Walipishana jimboni Ohio Jumapili, ambalo ndilo linalosemakana kuwa muhimu zaidi miongoni mwa majimbo saba yenye maamuzi katika uchaguzi wa Marekani. Juu ya hilo, Obama alizitembelea New Hampshire, Florida na Colorado siku hiyo ya Jumapili, wakati Romney alizitembelea Iowa, Virginia na Pennslyvania. Msisitizo wa Obama katika kipindi hiki ni kwa wapiga kura kuchagua kati ya dira mbili. "Huu siyo tu uchaguzi kati ya wagombea wawili au vyama viwili, ni uchaguzi kati ya dira mbili tofatu za Marekani," alisema Obama.
Rais Barack Obama akitambulishwa na rais wa zamani Bill Clinton katika mkutano wa kampeni mjini Concord, New Hampshire. Hoja za mwisho za Obama jimboni Ohio zilijikita katika uokozi wa kampuni za magari za Chrysler na General Motors mwaka 2009, ambao Romney aliupinga akiwa gavana wa jimbo la Massachusets wakati huo na kisema sekta ya magari ilipaswa kuachwa ifilisike. Matamshi hayo yamekuja kumuathiri, hasa katika jimbo lenye viwanda vingi la Ohio.
Katika mkutano siku ya Ijumaa mjini Springfield, Ohio, Obama aliwaambia wafuasi wake waliyozomea alipotaja jina la Romney, kwamba kupiga ndiyo kisasi bora zaidi. Romney alitumia mkutano wake mjini Cleveland kumshambulia Obama kuhusiana na kauli yake hiyo, na kusema badala yake, yeye anawaomba wapiga kura wachague kwa mapenzi ya nchi yao. Romney alisema mabadiliko aliyoahidi Obama yameshindikana
"Mabadiliko hayawezi kupimwa kupitia hotuba, mabadiliko yanapimwa kupitia mafanikio, na miaka minne iliyopita mgombea Obama aliahidi mambo mengi kwa watu wengi lakini ametimiza kidogo sana," alisema Romney.
Wapambe wapishana kushawishi wapiga kura
Makundi yanayojitolea kwa ajili ya wagombea yalikuwa yanapishana katika majimbo yenye maamuzi, wakiwasiliana na wafuasi wao kuhakikisha kuwa watapiga kura na kujitolea kuwasafirisha kwenda kwenye vituo vya kupigia kura. Wakati Romney akiwasihi wafuasi wake waende kwa wingi katika vituo vya kupigia kura siku ya jumanne, Obama anaelekeza juhudi zaidi katika majimbo yenye maamuzi.
Maoni yamekuwa yakiwaonyesha wawili hao wakikaribiana kwa sana lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Obama bado ana nafasi ya kushinda. Edward Wycof William, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema maoni yamekuwa yakibadilika kutoka wiki moja hadi nyingine, lakini kilichoonekana ni kwamba Romney hajaongoza kabisaa katika maoni yoyote katika majimbo muhimu.
Mitt Romney akiweka sahihi yake katika fulana ya mfuasi wake mjini Des Moines, Iowa Novemba 4. Obama akumbushia hali ngumu aliyoikuta mwaka 2008
Obama anatafuta awamu ya pili huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa asilimia 7.2. Hakuna rais aliyefanikiwa kupata muhula wa pili tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia kukiwa na kiwango cha ukosefun wa ajira kilicho juu ya asilimia 7.2. Uchumi bado unakua kwa chini ya asilimia 2, lakini Obama amewakumbusha wapiga kura juu ya mazingira ya mgogoro alimochaguliwa miaka minne iliyopita.
"Kumbukeni mwaka 2008 tulikuwa katikati ya mgogoro mbaya zaidi tangu mdororo mkubwa wa uchumi. Tulikuwa katikati ya vita viwili. Na sasa biashara zetu zimetengeneza ajira karibu milioni 5.5, viwanda vya magari vinafanya vizuri na sekta ya nyumba inaanza kurejesha thamani yake, tunategemea mafuta kutoka nje kwa kiasi kidogo kuliko wakati wowote katika kipindi cha miaka 20," alime Obama na kuongeza kuwa vita vya Iraq vimekwisha, vile vya Afghanistan vinakaribia mwisho na Osamba bin Laden aliuawa.
Wanajeshi wa Marekani wakiushusha shehena ya msaada kwa ajili ya waathirika wa kimbunga Sandy. Marekani inakwenda kwenye uchaguzi wakati eneo la kaskazini mashariki likikabiliana na madhara ya moja ya tufani kubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo. Takriban watu milion 27 wamekwisha piga kura katika uchaguzi wa mapema. Zaidi ya milioni 130 walipiga kura mwaka 2008. Wapiga wanatarajiwa kuamua hatma ya viti vyote 435 vya Bunge la wawakilishi ambalo linatarajiwa kuendelea kudhibitiwa na chama cha Republicans, na theluthi moja ya viti vya bunge la Seneti lenye viti 100, ambako chama cha Democrats kinatarajiwa kuedeleza udhibiti mdogo. Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika wakati sehemu ya kaskazini mashariki inakabiliana na madhara ya kimbunga cha Sandy kilichoharibu maelfu ya makaazi na kuua watu zaidi ya 100.
Waendesha kura za maoni wamtabiria ushindi Obama
Obama anaendelea kuwa na faida dhidi ya Romney katika majimbo yenye maamuzi, ambayo ndiyo yanaamua mshindi wa urais. Ili kushinda kiti hicho, mgombea laazima kura 270 za majimbo. Obama anahitaji kujihakikishia kura 243 za majimbo yanayoegemea chama cha Democrats, wakati Romney anaweza kujihakikishia kura 206, na hii inamuongezea shinikizo la kutafuta zaidi kura za majimbo yenye maamuzi.
Tayari mawakili wa kambi zote wanajianda kwa mpanbano mrefu wa mahakani katika majimbo yenye ushindani mkubwa. Baadi ya wataalamu wanatarajia vuta nikuvute kama zile za mwaka 2000, zilizochukua wiki tano kumpa ushindi George W. Bush. Tayari mvutano umeripotiwa jimboni Florida, baada ya wapiga kura wanaodhaniwa kuwa wa Democrats kuzuiwa na gavana wa jimo hilo ambaye ni wa chama cha Republican.
Obama na timu yake wakifuatilia mauaji ya Osama bin Laden. mauaji hayo yamekuwa moja ya hoja zake za kutaka muhula wa pili. Maoni yaliyochapishwa na gazeti la Wall Street Journal siku ya Jumapili yalimpa Obama asilimia moja zaidi ya Romney kitaifa akiwa na asilimia 48 dhidi ya 47 za Romney. Tovuti ya Real Clear Politics ilimpa Obama uongozi wa asilimia 0.2. Karibu waendesha kura za maoni wote wamemtabiria ushindi Obama katika kura za majimbo. Talking Point Memo imempa Obama kura 303 dhidi ya 191 za Romney, Fivethirtyeight.com imempa Obama kura 307 dhidi ya 231 za Romney na Pricneton Election Consortium ilimpa Obama kura 277 dhidi ya 206 za Romney(Chanzo DW)