Saturday, July 6, 2013

Papa John Paul II kutangazwa Mtakatifu.

http://media.tumblr.com/tumblr_lk598yBV7a1qaf7km.jpg 

VATICAN, Papa Francis amethibitisha uamuzi wa kumtangaza kuwa mtakatifu mwenyeheri Yohane Paul ll ambaye alifariki dunia mwaka 2005.

Katika uamuzi wake jana, Papa Francis ameeleza kuwa miujiza mbalimbali na ushahidi wa matendo ya mwenyeheri Yohane Paul II yanampa nafasi ya kumtangaza mtakatifu kulingana na kanuni za Kanisa Katoliki.

Uamuzi huo wa kumtangaza mtakatifu Yohane Paul ll utamfanya Papa Francis kumweka katika orodha ya watakatifu kiongozi huyo ambaye aliongoza kanisa hilo tangu mwaka 1978 pamoja na Papa mwingine, Yohane XXlll, ambaye alifariki dunia miaka 50 iliyopita na ambaye alikuwa kipenzi cha wengi.

Kwa mamlaka yake, Papa Francis atamtangaza pia Papa Yohane XXlll kuwa mtakatifu, ingawa makao ya kanisa hilo, Vatican hayathibitishi rasmi muujiza wake.

Vatican ilieleza jana kuwa Papa Francis anao uwezo na mamlaka ya kumtangaza mtu yeyote kuwa mtakatifu kufuatana na mchakato ambao umewekwa na kanisa hilo na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, bila kuangalia au kuegemea zaidi kigezo cha muujiza.

Hata hivyo, Vatican inaeleza kuwa sherehe za kumtangaza mwenyeheri Papa Yohane Paul ll kuwa mtakatifu zitafanyika kabla ya mwisho wa mwaka.

Tayari, Desemba 8 imeandaliwa rasmi kama siku maalumu ya kufanyika kwa shughuli hiyo, kutokana na kuwa sikukuu kubwa ya kanisa hilo kwa kumbukumbu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, siku ambayo pia watawa hasa wa kike huweka nadhiri zao.

Vyombo vya habari vya Poland alikozaliwa mwenyeheri Papa Yohane Paul ll vimeendelea kueleza kuwa Oktoba ndiyo unaoweza kutumika kwa shughuli hiyo, siku ambayo ni ukumbusho wa kuteuliwa kwake kuwa kiongozi wa kanisa hilo mwaka 1978.

Hata hivyo, maofisa wa Vatican wameeleza kuwa itakuwa mapema mnno kwa shughuli hiyo kubwa kwa kanisa hilo.

Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi alithibitisha kuwa muujiza wa kwanza wa mwenyeheri Papa Yohan Paul ll ulihusisha mwanamke raia wa Costa Rica.

Gazeti la Kikatoliki la Hispania, La Razon limemtaja mwanamke huyo kuwa Floribeth Mora na kueleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya ugonjwa wa kichwa, ambao ulipona kwa maajabu Mei Mosi, 2011 , siku ambayo tukio la kutangazwa kwa Yohane Paul ll kuwa mwenyeheri kulifanyika mbele ya waumini 1.5 milioni katika Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa heshima yake.

Katika matoleo kadhaa ya gazeti hilo mwezi uliopita, La Razon limeeleza kuwa Mora aliamka akiumwa kichwa Aprili 8 na kwenda hospitali, hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kurudishwa nyumbani na kuambiwa kuwa ataishi kwa mwezi mmoja.(MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment