Wednesday, July 10, 2013

MATOKEO YA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO KUTOLEWA LEO

DAR ES SALAAM, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema majina  ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu,  yatatangazwa leo.

Msemaji wa wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema jana kuwa, majina hayo yatatangazwa leo shughuli itakayofanyika katika ofisi za wizara hiyo.

 “Kesho (leo) saa nne, selected (waliochaguliwa) watatangazwa,” alisema Ntambi.

Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema majina ya wanafunzi hao yatatangazwa siku yoyote ndani ya juma hili.

Mulugo jana alisema majina hayo hayajachelewa kutangazwa na kwamba wanafunzi wa kidato cha sita hufungua wiki ya tatu ya Julai na kwamba hata sasa bado hawajafungua.

“Matokeo tutayatoa wiki hii na  hatujachelewa kuyatangaza kwa sababu  kwa kawaida kidato cha tano na sita wanafungua shule wiki ya tatu Julai , kwa hiyo tukitoa wiki hii tutakuwa hatujachelewa,” alisema Mulugo.

Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti.

“Mpaka sasa hatujaambiwa kwa nini hii hali imekuwa hivi, kwa kawaida kidato cha tano huripoti shuleni wiki moja kabla ya kidato cha sita, lakini mpaka sasa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano bado hawajatangazwa,” alisema Mwalimu huyo.

Wakati majina hayo yakitarajiwa kutangazwa leo, ni dhahiri kuwa shule za Serikali zenye kidato cha tano na sita zitaendelea kupata idadi ndogo ya wanafunzi tofauti na uwezo huku baadhi zisizo za Serikali zikitishia kuachana na biashara ya shule.

Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa mtihani wa kidato cha nne, ambapo kwa mwaka 2012 waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 35,349. Wwanafunzi walio katika nafasi kubwa ya kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni wale waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.(MWANANCHI)


No comments:

Post a Comment