Monday, September 24, 2012

KOREA KASKAZINI KUFANYA MAPINDUZI KATIKA KILIMO

http://www.csmonitor.com/var/ezflow_site/storage/images/media/content/2012/0725-north-korea-kim-jong-un/13252612-1-eng-US/0725-north-korea-kim-jong-un_full_600.jpg
Pyongyang-Korea Kaskazini,
Habari kutoka Korea kaskazini zinasema kuwa mageuzi ya kiuchumi yatakayoruhusu wakulima kuweka mazao yao na kushinikiza masoko huru, yanaidhinishwa .

lengo la hatua hiyo linaonekana kulenga kuongeza mazao katika nchi hiyo iliyo na uchumi unaoendeshwa na serikali na unaokumbwa na ukosefu mkubwa wa chakula.

Hakuna tangazo rasmi lililotolewa na wizara ya kilimo nchini humo lakini wachambuzi wanaiona kuwa ishara ya uwezekano wa mabadiliko ya mwelekeo chini ya kiongozi mkuu mpya Kim Jong-un ambaye tangu amerithi uongozi kutoka kwa baba yake amefanya baadhi ya mabadiliko ikiwemo kuwa na hotuba katika vyombo vya habari mara kwa mara na badiliko alilolifanya la kumbadilisha mkuu wa jeshi wa nchi hiyo aliyekuwa mzee na kumteua mkuu mpya ambaye n kijana.

Masoko huru yamekuweko kwa miaka kadhaa Korea kaskazini tangu kiongozi mwazilishi wa Korea kaskazini Bw.Kim Il Sung kuanzisha mfumo wa mashamba ya ushirika ambayo yaliwataka wakulima kutunza hifadhi ya chakula kinachobaki badala ya kukiuza.

Wednesday, September 19, 2012

URUSI YAIAMURU MAREKANI KUSIMAMISHA MISAADA INAYOIPA.

 

Moscow-Urusi,
Serikali ya Urusi imelipiga marufuku shirika la kutoa misaada la Marekani USAID nchini humo kwa kile ilichodai mbinu za shririka hilo kuvisaidia vikundi vinavyotaka kubadilisha tamaduni za kisiasa za ndani na kuathiri uchaguzi wa nchi hiyo.

waziri wa mabo ya nje wa Urusi amesema katika taarifa yake kuwa shirika hilo linajaribu kubadili siasa za Urusi, zikiwemo uchaguzi na vyama mbali mbali vya umma kwa kutoa misaada.

Uamuzi huo utakuwa ni pigo kubwa kwa Rais Obama ambaye anakabiliwa na uchaguzi mwezi Novemba mwaka huu na anafanya kila juhudi kurudisha uhusiano mzuri na moja ya maasimu wake hao wa zamani.

Kwa upande wake serikali ya Marekani kupitia kwa msemaji wa Ikulu bi.Victoria Nuland imesema uamuzi huo wa Urusi hautakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa nchi hizo ikisisitiza kuwa Marekani  itaendeleza juhudi zake za kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na maendeleo nchini Urusi.


Sunday, September 16, 2012

POLISI WAWASHAMBULIA TENA WACHIMBA MIGODI AFRIKA KUSINI



http://www.aljazeera.com/mritems/Images/2012/9/16/2012916113248805734_20.jpg
MARIKANA,AFRIKA KUSINI.
Polisi Afrika kusini wamewashambulia kwa risasi za mipira na mabomu ya machozi wanamigodi waliokuwa wakiandamana kudai ongezeko la mishahara na kupinga mashambulizi ya polisi dhidi yao hapo Jumamosi ya jana.

Maandamano hayo yalikuwa ya amani ambapo waandamanaji walibeba fimbo badala ya mapanga kama mwezi uliopita yalipotokea mauaji ya wanamgodi 45.Polisi wamesema wamevuruga maandamano hayo kwa sababu yalikosa kibali na leo wamewaomba wanamgodi hao kuachana na maandamano hayo pamoja na mikusanyiko yoyote isiyo halali.

Katika tukio hilo la jana polisi licha ya kusambaratisha maandamano hayo pia walipekua vyumba vya wanamgodi wa mgodi wa Marikana ambapo wanadai kukamata visu, mapanga,madawa ya kulevya na silaha nyingine za kijadi na kuwakamata watu 12 kwa kosa la kukutwa na silaha pamoja na madawa hayo.

Migomo katika mgodi huo imeendelea baada ya kushindwa kufikiwa kwa makubaliano kati ya wamiliki wa mgodi huo na wafanyakazi wanaodai kuongezwa kwa mishahara, hali iliyoyumbisha bei ya Platinum katika dunia na kuchochea migomo katika migodi mingine 6 nchini humo.

Friday, September 14, 2012

MAANDAMANO YA WAISLAMU KUPINGA FILAMU YA KIMAREKANI YAZIDI KUPANUKA




 
Sudan,Yemen na Tunisia,
Waandamanaji wa kiislamu wenye itikadi kali na waliochukizwa na filamu yenye kudhihaki dini ya kiislamu wamezingira na kushambulia balozi za Ujerumani,na Marekani mjini Khatoum nchini Sudan leo.

Waandamanaji hao wamevavamia Balozi za Ujerumani nchini humo na kuwasha moto pamoja na kuchana bendera ya Ujerumani kisha kupandisha bendera yenye nembo ya Kiislamu.Waandamanaji wengine wamekusanyika katika ubalozi wa Marekani baada ya swala ya Ijumaa ya leo ingawa vurugu hazijaripotiwa katika balozi hiyo.

Huko Yemen yametokea mapambano makali kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga filamu hiyo ambapo mtu mmoja ameripotiwa kufariki na wengine 15 kujeruhiwa.

Tunisia, katika mji mkuu wa Tunis waandamanaji wameupiga mawe ubalozi wa Marekani na kuwalazimu askari wa kutuliza ghasia nchini humo kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.


Filamu hiyo iliyotengenezwa nchini Marekani na kusambazwa katika mtandao imeamsha hasira na chuki za ulimwengu wa kiislamu dhidi ya Marekani huku serikali ya Marekani kupitia kwa waziri wake wa mambo ya nje Bi.Hilary Clinton ikikanusha kuhusika na filamu hiyo na kuilaani vikali kuwa ni yenye kuchukiza na kufedhehesha.

Saturday, September 8, 2012

USAFIRI WA RELI DAR KUANZA OKTOBA .

 
DAR ES SALAAM-TANZANIA,
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesema usafiri wa reli yenye urefu wa kilomita 197 jijini l Dar es Salaam utazinduliwa rasmi mwaka huu mwezi Oktoba hata kama baadhi ya miundo mbinu ya reli hizo haitakamilika.Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya reli Tanzania Bw.Mohamed Mohamed amesema sehemu kubwa ya ujenzi huo imekamilika ingawa bado kuna changamoto nyingi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kandarasi za ujenzi wa miundo mbinu hiyo ikiwemo sehemu za kukatisha tiketi, vuwekaji wa kokoto katika reli , vyoo na alama za tahadhari zimeshatolewa kwa makampuni mbalimbali.

 Mkurugenzi huyo alisema moja ya changamoto ni namna ya kuwaamisha watu waliopo ndani ya eneo linapotakiwa kupita mradi huo ambapo aliwataka watu wote waliopo ndani ya kilometa 15 kutoka eneo la Reli kuondoka.

Mradi huo wa relikwa sasa tayari  umeshaanza na ukarabati wa njia ya reli ya Stesheni ya Dar es Salaam hadi Ubungo Maziwa unaendenlea, njia ambayo treni itatumia takriban dakika 35 kutoka mwanzo hadi mwisho wa kituo hukuikisafirisha abiria 16,000 kwa siku.

Kwa reli ya Tazara  safari hiyo inatarajia kuhudumia abiria 20,000  kwa siku na kufanya jumla ya abiria kuwa 36,000.na hivyo kuwa msaada kwa Jiji hilo lenye wakazi zaidi ya milioni 4.

Friday, September 7, 2012

OBAMA AOMBA MUDA ZAIDI KWA WAMAREKANI-Ambeza Romney.


