Wednesday, February 19, 2014

LOWASSA NA WENZAKE WATIWA KITANZINI-WAFUNGIWA KUGOMBEA UONGOZI CCM.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza uamuzi mzito dhidi ya wanachama wake sita ambao hivi karibuni waliitwa na Kamati Ndogo ya Maadili na kuwahoji kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2015.
CCM imewatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, hivyo kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wanachama hao wote sita walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya wakati jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo kali. Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za chama hicho inamaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha,” alisema Nnauye.
Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo hao, kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote watakuwa wakichunguzwa mienendo yao.
Nnauye alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni za kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema Nnauye.
Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali.”
Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.
Nnauye alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
CHANZO:MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment