Friday, February 21, 2014

KAMPENI BUNGE LA KATIBA ZAANZA CHINICHINI-Sitta na Membe wahusishwa.


Dodoma,
Wakati ratiba ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba, ikitarajiwa kutangazwa rasmi siku ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo, jana baadhi ya wajumbe walikuwa wakifanya kampeni za wazi ndani ya Ukumbi wa Bunge. Ratiba ya uchaguzi ilitarajiwa kutangazwa jana jioni na ingeonyesha ni lini Rais Jakaya Kikwete, atalizindua bunge hilo na kuelezea siku kamili ya uchaguzi wa viongozi wake.


Ndani ya ukumbi jana, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), alionekana akizungumza na wajumbe, jambo ambalo baadhi ya watu wamelitafsiri kuwa ni kufanya kampeni. Chenge ni mmoja wa makada wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.


Mwingine anayetajwa ni Mbunge wa Urambo Mashariki ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.


Wakati Chenge akiendelea na kampeni zake, Sitta alitumia muda mwingi kuzungumza na wajumbe ambao wengi walikuwa wakimfuata mahali alipoketi na baadaye, alionekana akiwazungukia wajumbe.


Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde, alisema hana jambo lolote la kufanya juu ya mapenzi yake kwa Sitta kwani ndiye anayeweza kuendesha shughuli hizo.


“Mimi Lusinde, kwa mapenzi yangu kabisa nasema kuwa kama jina la Sitta litachomoza basi lazima nimsaidie kuhakikisha anakalia kiti hicho kwa kuwa naona anaweza kuliko wengine,” alisema Lusinde.


Alisema kuwa bunge hilo limesheheni wataalamu wa sheria waliobobea na ambao kila mmoja anaweza kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu, lakini akasisitiza kwamba kwa kuwa anayetakiwa ni mmoja basi angetamani nafasi hiyo imwendee Sitta.


Mjumbe mwingine kutoka katika Bunge la Muungano ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa kumchagua Sitta ni sawa na kumsaliti Chenge ambaye ni jirani yake na wanakaa viti karibu bungeni.

Chanzo:Mwananchi.

No comments:

Post a Comment