CHARLOTE,NORTH CAROLINA-MAREKANI ,
Hatimaye mgombea wa kiti cha urais nchini Marekani kupitia chama cha Democrats Rais Barack Obama amekubali uteuzi wake na kuwataka wamerakani kumpa muda zaidi wa kuboresha uchumi na maisha ya Wamarekani.
Akiongea katika mkutano mkuu wa chama cha Democrats Obama amesema amefanya mengi katika kipindi chake cha uongozi na Wamarekani wanatakiwa kuchagua kati ya nchi pamoja na uchumi au tuhuma kutoka kwa wapinzani wake.

Uchumi na Ajira:
Akiongelea uchumi rais huyo amesema siyo rais kumaliza matatizo ya uchumi yaliyoanza kwa miongo kadhaa kwa kipindi cha miaka michache,
"Siwezi kujifanya njia ninayoitoa ni ya haraka au rahisi"alisema Obama na kuongeza"Itachukua zaidi ya miaka michache kumaliza changamoto ambazo zimejengwa kwa miongo kadhaa"

 Rais huyo ameongelea umuhimu wa mpango wake wa kuitegemeza nchi katika nishati ya mafuta ili kufikia mwaka 2020 Marekani iweze kupunguza kiwango cha mafuta inayoyaingiza kutoka nje  kwa zaidi ya nusu,mpango ambao umepangwa kutengeneza ajira laki sita  katika viwanda vya gesi asilia akisema kuwa mpango huo utaongeza ajira.

Pia rais huyo ameongelea mpango wake wa kuongeza ajira katika viwanda vya uzalishaji zipatazo milioni 1, pamoja na ajira 100,000 za walimu wa hesabu na sayansi katika sekta ya Elimu.

Sera za kigeni:
Akiongelea sera za kigeni rais huyo amemshambulia mpinzani wake Romney kwa kupinga sera zake akisema yeye si mzoefu katika sera hizo na yeye(Obama) ameonesha uimara katika sera hizo akigusia pia kauli ya Romney kuwa Urusi ni adui namba moja wa Marekani, ambapo amesema huwezi kuwaita Urusi ni maadui namba moja wa Marekani badala ya Al Qaida isipokuwa ukiwa na mawazo mgando ya vita baridi, Pia rais huyo amehofia ukweli wa Romney kuboresha uhusiano na China ilhali kauli zake zimemwingiza katika mvutano na marafiki wao wakubwa Uingereza akirejea kauli za Romney wakati wa ufunguzi wa Olimpiki.

 Usalama wa nchi:
Obama alisema ametimiza sehemu kubwa ya ahadi zake za mwaka 2008 katika usalama wa nchi ambapo aliahidi kumaliza vita nchini Iraq na amefanya hivyo, pia kuongeza mapambano na kuidhohofisha Taleban huko Afghanistan,Pia amesema Alqaida imedhoofishwa na inaendelea kudhoofishwa na kiongozi wake Osama ameuawa.

 Obama amesema hatotumia fedha za nchi hiyo kununua na kutengeneza silaha bali kuboresha maisha ya Wamarekani kwa kujenga shule zaidi na kutoa huduma nyingine za kijamii.

Pia rais huyo amesema alitoa ahadi ya kuendelea kuwathamini zaidi askari wastaafu walioitumikia Marekani kwa vipindi mbalimbali.

Mazingira:
Rais Obama pia ameongelea suala la utunzaji wa Mazingira akisema mpango wake wa gesi asilia utasaidia kulinda mazingira na kuiepusha Marekani na majanga ya kimazingira.

Mgombea huyo alikuwa akifunga mkutano wa Chama cha Democrats kuelekea uchaguzi mkuu wa Marekani ambapo atapambana na Mitty Romney wa Chama cha Republican hapo Novemba 6 mwaka huu.
Mkutano huo umeelezewa na wengi kumpa nguvu mpya mgombea huyo ingawa bado ushindani ni mkubwa kuelekea uchaguzi huo kwa huku changamoto ya ukuaji wa ajira ambazo zinapanda na kushuka bado ni kikwazo na haijatoa mwelekeo kamili juu ya imani ya wapiga kura kwa rais huyo.

Thursday, September 6, 2012

BILL CLINTON AMBEBA OBAMA.



NORTH CAROLINA-MAREKANI,
Rais mstaafu wa Marekani Bw.Bill Clinton amewaambia wamarekani na dunia nzima kuwa anamwamini rais Obama kwa 'moyo wake wote' katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii hasa baada ya alichokifanya katika miaka yake minne ya uongozi na anastahili kuchaguliwa tena.

Rais huyo mstaafu alikuwa akizungumza katika mkutano wa chama cha Democratic katika uwanja wa Time Warner Cable Arena. huko North Carolina.
Clinton amesema hakuna rais ambaye angeweza kuhimili kuurekebisha uchumi mbovu alioukuta rais Obama kama alivyouokoa rais huyo,
"hakuna rais ambaye angeweza kuurekebisha uchumi na madhara yake siyo mimi au walionitangulia" alisema Clinton.

 Clinton amesema Obama amejenga misingi ya uchumi imara na wa kisasa kwa ustawi wa Marekani akiongeza kuwa hata watu wasipomwamini anachokisema yeye wajue kuwa anamwamini rais huyo kwa moyo wake wote.

Chama hicho cha Democrat kipo katika mkutano wake kuelekea uchaguzi ambapo hotuba hiyo ya Clinton inaonekana kumuinua rais Obama hasa kutokana na kukubalika kwa Rais huyo mstaafu ambaye alikuwa na rekodi nzuri ya uchumi enzi za utawala wake na ambaye ni moja ya watu maarufu na wanopendwa zaidi nchini Marekani.

Wednesday, September 5, 2012

DK.MARY NAGU AENGULIWA KINYANG'ANYIRO CHA UJUMBE NEC

 
KILIMANJARO-TANZANIA,
Harakati za uchaguzi ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang'.

kwa mujibu wa taarifa kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na kanuni inayowataka wanachama wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea nafasi hiyo.

Imeelezwa kuwa licha ya baadhi ya wajumbe kujaribu kumtetea Dk Nagu bado hali ilikuwa ngumu baada ya wajumbe wengine wliozidi idadi kupinga suala hilo.
“Kikao kilikuwa kizito, lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na uwezo wa wagombea hasa katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alinukuliwa mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Mjumbe huyo aliongeza kuwa mapendekezo ya kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa uamuzi zaidi na baadaye yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.

Huko Lindi mke wa Rais mama Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini huku akiwa hana mpinzani na hivyo kuwa na nafasi ya kupita moja kwa moja katika nafasi hiyo.

Saturday, September 1, 2012

WAASI WATEKA NA KUHARIBU VITUO VYA NDEGE ZA JESHI SYRIA

 

SYRIA,
Waasi wameteka kituo kimpja cha jeshi la anga la Syria na kuharibu vituo vingine viwili mashariki mwa Syria asubuhi ya leo. Mashambulizi hayo yamekuwa ni ya kulipiza mashambulizi ya majeshi ya serikali ambayo kwa sasa yameongeza masahambulizi ya anga dhidi ya waasi hao.

Kwa mujibu wa mashuhuda Waasi hao wameteka kituo cha ndege za kijeshi na kuwakamata mateka 6 na vifaa vya kijeshi katika jimbo la Deir al- Zor karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uturuki huku pia wakishambulia na kuaribu vituo vingine viwili vya Hamdan na Albu Kamal mashariki mwa Syria karibu na mpaka wa nchi hiyo na Iraq.

Katika taarifa nyingine imedaiwa kuwa waasi hao wameitungua na kuiangusha helkopta ya kijeshi pamoja na ndege aina ya Jet Fighter zote za jeshi la serikali.

Waasi wameendeleza mashambulizi dhidi ya majeshi ya serikali ambayo yameongeza kasi ya kuwashambulia kwa ndege baada ya kupata upinzani mkubwa katika mapigano ya ardhini.

Rais Al Assad amekuwa katika upinzani mgumu kutoka kwa wananchi na sasa waasi kwa takribani miezi 17 ambapo watu zaidi ya 20,000 wameuawa.