Tuesday, February 11, 2014

Vigogo sita CCM waitwa Kamati ya Maadili


Dar es Salaam. Vigogo sita ambao wanatajwa kuwa wanajiwinda kwa ajili ya kuwania urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, wameitwa mbele ya Kamati ya Ndogo ya Maadili ya chama hicho, kwa ajili ya kuhojiwa kwa tuhuma za kukiuka maadili.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana zinawataja vigogo hao kuwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
“Wote wamepelekewa barua za wito wa kufika mbele ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Mzee Mangula (Philip, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara), ambayo itakutana mjini Dodoma, Februari 14 (kesho kutwa) ,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam na kuongeza:
“Barua hizo zimesainiwa na Mzee Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) mwenyewe na tayari zimeanza kusambazwa leo (jana) mchana.”
Kamati hiyo ndogo ya maadili, inaundwa na Mangula, Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Maua Daftari na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye jana alithibitisha kuwapo kwa Kikao cha Kamati ya Maadili Februari 14 pamoja na kuitwa kwa baadhi ya wanachama kwa ajili ya kuhojiwa.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina yao wala idadi ya walioitwa... “Wewe fahamu tu kwamba kikao hicho kitafanyika tarehe hiyo uliyoitaja, lakini masuala ya majina na idadi ya walioitwa yatajulikana kwenye kikao, mimi sina kwa sasa,” alisema Nnauye.
Katika siku za karibuni kumekuwa na vita ya maneno baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kutangaza mapema kugombea urais kabla ya ruhusa rasmi ya chama.
Kauli za walioitwa
Jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya walioitwa na wengi wao walisema hawakuwa wamepokea barua za wito huo.
Sumaye kwa upande wake alisema: “Kwa sasa niko Mwanza na sijapata barua yoyote ya kuitwa katika kikao chochote cha chama.”

No comments:

Post a Comment