Sunday, April 6, 2014

UCHAGUZI CHALINZE KUMEKUCHA

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/04/vituo_1-300x169.jpg 

UCHAGUZI mdogo wa ubunge Chalinze, Bagamoyo, mkoani Pwani unaofanyika leo ambapo jumla ya vituo 288 vya kupigia kura vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vitatumika tena.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi huo jana, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Samuel Salianga, alisema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 na vifaa muhimu vimesambazwa kwenye vituo hivyo.
Alivitaja vyama vitano vinavyoshiriki uchaguzi huo kuwa ni CCM, CHADEMA, CUF, NRA na AFP huku akibainisha idadi ya wapiga kura kuwa ni 92,939.
Kwa upande mwingine Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Chalinze kuhakikisha vinawatumia mawakala wanaotoka eneo la vituo ili wawatambue wapiga kura wa eneo hilo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema sheria haikatazi vyama hivyo kuteua mawakala kutoka majimbo mengine ya uchaguzi lakini ni vema kuwateua wale wanaotoka eneo lenye wapiga kura wanaowafahamu.
Licha ya kuwepo kwa idadi hiyo ya waliojiandikisha katika daftari la kupiga kura lakini kuna wasiwasi wa wapiga kura kutofikia idadi hiyo kutokana na miundombinu ya baadhi ya maeneo kuharibiwa na mvua zinazonyesha mkoani hapa.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunatokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Said Bwanamdogo, ambaye alifariki dunia Januari 22, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment