Wednesday, February 12, 2014

Adhabu kwa vigogo CCM-Wapo Lowassa,Makamba,Wassira,Sumaye.

Dodoma. Vigogo sita ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaanza kuhojiwa leo, huku wakikabiliwa na adhabu kadhaa ikiwamo ya kufungiwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa watapatikana na hatia ya makosa yanayowakabili.
Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho, inaanza kikao chake mjini Dodoma, chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula kuwahoji makada hao ambao ni wale wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuteka kikao hicho ni vitendo vinavyotokana na vita ya urais wa 2015, ambapo kumekuwa na matukio ya makada wa CCM kurushiana maneno hadharani na wengine kutuhumiwa kwa matumizi ya fedha.
Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM zinaruhusu wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kutangaza nia zao, lakini zinakataza kampeni kabla ya muda uliowekwa rasmi ambao ni baada ya wagombea wa nafasi husika kupitishwa na vikao vya chama hicho.
Vigogo hao ambao tayari walishapewa barua za kuitwa mbele ya kamati hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Kwa mujibu wa kanuni husika viongozi hao wanaweza kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungiwa kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi sita, 12 au 18, ikiwa watapatikana na hatia katika tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa, Kamati Ndogo ya Maadili haina uwezo wa kutoa adhabu za moja kwa moja kwa watuhumiwa hao na badala yake inaweza kutoa mapendekezo ya adhabu kwa Kamati Kuu ya Maadili ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Kamati ya Mzee Mangula ina mamlaka ya kufuta mashtaka baada ya kumsikiliza mhusika na kupima ushahidi dhidi yake, pale ambapo itaona kwamba pengine mhusika anapaswa kuchukuliwa hatua basi inapeleka mapendekezo katika Kamati Kuu ya Maadili,”alisema Nnauye.

No comments:

Post a Comment