WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likikutana kesho kwa ajili ya kupokea taarifa za kamati na kuanza mjadala wa jumla kwa wajumbe wote, Rais Jakaya Kikwete ameridhia ombi la kulisitisha kuanzia Aprili 28 hadi Agosti mwaka huu, ili kupisha Bunge la Bajeti liendelee na vikao vyake.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo Februari 18, mwaka huu, wajumbe wameweza kujadili sura mbili pekee za rasimu ya katiba ambazo hata hivyo uamuzi wake utategemea majadiliano yatayofanyika baada ya kamati zote kuwasilisha taarifa zao kuanzia kesho.
Bunge hili limetumia takribani wiki tatu kujadili kanuni zake, na hivyo kupunguza muda wake wa siku 70 uliowekwa kisheria bila kuanza kujadili sura na ibara za rasimu hiyo.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kukutana na viongozi wawili wakuu wa dini, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama
Sitta alisema kuwa juzi alipokutana na Rais Kikwete alimueleza umuhimu wa kuongeza muda kwa Bunge hilo ambapo alionyesha nia ya kulisogeza hadi Agosti mwaka huu.
Alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kumalizia kuipitia sura ya kwanza na ya sita ya rasimu inayozungumzia muundo wa serikali ambapo kesho wenyeviti wa kamati 12 za Bunge hilo watawasilisha taarifa zao kwa mtiririko bila majadiliano.
“Wakishawasilisha tunatarajia wiki ijayo wajumbe wote kupata fursa ya kuchangia kwa uwiano, lakini niseme kuwa sina hakika kama kwa muda uliosalia tutakuwa tumemaliza maana sheria namba 83 ya mabadiliko ya katiba inasema ni siku 70 tu, hivyo itakuwa ni aibu rasimu ipitiwe sura mbili pekee kati ya sura 17 zilizopo,” alisema.
Alieleza kuwa baada ya Bunge la Katiba kuahirishwa, litaanza Bunge la Jamhuri kwa ajili ya bajeti hadi Juni, na Julai wataitumia kwa kuwapa wabunge nafasi ya kutembelea majimbo yao ili Agosti Bunge la Katiba liweze kurejea tena kuendelea kupitia sura nyingine.
Sitta alifafanua kuwa baada ya Bunge Maalumu kuhitimisha kazi yao, watakabidhi kwa Rais Kikwete na mwenzake wa Zanzibar rasimu ya katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kuiwasilisha kwa wananchi waweze kuipigia kura ya ama kuikubali au kuikataa.
“Unajua licha ya kuwepo purukushani nyingi za hapa na pale nia ya wabunge wengi ni kupata katiba bora na nzuri hivyo mchakato utakamilika tu,” alisema.
Akizungumzia sababu ya kuwatembelea viongozi hao, Sitta alisema kuwa katiba inamgusa kila raia na ndiyo sababu kama mwenyekiti wa Bunge Maalumu aliamua kukutana nao ili kuwafahamisha wametoka wapi, wako wapi na nini kinaendelea.
Sitta aliongeza kuwa kwa kutambua nafasi ya viongozi hao katika jamii hasa kwa kuongoza kundi kubwa la Watanzania, amekutana nao ili kuwasihi na kuelimisha wananchi wengi wanaowaongoza ikiwemo kuliombea Bunge hilo litoke salama.
Sitta atia shaka
Katika hatua nyingine, ziara ya Sitta kwa viongozi wakuu wawili wa dini imeacha maswali mengi ambapo baadhi ya watu wameitafsiri kama kampeni ya Chama Cha Mapinduzi kutafuta uungwaji mkono katika kutetea mfumo wake wa muundo wa serikali mbili.
Hatua hiyo inatokana na msimamo wa viongozi hao wawili kuwa sambamba na ule wa CCM katika suala la muundo wa Muungano ambapo wote wanataka serikali mbili.
Vyanzo vyetu vya ndani vimedokeza kuwa kwa muda mrefu CCM ilikuwa ikitafuta namna ya kupenyeza karata yake ili kupata uungwaji mkono wa Kanisa Katoliki ambalo lina wafuasi wengi nchini.
Hivi karibuni, Kardinali Pengo alilazimika kukutana na vyombo vya habari ili kuweka sawa taarifa iliyokuwa imetolewa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo kupitia kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka akitaka mapendekezo ya wananchi kwenye rasimu kuhusu serikali tatu yaheshimiwe.
Alisema maoni hayo ni yake binafsi wala si msimamo wa kanisa hilo huku akiweka bayana kuwa yeye ni muumini wa serikali mbili, lakini pia akasisitiza kwamba hayo ni maoni yake.
No comments:
Post a Comment