Wednesday, July 10, 2013

WATUHUMIWA WA BOKO HARAM WAFUNGWA MAISHA

Wanachama wanne wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Kiislamu la Boko Haram, wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mashambulio ya bomu yaliyosababisha vifo vya watu kumi na tisa.

Wanne hao walipatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza mashambulio ya mabomu katika ofisi za tume ya uchaguzi na kanisa moja mwaka uliopita.

Hukumu hiyo ndiyo kali zaidi kuwahi kutolelwa kwa mwanachama au mshukiwa yeyote wa kundi hilo la Boko Haram.

Kundi hilo limehusika na mashambulio kadhaa ambayo yamesababisha maafa mengi katika maeneo ya Kaskkazini na Kati nchini Nigeria.

Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limekuwa likiwalenga raia wa kawaida na zaidi ya watu elfu mbili wameuawa tangu kundi hilo la Boko Haram kuanzisha uasi mwaka wa 2009, katika juhudi zake za kutaka kuundwa kwa taifa jipya la Kiislamu katika eneo lililo na idadi kubwa ya Waislamu Kaskazini mwa Nigeria.

Hali ya ulinzi Kaskazini mwa Nigeria;

Hali ya hatari, ilitangazwa tarehe kumi na nne mwezi Mei mwaka huu, katika majimbo ya Kaskazini Mashariki ya Adamawa, Borno na Yobe, hatua iliyoishurutisha serikali ya nchi hiyo kutuma zaidi ya wanajeshi elfu mbili kushika doria katika eneo hilo na pia kuvunja kambi za wanamgambo hao.

No comments:

Post a Comment