilipanga kusajili wakandarasi 807 na kutathimini wakandarasi wengine 587.

Kuhusu ujenzi wa barabara, alisema Sh bilioni 314 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu na za mikoa ambazo zitajengwa kupitia mfuko wa barabara.

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuainisha idadi ya madeni katika sekta ya barabara kuweza kufahamu uhalisia wa bajeti hiyo.

Akisoma maoni hayo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Juma Kapuya, alisema ni muhimu wabunge kufahamu iwapo fedha zilizoombwa zinakwenda kujenga barabara au kulipa madeni.

“Kamati ilipata taarifa kuwa hadi Aprili 8, mwaka huu wizara ilikuwa ikidaiwa zaidi ya shilingi bilioni 348 kwa ajili ya fidia kwa wananchi, wakandarasi na wakandarasi washauri.

No comments:

Post a Comment