Thursday, January 16, 2014

Ndugai, DC kikaangoni, CUF wapigilia msumari






Dar es Salaam. Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Ardhi (HakiArdhi), imekosoa hatua ya Naibu Spika, Job Ndugai kuingilia mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Kiteto na kusema kuwa ni mwendelezo wa uchochezi wa wanasiasa katika migogoro hiyo.
Akiwa kwenye mazishi ya Mchungaji Emanuel Manyaji (38) na mwanaye Shukuru Manyaji (13) ambao waliuawa na wafugaji kwa kuchinjwa wakiwa kanisani katika eneo la Hifadhi ya Embroy Murtangos wilayani Kiteto, Ndugai alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Martha Umbura kujiuzulu kutokana na madai kuwa hana sifa za kuendelea na wadhifa huo.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa HakiArdhi, Yefred Myenzi alisema, kauli hiyo ni mwendelezo wa malumbano ya wanasiasa yanayochochea migogoro kwa wananchi.
“Nimemsikia naibu spika akisema kuwa viongozi wa wilaya ndiyo wanahusika, je anao ushahidi? Kwa nini kauli kama hizi zitoke nje ya Wilaya ya Kiteto? Inaonyesha kuna wanasiasa wanaohamasisha wananchi wavamie ardhi iliyozuiwa kutumika.”
Kauli ya Ndugai imekuja wakati kukiwa na madai kuwa anamiliki mashamba katika eneo hilo la mgogoro.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu,Ndugai alikanusha kuwa na shamba wilayani humo na kuendelea kusisitiza kuwa, lazima mkuu wa wilaya awajibike kwa kuwa wananchi wa jimbo la Kongwa wana haki ya kuishi mahali popote nchini.
“Kwani kuwa na shamba ni kosa?... kwa kifupi mimi sina shamba Kiteto wala Kongwa kwa sababu mimi silimi. Haya ni mauaji mabaya mno. Mimi kama naibu spika siyo msemaji sana, hata bungeni sichangii hoja, ila kwa hili sitaacha kusema,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, mwananchi aamke salama na afanye kazi, sasa ikitokea mauaji, mauaji mauaji, unafikiri nini kifanyike? …
“Si Kiteto tu, wananchi wa Kongwa wako Mtwara, Dodoma,Kilimanjaro na popote pale Tanzania wanatafuta maisha,” alisisitiza.
Akifafanua chanzo cha mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Kiteto, Myenzi alisema ni hatua ya halmashauri hiyo kutaka kuwahamisha wakulima katika eneo ambalo wamekuwa wakilitumia kwa kilimo huku ikidaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi ijulikanayo kama Emboroy Murtangos.
“Mgogoro huu ulifikishwa katika vyombo vya sheria ambapo wakulima walishinda… mwaka 2007 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Hata hivyo halmashauri ya wilaya ilikata rufaa Mahakama ya Rufani na kushinda katika kesi namba 58 ya mwaka 2010. Hata hivyo wakulima wameomba mapitio ya kesi hiyo,” alisema Myenzi.
Licha ya mgogoro huo, Myenzi alitaja migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero na mgogoro wa mwekezaji na wananchi Mkoa wa Morogoro na mwingine wa mwekezaji na wananchi wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya.
1 |

No comments:

Post a Comment