Thursday, February 6, 2014

SUMAYE KUGOMBEA URAIS? Ashindwa kukanusha, aipiga mkwara CCM.

sumaye 5afa9
MBIO za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kuibua mambo mapya, baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kudai atachukua uamuzi mgumu kama chama chake kitateua mgombea urais asiye na sifa.
Akizungumza Radio Tumaini, mjini Dar es Salaam jana asubuhi, Sumaye alisema kama CCM itafanya mambo ya ajabu kwa kuteua mgombea asiyekubalika wala kuwa na sifa za kiongozi mwadilifu, atafungua ukurasa mpya.
"Nitachukua uamuzi mgumu kama CCM watateua mgombea ambaye hana sifa ya kuwaongoza Watanzania, nitachukua uamuzi mgumu, haiwezekani tukaongozwa na watu wanaotoa fedha nyingi kila kukicha.
"CCM wakifanya mambo ya ajabu kwa kuchukua mtu ambaye ametoa fedha, nitatafuta njia nyingine," alisema.
Alisema hata siku moja hatakuwa na kinyongo kama atateuliwa mtu safi na mwenye moyo mweupe wa kusaidia Watanzania.
Alipoulizwa swali kama atagombea urais, alisema "Mimi sisemi kama nagombea, nakwambia muda ukifika nitasema tu, kwa wakati huu naomba tuendelee kutulia kwanza.
"Muda ukifika nitaamua nini cha kufanya, unajua unapotaka kuchukua uamuzi huu kuna mambo mazito ambayo unapaswa kuyatafakari kwa undani zaidi.
"Miongoni mwa mambo haya, ni kusaidia Watanzania kutoka walipo ili wapige hatua moja mbele zaidi, kuachana na tabia ya mtu mmoja kujitajirisha kupita kiasi," alisema Sumaye.
Alisema kama Watanzania wakimhitaji ili awasadie, atakuwa tayari kufanya hivyo.
"Muda ukiwadia na Watanzania wakisema wananihitaji, basi nami nitakuwa tayari kuwasaidia...jukumu hili linahitaji mtu mwenye busara sana," alisema Sumaye.
Alipoulizwa kuhusiana na hali ya CCM kwa sasa, alisema kuna tofauti kubwa katia ya CCM ya mwaka 1977 na ya sasa ambayo imekuwa ikikumbwa na matukio mengi.
Akitoa mfano, alisema: "Hivi sasa ukitaka kugombea lazima uwe na fedha, haya ni mambo machafu ambayo CCM yetu ya miaka ya 77 haikuwapo kabisa.
"Nalisema hili kutoka moyoni mwangu, nimekuwa mbunge na mjumbe wa NEC kwa miaka 20, sijawahi kutoa rushwa wala kupokea.
"Ukiona watu hao wanatoa rushwa, ujue moja, hawana uwezo wa kuongoza wananchi wao na ndani ya mioyo yao hawana dhamira safi zaidi ya kutanguliza maslahi yao.
"Nikikuhonga leo ujue sina nia njema, sitakuhudumia pindi nitakapoingia madarakani, nitaanza kwanza kutafuta namna ya kurudisha fedha zangu... hii ni vita ambayo CCM tunapaswa kuipinga kwa nguvu zote," alisema Sumaye.
MUUNDO WA SERIKALI
Akizungumzia muundo wa Serikali, alisema yeye ni muumini wa muundo wa serikali mbili siku zote na atendelea kusimamia ukweli huo.
"Haiwezekani ndani ya taifa hili tukawa na serikali tatu, hivi Rais wa Jamhuri ambaye anamiliki mali nyingi, akisema anamnyima Rais wa Tanganyika misaada nini kitatokea... huu ndio mwanzo wa kuondoa utulivu wetu, tuwe makini, tutaparanganyika," alisema Sumaye.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema wakati wa utawala wa awamu ya tatu, chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, walipambana vya kutosha, ikiwa ni pamoja na kuondoa kipengele cha takrima.
"Tumepambana vya kutosha dhidi ya rushwa, hata takrima tulihakikisha inaondolewa wakati ule baada ya kubaini uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulijumuisha madiwani, ndiko hali hiyo ilikuwa imejikita.
"Nakumbuka enzi za utawala wangu, niliagiza idara zote za serikali mikoani na wilayani kukutana kwa saa moja kujadiliana masuala ya rushwa na ugonjwa wa Ukimwi," alisema Sumaye.
MAWAZIRI MIZIGO
Akizungumzia utendaji kazi wa awamu yake, Sumaye alisema ndani ya Baraza la Mawaziri hakukuwa na mawaziri mizigo.
"Sikuwa na mawaziri mizigo kwenye utawala wangu, utaona hata umma kwa sehemu kubwa unakiri tulifanya kazi nzuri.
"Nakwambia ukiwa na mizigo unapaswa kuitua haraka sana kabla ya watu hawajakuona," alisema Sumaye.
WAPINZANI
Kuhusu vyama upinzani, Sumaye alisema vimekuwa na mchango mkubwa wa kuimarisha serikali katika utekelezaji wa mambo muhimu.
"Siku zote nimekuwa muumini mkuu wa upinzani, wamekuwa kiungo muhimu, natamani kuona wanaingia kwa wingi kwenye Bunge letu, michango yao mizuri...nawaomba waendelee hivi hivi wasirudi nyuma," alisema Sumaye.
MBOWE
Kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kwamba Katiba itapatikana kwa ngumi, Sumaye alisema kauli hiyo si nzuri, kwa sababu amani ikitoweka, si CCM wala CHADEMA watakaopona.
"Nimemsikia akiruka na helikopta zake huko mikoani na kusema atatumia nguvu, hivi jamani leo amani ikitoweka, CCM na CHADEMA watapona?" Alihoji Sumaye. Chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment